1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manuwari za Umoja wa Ulaya sasa zitawakabili maharamia wa meli kutokea Somalia

Miraji Othman8 Desemba 2008

Umoja wa Ulaya sasa unaonesha meno yake makali dhidi ya maharamia wa meli wa Somalia

Maharamia wa Kisomalia wakiondoka kwenye meli ya Ukraine walioiteka nyara, MV FainaPicha: AP

Leo Umoja wa Ulaya unaanza shughuli za kupambana na maharamia wa meli katika mwambao wa Somalia. Manuwari sita na ndege tatu, chini ya Operesheni iliopewa jina la Atlanta, zitachukuwa mahala pa jeshi la Jumuiya ya NATO katika kuzilinda meli za kibiashara dhidi ya kuengezeka mashambulio ya maharamia katika mwambao wa Afrika Mashariki. Baraza la mawaziri la Ujerumani huenda likaamuwa hapo Disemba 10 juu ya kushiriki manuwari yake pamoja na hadi wanajeshi 1,400.

Karibu kila siku kuna habari za visa vya kuvamiwa meli katika mwambao wa Afrika Mashariki, hasa karibu na Somalia. Kinachotekwa nyara ni kila kitu kinachoelea majini, kutoka meli za matanga, zile za fahari zinazosafirisha watalii hadi za mizigo. Lakini kisa cha kijasiri kabisa ni kutekwa nyara ile meli kubwa ya kubebea mafuta inayoitwa SIRUS STAR. Kuna makampuni mengine ya meli yanayopitisha meli zao, kutokana na sababu za kiusalama, Ras ya Matumaini Mema huko Kusini mwa Afrika, badala ya Mfereji wa Suez, hivyo kuchukuwa wakati mrefu na pia kugharimia mafuta zaidi.

Katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa jumuiya ya kujihami ya NATO wiki iliopita, katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Jaap de Hoop Scheffer, alisema hali ya mambo ni kweli ya hatari:

" Utekeji nyara unazidi kuwa mbaya na umekuwa ni tatizo kubwa kwa misafara ya kimataifa ya meli, na sio tu katika eneo la Ghuba ya Aden, lakini mtu anaweza kusema duniani kote. Lakini pale mtu atakapolichukuwa eneo la Ghuba kama mfano, ninakupa tarakimu mbili: Kila mwaka inapita misafara 20,000 ya meli katika bahari hiyo, na kuvamiwa meli katika mwaka huu kumeongezeka kwa asilimia 300."

Hivi sasa Jumuiya ya NATO ina manuwari zake kadhaa katika bahari hiyo. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, alisema mkutano wa NATO uliofaywa Brussels umeleta maendeleo:

"Siku za karibuni kumeonyesha kwamba kuweko manuwari za NATO katika Pembe ya Afrika kumezuwia utekaji nyara mmoja au mwengine."

Manuwari hizo za NATO zinazisindikiza hasa zile meli zinazosafirisha misaada kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani hadi Somalia. Sasa zitaanza operesheni za nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zitachukuwa shughuli zilizokuwa zinafanywa na NATO. Mkuu wa diplomasia wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, anaoneka kuwa ameridhika, kwani anahisi operesheni hiyo itakuwa madhubuti na yenye meno makali. Lengo litakuwa kutishia, kuzuwia na kuzilinda, hasa meli zinazosafirisha misaada ya Umoja wa Mataifa.

Lakini Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya NATO zinatambua kwamba tatizo hilo halitatokomea kabisa duniani. Kwa hivyo, nchi za NATO zinafikiria kama baadae zitabidi zianzishe tena operesheni, na kama operesheni kama hiyo iwe ya muda mrefu. Kuna mambo mengi ambayo yatabidi yatanzuliwe kwanza. Kwa mfano, NATO na Umoja wa Ulaya zinatarajia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litowe mwangaza wa kisheria juu ya suali: Nini kitakachojiri pale maharamia watakapokamatwa. Serekali nyingi zinapendekeza kwamba Jumuiya ya NATO iende kwenye mzizi wa fitina na izizingire bandari za Somalia ambazo zinajuklikana kuwa ni maficho ya maharamia.

Lakini katibu mkuu wa Jumuiya ya NATO, Japap de Hoop Scheffer, anasema jumuiya hake haifikirii hivi sasa kuzizingira bandari hizo, kwa hivi sasa jambo hilo halimo katika ajenda ya NATO.

Hata hivyo, hayo ni kwa hivi sasa tu, kwamba uharamia unazidi duniani kote na hivyo kuengeza mbinyo kwa makampuni ya meli na jumuiya za kutoa misaada zichukuwe hatua. Basi yawezekana agizo la baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likabadilika.




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW