1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Berlin ina nguvu kuliko chuki

28 Mei 2018

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia na kinachopinga wahamiaji nchini Ujerumani cha AfD kiliitisha maandamano mjini Berlin. Lakini ni mashabiki wake wachache tu waliojitokeza kuliko ilivyotarajiwa.

Deutschland - Berlin Gegendemo zu AFD Demonstration
Picha: picture alliance / Britta Pedersen/dpa-Zentralbild/dpa

Uhuru wa kufanya maandamano ni sehemu ya demokrasia. Maandamano na upinzani ni vielelezo vya malumbano ya kisiasa. Katika historia ya Ujerumani palikuwapo na wakati wa maandamano makubwa sana na pia wakati wa ishara za kisiasa na chembelecho ulikuwa ni wakati ambapo idadi kubwa ya watu walishiriki katika mazoezi ya kupiga kura.

Hapo jana maalfu kwa maalfu ya watu walishiriki kwenye maandamano mjini Berlin. Upande mmoja ulikuwa wa wale walioandamana kupinga Uislamu, kumpinga kansela Angela Merkel na kuonyesha chuki dhidi ya wakimbizi. Na katika upande mwingine walikuwapo wale waliotumia wasaa wa maandamano hayo ili kutetea maadili ya jamii ya uwazi. Kwa mujibu wa taarifa ya polisi ni mashabiki 5000 tu wa chama cha AfD waliojitokeza kwenye maandamano ya jana. Katika upande mwingine walisimama kidete watu 20,000 kuwakabili mashabiki wa chama hicho kinachowachukia waislamu na wakimbizi. Jambo la kutia moyo ni kwamba washiriki wa upande wa kutetea haki walikuwa vijana zaidi kuliko wafuasi na mashabiki wa AfD.

Wafuasi wa chama cha AfD kwenye maandamano ya mjini BerlinPicha: Reuters/H. Hanschke

Wito wa kwanza kutolewa na chama cha AfD kwenye maandamano hayo hapo jana ulikuwa juu ya kile walichoita upinzani, upinzani kwa sauti ya juu sana. Wito huo ulirudiwa mara kwa mara na uliwasilisha mambo mengi katika muda wa saa tatu wa kufanyika kwa maandamano ya watu hao wanaotumia hoja finyu za mrengo wa kulia ili kujijengea umaarufu.

Naibu kiongozi wa wabunge wa AfD kwenye bunge la Ujerumani Beatrix von Storch anataka Wajerumani wenye nasaba za uhamiaji wanyimwe uraia wa Ujerumani na wasipewe pasipoti za Ujerumani. Naye mwenyekiti wa chama hicho kinachojiita chama mbadala, Jörg Meuthen amemkashifu kansela Angela Merkel kwa kumwita kuwa ni kasisi mkuu wa dhihaka ya mamlaka. Bwana huyo alitoa madai juu ya kunajisiwa kwa utamaduni wa Ujerumani! Na katika muda wote wa saa tatu kwenye maandamano ya jana zilisikika kauli za kuupinga Uislamu kutoka kwa viongozi na mashabiki wa AfD.

Katika upande wa pili walisimama watu 20,000 kupinga ubaguzi na kwenye mabango yao watu hao walisema "mji wa Berlin una nguvu zaidi za kupinga uzalendo wa kujikweza". Sehemu kubwa ya jamii ilijitokeza kuonyesha mchanganyiko wa nasaba za binadamu. Msimamo wa waungwana hao 20,000 ulileta picha nzuri ya maandamano ya hapo jana mjini Berlin.  Licha ya keleke nyingi maandamano yalifanyika kwa amani chini ya jicho la walinzi wa usalama. Lakini hiyo pia ni sehemu ya demokrasia.

Mwandishi: Zainab Aziz/ Strack, Christoph

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman      

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW