1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maombolezo ya Khamenei yaitikisa miji ya Iran

7 Julai 2026

Mitaa ya mji mtakatifu kwa Waislamu wa madhehebu ya shia wa Qom umefurika umma wa watu karibu milioni moja na nusu. Ni mara ya kwanza kwa Iran kushughudia maziko ya kitaifa makubwa tangu mwaka 1989.

Bango la picha ya Ayatollah Ali Khamenei katika mji wa Qom
Bango la picha ya Ayatollah Ali Khamenei katika mji wa QomPicha: Ahmadreza Taheri/ISNA/WANA/REUTERS

Wairan bado wanaendelea na shughuli za mazishi ya aliyekuwa kiongozi wa juu wa jamhuri hiyo ya Kiislamu Ayatollah Ali Khamenei. Umma wa maelfu ya Wairan umejitokeza hivi leo katika mitaa ya mji mtakatifu wa Qom kushiriki kwenye mfululizo wa shughuli za maombolezo zilizoingia siku yake ya nne.

Picha za video zilizorushwa na kituo cha serikali zimeonesha namna mitaa ya mji mtakatifu kwa Waislamu wa madhehebu ya shia wa Qom ulivyofurika umma wa watu karibu milioni moja na nusu. Wakiwa wamevalia mavazi meusi yanayoonesha alama ya kuomboleza kuondokewa na kiongozi wao wa juu Ayatollah Ali Khamenei aliyeuwawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel Februari 28.

Jeneza lenye mwili wa kiongozi huyo likiwa limewekwa katika msikiti wa Jamkaran kwenye mji huo wa Qom ambako kunapatikana maeneo muhimu ya ibada ya jamii ya Washia. Msikiti ulikolala mwili wa Khamenei inasadikiwa katika imani za madhehebu ya Shia kwamba aliwahi kupokelewa imamu wa 12 na wa mwisho wa shia Muhammad al Mahdi ambaye wanaamini siku moja atarejea kusimamisha haki ulimwenguni.

Waombolezaji wakishiriki sala maalum ya mazishi ya Khamenei katika msikiti wa Jamkran Picha: Office of the Iranian Supreme Leader/WANA/REUTERS

Picha za Khamenei na mwanawe aliyerithishwa nafasi yake ya kuiongoza Iran, Ayatollah Mojtaba Khamenei zimechapishwa kwenye mabango yanayooneshwa na waombolezaji. Imefanyika pia sala maalum ndani ya msikiti huo ikiongozwa na mmoja wa viongozi wa juu na mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa wahafidhina wa madhebu ya Shia ndani ya Iran, Abdollah Javadi Amoli mwenye umri wa miaka 93. Umma ulisikika ukitamka maneno ya kuilaani Marekani  kwenye ibada hiyo. Iran yajitayarisha kumzika Kiongozi Mkuu aliyeuawa huku wiki ya maombolezo makubwa ikianza.

Yanayoshuhudiwa kwenye mji mtakatifu wa Qom ndiyo yaliyojitokeza pia mjini Tehran zilikofanyika shughuli za maombolezo ya Khamenei yaliyoingia siku yake ya nne hivi leo na ikitarajiwa kwamba mwili huo utapelekwa pia Najaf na Karbala huko Iraq kabla ya kuwasili kituo cha safari yake ya mwisho nyumbani kwao katika mji mtakatifu wa Mashhad utakakozikwa tarehe 9 Alhamisi ambako watu milioni 35 wanatarajiwa kushiriki.

Ni mara ya kwanza kwa Iran kushughudia umma mkubwa kwenye maziko ya kitaifa tangu mwaka 1989 yalipofanyika mazishi ya mtangulizi wa Khamenei, Ayatolla Ruhollah Khomeini, aliyekuwa muasisi wa Jamhuri hii ya Kiislamu. Jenerali Qassem Soleimani ni nani?

Mara ya mwisho Iran kushuhudia mazishi makubwa yaliyokusanya mamilioni ya waombolezaji ni 1989 alipokufa Ayatollah Ruhollah Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya IranPicha: Mehdi Alavi/ISNA/AFP/Getty Images

Lakini wakati Wairan wakiwa kwenye dimbwi la simanzi na maombolezo kumeripotiwa shambulizi katika bahari ya Ghuba ya Uajemi lililolenga meli iliyokuwa ikisari kwenye Mlango Bahari wa Hormuz. Shambulio hilo ndilo la karibuni kabisa kwenye vita vya Iran na kituo cha televisheni cha Iran kimesema meli hiyo inayosafirisha gesi imeshambuliwa baada ya kupuuza miito ya tahadhari.

Inavyoonesha mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu yamesitishwa mpaka yatakapomalizika mazishi ya Ayatollah Ali Khamenei, ingawa muda mfupi uliopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa X akisema mazungumzo kuhusu makubaliano ya mwisho ya amani  na Washington hayatofanyika ikiwa vitisho vinaendelea. Hivi karibuni Rais Donald Trump alitoa vitisho kwa kusema atamaliza kazi ikiwa makubaliano hayatopatikana.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW