1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Changamoto kubwa zamsubiri Buhari

Admin.WagnerD1 Aprili 2015

Kuchaguliwa Muhammadu Buhari kuwa Rais nchini Nigeria ni ushindi wa demokrasia nchini humo. Hayo anasema mwandishi wetu Thomas Mösch katika maoni yake.

Wahlkampf in Nigeria 2015 Muhammadu Buhari
Picha: AFP/Getty Images/P. Utomi Ekpei

Ushindi wa Mohammadu Buhari hauna maana kwamba kuchaguliwa kwake ni jambo maalumu bali kwa mara ya kwanza tokea kurejea demokrasia ,mabadiliko yamefanyika nchini Nigeria.

Ni hadi hivi karibuni tu kwamba watu wengi nchini Nigeria hawakuamini iwapo ingeliwezekana kwa chama kilichokuwa kinatawala, PDP kilichokuwa na nguvu kubwa, kingelishindwa katika uchaguzi. Isingekuwa vigumu kwa chama hicho kufanya njama ili kupita katika uchaguzi. Na ndiyo sababu kwamba uchaguzi wa Nigeria safari hii ulikuwa wa kusisimua sana.

Mabadiliko ya uongozi yafanyika kwa amani

Kutokana na ukweli kwamba,mabadiliko ya uongozi yamefanyika kwa amani, tunaweza kusema kuwa demokrasia imepiga hatua kubwa nchini Nigeria.Na kwa nini safari hii mambo yalikuwa tofauti?

Hatua ya kwanza muhimu ni uamuzi wa vyama muhimu vya upinzani kuungana .Na la muhimu zaidi ni kwamba vyama hivyo vilikubaliana kuwa na mgombea wa pamoja. Ni kutokana na mkakati huo kwamba iliwezekana kwa mgombea wa vyama vya upinzani Muhammadu Buhari kujijenga miongoni mwa wapiga kura siyo tu katika ngome yake kuu-yaani katika jimbo la Waislamu kaskazini mwa Nigeria. Bali pia aliweza kujiimarisha katika sehemu zingine za Nigeria, na hasa kusini magharibi.

Mkuu wa idhaa ya DW-Haussa Thomas Mösch.Picha: DW

Jonathan alifanya ajizi katika usalama

Lakini pia inafaa kutilia maanani kwamba Rais Goodluck Jonathan mwenyewe alimsaidia Buhari katika kushinda uchaguzi. Jonathan hakutafuta njia ya mawasiliano na watu wa kaskazini mwa Nigeria. Ushahidi wa wazi ni jinsi alivyolishughulikia suala la magaidi wa Boko Haram .

Jonathan alianza kuwakabili magaidi hao kwa nguvu zake zote baada ya kutanabahi kwamba ushindi wake katika uchaguzi ulikuwa mashakani. Kutokana na kushindwa kuwakabili magaidi wa Boko Haram kwa muda mrefu, alisababisha kura za baadhi ya Wakristo ziende kwa Buhari.

Vijiji vingi vilivyotekwa na Boko Haram hapo awali vilikuwa vya Wakristo. Idadi kubwa ya wasichana waliotekwa nyara na Boko Haram mwaka mmoja uliopita walikuwa Wakristo. Watu wengi nchini Nigeria walitambua kwamba Jonathan hakuweza kuwapa usalama.

Changamoto kubwa kwa Buhari

Hata hivyo mshindi wa uchaguzi Mohammadu Buhari sasa anapaswa kuanza kazi ya kuzikabili changamoto kubwa. Nigeria sasa inapitia kipindi kigumu . Uchumi wa nchi hiyo unategemea mauzo ya mafuta. Na bei ya bidhaa hiyo imeanguka kwenye soko la dunia. Buhari pia anapaswa kuyaendeleza mapambano dhidi ya magaidi wa Boko Haram. Buhari anaetokea kaskazini mwa Nigeria anatambua kwamba kuwashinda Boko Haram hakutakuwa mwisho wa matatatizo ya sehemu hiyo. Sehemu hiyo inahitaji maendeleo ya uchumi .

Ufisadi pia ni uwanja mwingine wa mapambano kwa Buhari. Ni uwanja uliopanuka sana wakati wa utawala wa Goodluck Jonathan.

Changamoto nyingine kubwa kwa Buhari ni kwamba yeye ni Jenerali mstaafu. Sasa anapaswa kuthibitisha kwamba ataikumbatia demokrasia kifuani.Aliemtangulia miaka mingi iliyopita,Olusegun Obasanjo alijikwaa juu ya suala la demokrasia.Mara kwa mara alirudi kwenye tabia za kijeshi.Haki za binadamu ziliachwa nyuma.

Mwandishi: Mösch Thomas.

Mfasiri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Mohammed Abdul-rahman