Maoni: Demokrasia ya Afghanistan imegeuka ya kadri
1 Septemba 2021Heiko Maas amekabiliwa na uhalisia huo mpya haraka sana. Waziri huyo huyo wa mambo ya nje ambaye miezi michache tu iliyopita aliondoa uwezekano wa kundi la Taliban kuchukuwa madaraka haraka, hivi sasa anajaribu kufikia maelewano na washindi hao.
"Hakuna njia yoyote ya kukwepa mazungumzo na Taliban, maana hatuwezi kumudu hali ya ukosefu wa utulivu Afghanistan," Maas alisema Jumanne mjini Doha, moja ya vituo vya ziara yake.
Soma pia: Merkel asema jumuiya ya kimataifa lazima ikubali kuzungumza na kundi la Taliban
Hata kufunguliwa tena kwa ubalozi wa Ujerumani mjini Kabul ni jambo linalozingatiwa. Waziri huyo wa mambo ya nje anaharakisha kusema kwamba hii haitamaanisha kuitambua Taliban chini ya sheria ya kimataifa.
Lakini matamshi ya kidiplomasia kama hayo hayafichi hali halisi ya kutapatapa. Ni mtanziko ule ule wa zamani: Ikiwa unataka kuwa na ushawishi wowote katika nchi, hata kama ni kutoa msaada wa kibinadamu, inakubidi uwe na mawasiliano na wanaotawala nchi hiyo, bila kujali unavyowafikiria.
Mtanziko wa wimbi jipya la wakimbizi
Turudi kwenye uhalalishaji wa Maas wa mazungumzo na Taliban, kwamba huwezi kumudu ukosefu wa utulivu Afghanistan. Mwanzoni inasikika kama kilele cha unafiki. Mtu anaweza kujiuliza je, utulivu miongoni mwa Wataliban unapaswa bado kuwa bora kuliko machafuko?
Lakini hoja ya utulivu ndiyo hasa aliyoisikia tena na tena Maas wakati wa ziara yake. "Hatupaswi kuruhusu mporomoko wa kiuchumi. Hauko katika maslahi ya yeyote," alionya waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Shah Mehmood Quereshi, kwa mfano, ambaye nchi yake inashiriki mpaka wenye urefu wa karibu kilomita 2,500 na Afghanistan.
Soma pia: Wanajeshi wa Ujerumani kuendelea kuwepo nchini Afghanistan
Quereshi anafikiria kimsingi juu ya wimbi jipya la wakimbizi. Huo ndiyo wasiwasi mkubwa siyo tu mjini Islamabad, bali pia Tehran, Ankara, Berlin na miji mikuu ya mataifa ya Ulaya.
Hakuna kurudia yaliojitokeza 2015
Wakati wa kampeni za uchaguzi nchini Ujerumani, mgombea wa ukansela wa vyama vya muungano wa kifahidhina Armin Laschet, alionya kuhusiana na Afghanistan kwamba hali kama ya mwaka 2015, wakati mamia kwa maelfu ya wakimbizi walipowasili ndani ya miezi michache, hasa kutoka Syria, haipaswi kuruhusiwa kujirudia.
Kimsingi mataifa yote ya Ulaya yanakubaliana kwamba ni muhimu kuzuwia wimbi jipya la wakimbizi. Nchini Ufaransa kwa mfano, ambako mgombea wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen, anauwezekano wa kujinyakulia alama kuhusiana na suala la uhamiaji katika uchaguzi wa rais mwaka ujao; nchini Denmark ambako wa chama tawala cha Social Democratic kinalenga kuwa na sera kali hasa kuhusu uhamiaji; nchini Austria ambayo haitaki kuchukuwa hata mkimbizi mmoja wa Afghanistan; na katika mataifa yote eneo la Ulaya Kati-Mashariki ambayo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya, yanayokataa mgawanyo wa wakimbizi wanaotambuliwa rasmi. Hivyo, utulivu nchini Afghanistan unageuka kuwa suala la maslahi ya juu kabisaa.
Soma pia:Wanajeshi wanne wa Ujerumani wauliwa Baghlan karibu na Kundus nchini Afghanistan
Upenyo wa Ujerumani ni mdogo
Lakini siyo kwa gharama yoyote. Heiko Maasa anatumai kutumia nyenzo ya msaada wa kiuchumi kuishawishi Taliban kukubali muafaka kuhusu haki za binadamu. Ni nyenzo fupi tu: Taliban hawana uwezekano wa kujifanya wamebadilika maadamu wanaweza kupata ufadhili wa mataifa ya magharibi. Kama kweli wamebadilika, kama waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Quereshi alivyomuambia mwenzake wa Ujerumani, inasalia kuwa siyo chochote zaidi ya matumaini kwa sasa. Na mataifa mengine kama China na Urusi hayatoi masharti yoyote kwa Kabul. Hivyo njia ya kupenya kwa diplomasia ya Ujerumani inasalia kuwa finyu.
Ni mwisho mchungu: Ujerumani na mataifa mengine, walilifurusha kundi la Taliban miaka 20 iliyopita, na walitaka kuleta demokrasia na haki za binadamu nchini Afghanistan. Na hivi sasa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, anafuta maelewano na watawala wa zamani na wapya, ili kunusuru kinachoweza kunusurika. Lakini hakuna kingine cha kufanya.