Magazetini.
4 Juni 2008Masuala yanayozungumziwa leo duniani kote ni mkutano wa mjini Rome ambapo wajumbe wanajadili njia za kupambana na tishio la njaa, na juu ya seneta Barack Obama.
Magazeti ya Ujerumani pia yanazingatia masuala hayo katika maoni yao.
Juu ya seneta Obama gazeti la Ostthüringer linasema vijana kati ya umri wa miaka18 na 35 , nchini Marekani wameweza kushuhudia kampeni ya seneta huyo kama hatua ya kihistoria na mwanzo mpya wa mustakabal wa nchi yao. Gazeti linasema vijana hao hawajioni kuwa ni sehemu ya chama bali wanajiona kuwa ni sehemu ya mchakato. Mhariri wa gazeti la Ostthüringer anasema vijana hao ni rika la Obama.
Mhariri huyo anaeleza kuwa hadi sasa hakuna mwanasiasa wa Marekani alieweza kuwahamasisha vijana wengi kama seneta Obama.
Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linatoa maoni juu ya mshindani wa Obama-seneta Hillary Clinton ambae kimsingi ameshindwa kufikia lengo lake.
Gazeti hilo linasema ,wamerekani waliotaka kushuhudia tukio la kihistoria katika nchi yao-yaani kumwona mwanamke wa kwanza akigombea urais, wameingiwa uchungu.Hatahivyo gazeti linaeleza kuwa, huo ni ujumbe mzuri kwa demokrasia ya Marekani. Tawala za kifamilia, iwe ni akina Bush au akina Clinton, siyo jambo linalotakiwa katika demokrasia.
Mkutano juu ya mgogoro wa chakula duniani unaohudhuriwa na wakuu wa nchi unaendelea mjini Roma. Gazeti la Der neue Tag limetoa maoni yake juu ya mkutano huo kwa kusema kuwa kuwapo kwa mgogoro wa chakula duniani ni kashfa.
Gazeti hilo linaeleza katika maoni yake kuwa miongoni mwa wanaowajibika, hakuna anaeweza kukwepa lawama, iwe katika nchi zinazokabiliwa na mgogoro huo au katika nchi tajiri za magharibi.