1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mane aipeleka Senegal AFCON 2022

16 Novemba 2020

Senegal imekuwa timu ya kwanza kufuzu katika Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON 2022 baada ya Sadio Mane kufunga katika ushindi wao wa 1 – 0 dhidi ya Guinea Bissau Jumapili

Sadio Mané I Trikot Senegal
Picha: Celso Bayo/ZUMA/picture alliance

Senegal sasa ina pointi 12 katika mechi nne katika Kundi I na imejihakikishia moja kati ya nafasi mbili za kufuzu katika kundi hilo. Senegal ilipoteza dhidi ya Algeria katika fainali ya Kombe hilo nchini Misri mwaka jana. Kinyang'anyiro cha 2021 kilisogezwa mbele hadi Januari-Februari 2022 kwa sababu ya janga la virusi vya corona.

Mabingwa watetezi Algeria, Ghana na Tunisia zote zimeshinda mechi tatu kati ya tatu walizocheza za kufuzu na huenda wiki hii zikajiunga na Senegal katika tamasha hilo.

Algeria itacheza ugenini dhidi ya Zimbabwe leo baada ya kuifunga Zimbabwe 3 – 1 nyumbani wiki iliyopita ikisaidiwa na bao na asisti ya Royad Mahrez. Ghana itakuwa Khartoum kucheza na Sudan na Tunisia itapambana na Tanzania kesho. 

Senegal itakamilisha ratiba yake kati ya Machi 22 na 30 kwa kucheza ugenini dhidi ya Congo Brazaville na kuialika eSwatini. Congo ina pointi sita, Guinea-Bissau ina tatu na eSwatini haina kitu katika mapambano ya kufuzu pamoja na Senegal.

Algeria ndio mabingwa watetezi wa AFCONPicha: picture-alliance/AA/F. Batiche

Ushindi wa Congo leo ugenini dhidi ya eSwatini utaiweka katika nafasi nzuri ya kutinga fainali hizo ambazo walikosa kushiriki 2019.

Guinea ilitoka sare ya 1 – 1 na Chad katika Kundi A kumaanisha kuwa Guinea inaongoza kwa pointi nane baada ya mechi nne, lakini Mali inaweza kuwapiku kama watashinda kesho dhidi ya Namibia.

Comoros ilipiga hatua kubwa ya kutinga fainali za Afcon kwa mara ya kwanza baada ya ushindi wa 2 – 1 dhidi ya Kenya jana katika Kundi G.

Comoros hawajapoteza mechi mpaka sasa na wana pointi nane, Misri wana pointi tano, Kenya wana tatu na Togo wana moja. Huyu hapa Jacob Ghost Mulee kocha wa Harambee Stars akizungumza muda mfupi baada ya timu kuwasili Nairobi leo mchana ikitokea Moroni. Togo itaialika Misri kesho mjini Lome, na lazima ishinde ili iwe na nafasi nzuri.

Burundi ililifungua tena Kundi E baada ya ushindi wa 3 – 1 dhidi ya Mauritania. Morocco inaongoza kundi hilo ikiwa na pengo la pointi mbili dhidi ya Mauritania ambayo ina tano, Burundi nne na Jamhuri ya Afrika ya Kati tatu. Afrika ya Kati itaialika Morocco kesho

Rwanda kesho itakuwa na kibarua katika uwanja wa Kigali Nyamirambo dhidi ya Cape Verde. Timu hizi zilikwenda sare ya kutofungana 0-0 wiki iliyopita. Amavubi Stars wana mlima wa kupanda hawajashidna mechi hata moja katika kundi lao la F, wana alama 1, walikandikwa na Msumbiji 2-0, Cameroon ikawazaba 1-0. Cameroon inaongoza na alama 7, Msumbiji ya pili na alama 4 huku Cape Verde ikija kwenye nafasi ya 3 na alama 3.

AFP, AP, Reuters, DPA