Maombolezo yaendelea nchini Korea kaskazini kufuatia kifo cha kiongozi wake Kim Jong Il
20 Desemba 2011Kama ishara ya kuonyesha kuwa mabadiliko katika utawala wa pekee wa kinasaba ulimwenguni yangali sawa, Kim Jong Un, mtoto wake mdogo marehemu Kim na ambaye ndiye mrithi wake, alitoa pia heshima zake akiwa pamoja na maafisa wakuu wa jeshi na wale wa chama cha wafanyakazi na kufanya kile chombo cha habari cha taifa kilitaja kuwa sherehe takatifu katika mji mkuu Pyongyang huku taifa nzima likiomboleza.
Mhadhiri mmoja wa jumba la makumbusho la kihistoria, Ri Ho Il ameliambia shirika la habari la AP kuwa watu wa Korea wana masikitiko makubwa kutokana na kifo hicho cha baba wa huruma wa taifa. Kwamba aliitetea furaha ya watu wake, na kufanya kazi yake usiku na mchana. Televisheni ya taifa ilionyesha jeneza la kioo ulikolazwa mwili wake Kim likizingirwa na maua. Alifunikwa na blanketi nyekundu, na kichwa chake kuwekwa kwenye mto mweupe. Jeneza hilo liliwekwa kwenye chumba cha ikulu ya ukumbusho ya Kumsusan, mahali ambako mwili uliokushwa wa babake mwanzilishi wa taifa Kim Il Sung umekuwa ukionyeshwa kwenye kioo tangu kifo chake mwaka wa 1994.
Kim Jong Il mwenye umri wa miaka 69, alifariki jana kutokana na mshutuko wa moyo ulosababishwa na kazi nyingi na uchovu kulingan vyombo vya habari nchini humo. Huku taifa hilo likiendelea na maombolezi ya siku 11, bendera zilipeperushwa nusu mlingoti katika vituo vyote vya kijeshi, viwanda, maeneo ya kibiashara, mashambani na majengo ya umma. Barabara za mji wa Pyongyang zilisalia kuwa tulivu lakini makundi ya watu yalikusanyika katika vituo mbalimbali kutoa heshima zao kwa Kim.
Maafisa wa Korea kaskazini wanasema hawatawalika wajumbe wa kigeni na hawatakubalia burudani lolote wakati wa kipindi cha maombolezo.
Punde baada ya kifo chake kutangazwa hapo jana, rais wa Marekani Barrack Obama alikubaliana na rais wa Korea Kusini kwa njia ya simu, Lee Myung Bak, kuchunguza kwa umakini mwelekeo wa matukio. Serikali ya japan pia ilisema iko chonjo kuhusu matukio yoyote yasiyotarajiwa. Jeshi la Korea Kusini liliwekwa katika hali ya tahadhari na watalaam wakaonya kuwa siku chache zijazo zinaweza kuwa kipindi muhimu kwa Kaskazini, ambayo ijapokuwa inasakamwa na usimamizi mbaya wa kiuchumi na baa la njaa la kira mara, ina jeshi thabiti linaloungwa mkono la watu milioni moja la laki mbili.
Korea kusini ilitoa rambirambi zake kwa watu wa Korea kaskazini lakini serikali ikasema hakuna ujumbe rasmi utakaosafiri kutoka Seoul hadi Pyongyang kutoa heshima zao. Kifo cha Kim huenda kikawa pigo kubwa kwa juhudi za marekani na wengine za kuishawishi Korea Kaskazini kuwachana na mipango yake ya silaha za kinyuklia.
Kuna hofu pia kuwa Kim Jong Un kwa vile ni mchanga bado na asiyewahikufanyiwa jaribio lolote, huenda akahisi anahitaji kujithihirisha katika jukwaa la kimataifa.
Marehemu Kim Jong Il alikuwa madarakani kwa miaka 17 baada ya kifo cha babake Kim Il Sung , na aliandaliwa kuurithi uongozi miaka kadhaa kabla ya hapo. Korea kaskazini ilifanya jariboo moja la kombora la masafa mafupi hapo jana, lakini maafisa wa Korea kusini wakaliona kama tu jaribio lao la kawaida.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed