Kuaga kwa Spika na mgogoro wa bunge
10 Septemba 2019John Bercow alikuwa mtukutu, fasaha wa kuzungumza, na alikuwa zaidi ya mwenyekiti alieshughulikia tu ajenda na kudhibiti matusi. Alijieleza katika tangazo lake la kujiuzulu kuwa yeye ni mtetezi wa wabunge wa kawaida, mtu aliehakikisha kuwa haki za bunge haziondolewi na maafisa wa juu kwenye benchi la serikali. Lakini hata katika kumsifu Spika na uongozi wake migawanyiko katika siasa za Uingereza ilidhihirika wazi.
Wakati upinzani na wahafidhina wenye msimamo wa wastani walikuwa na maneno mazuri kwa John Bercow, atakaeachia nafasi hiyo mwishoni mwa Oktoba, wengine miongoni mwa wabunge wa chama cha Conservative walionyesha dharau ya waziwazi. Wanadhani spika huyo alikuwa anaupendelea upinzani. Husuani, amesimamia haki za wabunge dhidi ya serikali ya vitisho na inayohanikiza.
Mashambulizi dhidi ya utaratibu wa bunge
Wahafidhina wa mrengo mkali wa kulia hata hivyo, walitaka kisasi na hivyo kutupilia mbali utamaduni kwamba hakuna upinzani kwa spika katika jimbo lake. Vita kati ya serikali na bunge vimekuwa vikali sana kiasi kwamba wafuasiwa Boris Johnson wako tayari kutumia kila njia kulipuuza bunge na kupitisha mpango wa Brexit wa waziri mkuu huyo.
"Tunalidhoofisha Bunge na kujihatarisha sisi wenyewe," Spika Bercow aliwaambia wabunge, kabla hawajalaazimishwa kuchukuwa likizo ya wiki tano iliyowekwa na waziri mkuu. Lakini yule ambaye onyo hili linaelekezwa amefunika masikio yake. Johnson angependelea kuongoza kwa namna ya watawala wa kimabavu mfamo wa Urusi, Uturuki na kwingineko, bila kuingiliwa na wabunge.
Kampeni ya propaganda dhidi ya wabunge
"Wasaliti wa watu" ni maneno yalioandikwa kwenye mabango ambayo yameonyeshwa kwa wiki kadhaa katika wilaya ya serikali ya Westminster. Chaguo la maneno hayo ya udanganyifu linatoka kwa vyombo vya habari vinavyoegemea mrengo mkali wa kulia, ambavyo kwa pamoja na serikali, vinawashawishi raia kwamba bunge ni mahala pasipo na maana, ambako muda unapotezwa bure badala ya kutekeleza matakwa ya Brexit ya walio wengi haraka iwezekanavyo. Kuwatweza wabunge, kuwaita waoga, washenzi na watoro, imekuwa sehemu ya mkakati wa Boris Johnson.
Na kwa kufanya hivyo, analiweka shoka kwenye mizizi ya demokrasia ya bunge. Wawakilishi wa watu siyo watekelezaji tu wa matakwa ya walio wengi katika majimbo yao. Wanasimamia maslahi ya raia wote na kile kilicho bora kwao kwa kadri ya ufahamu wao na imani. Hata kama walio wengi mjini Nottongham wakichagua kuruka kutoka kwenye ndege, ni wajibu wa mwakilishi wao kuwaeleza kwamba hakuna parachuti kwenye ndege hiyo. Na ikiwa bado watataka kuruka, awazuwie ikibidi.
Hicho ndicho walichojaribu kufanya wabunge kwenye Baraza la Wawakilisji kupitia sheria yao dhidi ya Brexit isiyo na makubaliano. Wengi wao yumkini walipuuza uzito wa kuondoka Umoja wa Ulaya wakati walipopigia kura utekelezaji wake zaidi ya miaka miwili iliyopita. Lakini sasa imedhihirika kuwa sumu kali ya kisiasa inatafuna siasa za Uingereza kutokea ndani. Na wabunge wanakashifiwa hadharani kwa juhudi zao za kuzuwia kishindo cha kisiasa na kiuchumi. Matusi na vitisho vya kuuawa katika mitandao ya kijamii vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
Taifa mama la demokrasia linajikongoloa lenyewe
Uingereza mara zote imejivunia umri wa taasisi zake, tamaduni zake na wakati mwingine sheria zake tata. Sifa yake kama taifa mama la demokrasia isiyoyumba, ilikuwa sehemu ya taswira ya Uingereza, sehemu ya sifa yake ya kisiasa nje ya nchi. Tangu kuanza kwa mgogoro wa Brexit hata hivyo, Waingereza walianza kupoteza sifa ya kuongozwa kwa busara na utashi. Na sasa majirani waliotamauka wanaitazama serikali mjini London ikidhoofisha taasisi zake za kidemokrasia, ikiharibu sifa yake na kuufanya utendaji wake kuwa mgumu zaidi.
Wabunge katika baraza la wawakilishi wamelaazishwa kwenda likizo na hawawezi kufanya chochote hadi siku ya Brexit. Wamejaribu kila kitu kuifunga mikono ya Boris Johnson. Lakini iwapo sheria mpya dhidi ya Brexit ya mparaganyiko ni imara vya kutosha kumdhibiti waziri mkuu huyo ni jambo lisilo na uhakika.
Zaidi ya yote, Bunge halina ulinzi dhidi ya kuwekwa kando. Katika wiki zijazo waziri mkuu Johnson anaweza kufanya chochote anachotaka mjini London, kwa sababu hakuna usimamizi wa kidemokrasia. Na hiyo ni hali hatari zaidi ya mambo kwa mkuu huyo wa serikali ambaye yuko kwenye mkondo wa maangamizi.