1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mandela yuko taabani

Admin.WagnerD24 Juni 2013

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Nelson Mandela yuko katika hali mbaya sana hospitalini, lakini madaktari wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha hali yake inaimarika.

Nelson Mandela
Nelson MandelaPicha: picture-alliance/dpa

Ni taifa lililoko katika sala, raia wengi wa Afrika wanaendelea kutumaini kuwa Nelson Mandela anapata nafuu ya haraka. Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini amekuwa hospitalini tangu tarehe 8 Juni, akitibiwa kufuatia maambukizi ya mapafu, lakini madaktari wanasema afya ya Mandela, ambaye anajulikana kama Madiba, inazidi kuwa mbaya.

Raia wa Afrika wakisoma gazeti siku ya Jumatatu. Waafrika Kusini wengi wanoanekana kuanza kukubaliana na ukweli kwamba Mandela anaweza kuondoka muda wowote.Picha: Reuters

"Mabibi na mabwana, rais mstaafu Mandela, anaendelea kuwa katika hali mbaya hospitalini. Madaktari wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha ustawi wake na faraja. Tunavishukuru vyomba vya habari kwa msaada na kuendelea kuufahamisha umma katika wakati huu mgumu," alisema rais Jacob Zuma katika mkutano na waandishi wa habari asubuhi ya Jumatatu.

Afya yake kutoathiri ziara ya Obama

Zuma amesema yeye na makamu wa rais wa chama cha Africa National Congress, ANC, Cyril Ramaphosa walimtembelea Mandela usiku wa kuamkia leo. Lakini amekataa kutoa maelezo zaidi kuhusu afya ya Mandela, zaidi ya kusema kuwa yuko katika hali mbaya sana. Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kufanya ziara nchini Afrika Kusini wiki hii, lakini Zuma amesema kuwa kudorora kwa afya ya Mandela hakutaathiri ziara hiyo.

Kudorora kwa afya ya Mandela wikendi hii, ikiwa ni wiki mbili tangu alipolazwa akiwa katika hali mbaya lakini imara, kumeibadili hali kutoka kwenye kumuombea kupona haraka hadi kwenye kuanza maandalizi ya kumuaga. "Kama ni wakati wa yeye kuondoka, anaweza kuondoka, namuombea kwa Mungu ampokee vyema," alisema Petunia Mafuyeka, ambaye ni Nesi wakati akielekea kazini mjini Johannesburg.

Baadhi wataka aachwe apumzike

Kulikuwepo na wasiwasi miongoni mwa umma kuhusu jitihada za madaktari kurefusha maisha ya rais huyo wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, ambaye ni mmoja wa watu maarufu zaidi duniani katika karne ya 20. "Nina wasiwasi wanajaribu kumuweka hai, nadhani wanapaswa kumuacha aondoke," alisema Doris Lekakala, Meneja madai. Ameshakuwa mzee, waache tu mambo yachukuwe mkondo wake. Anapaswa kupumzika."

Wafanyakazi wa Posta wakiyapita magari ya vyombo vya habari yaliyoegeshwa nje ya hospitali alikolazwa Mandela.Picha: Reuters

Tangu alipostaafu mwaka 1999 baada ya muhula mmoja kama rais, Mandela amejiweka mbali na siasa, katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, na endapo atafariki kunatizamiwa kuwa na athari ndogo kisiasa. Mara yake ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa Julai mwaka 2010 wakati wa mashindano ya kombe la dunia.

Umma ulipata kumuona mara ya mwisho katika picha ya video iliyotangazwa na televisheni ya taifa mwezi April, wakati rais Zuma na viongozi wengine waandamizi wa ANC walipomtembelea nyumbani kwake. Wakati huo, chama cha ANC kiliuhakikishia umma kuwa Mandela yuko katika hali nzuri, ingawa picha hiyo ya video ilionyesha mtu mzee aliedhoofu, akiwa amekaa katika kiti bila hata kutikisika.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, afpe,ape
Mhariri: Saum Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW