MAONI: G20 yakabiliwa na mtanziko
20 Machi 2017Haya si matokeo aliyoyatarajia waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble. Mwanzoni mwa mkutano wa mawaziri wa fedha wa mataifa ya G20 mjini Baden Baden, mwenyeji wa mkutano huo bado alishawishika kwamba sera ya pamoja ingeafikiwa pamoja na Marekani. Ahadi ya kuunga mkono biashara huru na kupinga hatua za kuyalinda masoko ya mataifa binafsi ilitarajiwa kujumuishwa katika tamko la mwisho la pamoja, kama ilivyo desturi baada ya mikutano ya aina hiyo.
Hata hivyo waziri Schäuble alishindwa kupata muafaka na mwenzake wa Marekani, Steven Mnuchin. Walichoweza kukubaliana ni taarifa dhaifu kwamba walikuwa wakishirikiana kuimarisha mchango wa biashara kwa uchumi wa nchi zao. Ahadi ya juu juu tu.
Je vita vya kibiashara vinakaribia?
Angalau mkutano wa Baden-Baden umeweka bayana jambo moja: Timu mpya katika ikulu ya Marekani inaonekana kufanya kazi. Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema wazi katika mkutano wake na kansela wa Ujerumani, Angela Merkel: Wajumbe wa Ujerumani wamefanya kazi nzuri zaidi kuliko wale wa Marekani na kuwataka Wamarekani watie bidii zaidi. Mkutano wa Baden-Baden unatupa kionjo cha maana halisi ya kauli hii. Hata Wolfgang Schäuble, mwanasiasa mwenye uzoefu na ujuzi wa kupanga mikakati hakuweza kuuvunja ukuta uliowekwa na Marekani.
Hata hivyo kuuleza mkutano wa waziri Schäuble kuwa haukuleta tija haitakuwa haki. Mikutano ya aina hii mara kwa mara haiwi rasmi; nyaraka za mwisho hazina mafungamano ya kisheria, lakini zinaweza aina fulani ya msingi kwa kazi inayoendelea ya mataifa ya G20.
Na hata kama katika miaka iliyopita viongozi walikuwa wakiahidiana wataimarisha biashara huru na kupunguza vikwazo, mwenendo kuelekea ulinzi wa masoko binafsi kwa kweli umekuwa bayana kwa muda sasa. Tangu mwaka 2008 Shirika la Biashara la Kimataifa, WTO, limeorodhesha hatua zaidi ya 2,000 zinazokwamisha biashara. Ikizingatiwa nchi za G20 zinawakilisha asilimia 80 ya biashara jumla duniani, ni wazi kabisa kwamba hawatimizi ahadi zao.
Vipi kuhusu Afrika?
Mjadala kuhusu sera ya biashara pia uliugubika baadhi ya ufanisi ambao kundi la G20 lilifaulu kuuwasilisha. Maendeleo mazuri yamepatikana, kwa mfano, na wale wanaoshughulika na kuhakikisha kuna uwazi katika shughuli za kifedha, au kutozwa kodi makampuni makubwa ya kimataifa, na Wamarekani pia walishirikishwa katika hilo. Halafu kuna mpango mpya wa waziri Schäuble kuhusu bara la Afrika: ulinzi zaidi kwa wawekezaji binafsi kuwahimiza waondoshe wasiwasi wao kuhusu kufadhili miradi barani Afrika. Ni makubaliano jumla hapa pia, ingawa hata hivyo mpango huu sio mapinduzi makubwa.
Mwisho wa mkutano huo wa siku mbili, hakuna aliyekuwa na shauku na jambo hilo. Swali pekee linaloulizwa tena na tena lilikuwa: Je tunaelekea katika vita vya kibiashara? Ni suala ambalo si la kupuuzwa.
Mwandishi:Böhme, Henrik
Tafsiri:Josephat Charo
Mhariri: Mohammed Abdulrahman