1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: FIFA ni kisa cha kuvunja matumaini

28 Mei 2015

Maafisa kadhaa wa FIFA wamekamatwa, na mamlaka nchini Uswisi zinachunguza juu ya utoaji wa zabuni za uenyeji wa mashindano ya kombe la dunia mwaka 2018 na 2022. Imetosha, anasema mhariri wa michezo DW Stefan Nestler.

FIFA Sepp Blatter Korruption Ermittlungen Verhaftungen Symbolbild
Picha: Reuters/A. Wiegmann

FIFA imejaa rushwa, kuanzia ngazi ya juu kabisaa ya shirkisho hilo. Baada ya matukio ya Jumatano, ambapo maafisa kadhaa wa FIFA walikamatwa mjini Zurich, ni dhahiri kwa kila mmoja. maafisa hao wametuhumiwa na wachunguzi wa Marekani kwa kukubali zaidi ya dola milioni 100 katika hongo, ili kutoa upendeleo kuhusiana na haki za utangazaji na masoko katika soka la Amerika ya Kaskazini, Kati na Kusini.

Miongoni mwa waliokamatwa, ni wawili kati ya makamu nane wa rais wa kamati ya uongozi wa FIFA, ambayo ndiyo chombo muhimu zaidi cha shirikisho hilo la kandanda dunini. Moja wao ni Jefferey Webb, rais wa shirkisho la vyama vya kandanda vya Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF), ambaye ni mshirika wa karibu wa rais wa FIFA Sepp Blatter. Mkuu huyo wa FIFA raia wa Uswisi hata hivyo hayuko kwenye orodha ya wanaochunguzwa, inavyoonekana.


Gamba la ulinzi lisiloonekana

Hilo halishangazi. Katika miaka 17 ya uongozi wa Blatter katika FIFA - kila inapabainika kuwa maafisa wa shirikisho hilo wamechukuwa hongo - Blatter mara zote hutoka msafi. Ni kama vile ana gamba lisiloonekana la ulinzi. Ni mara moja tu alipoingia matatizoni, ilipodhihirika kuwa alifahamu kuhusu hongo iliyotolewa kwa watendaji wa FIFA na mshirika wa masoko wa FIFA, ISL, katika kazi yake kama katibu mkuu wa FIFA.

Shirika hilo la Blatter lilisema wakati huo kwamba pesa hizo zilikuwa "kamisheni" ya haki na FIFA ilifanikiwa kuzima kesi dhidi yao mwaka 2010 baada ya kulipa mamilioni katika fidia. Zaidi ya hapo, anachokifanya tu Blatter ni kupuuza tu kila mgogoro. Na imekuwepo michache, ya karibuni zaidi ikiwa juu ya utoaji wa zabuni za uenyeji wa michuano ya kombe la dunia kwa Urusi na Qatar kwa miaka ya 2018 na 2022. Serikali ya Uswisi sasa inachunguza michakato hii kubaini kama kulikuwepo na rushwa ndani yake.

Hakuna utamaduni wa kujitathmini

Kwa kuzingatia haya yote, ni vigumu kufikiri kwamba Blatter anaweza kuchaguliwa tena kwa mara ya tano kuwa rais wakati wa mkutano mkuu wa FIFA kesho Ijumaa. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 79 anaweza kutegemea tu kura atakazozipata kutoka Afrika na Asia, na pia mataifa ya Amerika. Mataifa ya Ulaya, ambayo Blatter alitaka kuyaondoa, yamedhihirika kuwa chui asiye na meno.

Katika shirika linaloendeshwa kwa kufuata msingi bora ya uongozi, Blatter angekuwa amekwisha laazimishwa kukabidhi barua yake ya kujiuzulu. Na kama angekuwa na hisia zozote za kimaadili, angefanya hivyo mwenyewe. Lakini FIFA ni shirika lililochafuka. Nini kinafaa kufanyika kabla halijasafishwa? Hakuonekani kuwepo na utamaduni wa kujitathmini, licha ya kuwa na kamati ya maadili ya FIFA. Eneo zima linapaswa kufungwa.

Mwandishi: Nestler Stefan
Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Josephat Charo