1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Hotuba ya Netanyahu Marekani

4 Machi 2015

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa na lengo moja tu alipolihutubia Bunge la Marekani- kuitanabahisha Marekani juu ya hatari ya kufikia mapatano na Iran. Lakini pana tatizo kwa Netanyahu.

USA Washington Rede Benjamin Netanjahu Kongress
Picha: Reuters/G. Cameron

Lengo la Waziri Mkuu wa Israel lilikuwa kuionya Marekani dhidi ya kufikia mapatano ya hatari na Iran kutokana na mazungumzo yanayofanywa baina ya Iran, Marekani na nchi nyingine tano. Ni lengo linalofahamika, lakini pana tatizo moja.

Iwapo pana taasisi inayohakikisha kwamba utawala wa Obama hauingii katika mapatano ya hatari na Iran, basi ni Bunge la Marekani linalodhibitiwa na wajumbe kutoka chama cha Republican.ambo hilo lilikuwa wazi kabisa kwa Waziri Mkuu wa Israel tokea mwanzoni alipoingia katika ukumbi wa Bunge na kuwahutubia wabunge wa mabaraza yote.

Rais ObamaPicha: Reuters/K. Lamarque

Marekani ni mlinzi thabiti wa Israel

Lakini ukweli ni kwamba Israel wakati wote inaungwa mkono thabiti na pande zote mbili yaani vyama vya Demokratic na Republican. Na Sera hiyo imekuwapo kabla hata Netanyahu hajawa Waziri Mkuu wa Israel. Inapohusu Israel, wakati wote pamekuwapo mwafaka wa kisiasa baina ya vyama hivyo.

Hata kabla ya Netanyahu na Spika wa Bunge kutoka chama cha Republican kula njama za kumtenga Rais Obama, wabunge wengi wa vyama vya Republican na Demokratik walishasema siku nyingi kuwa hawatayakubali mapatano yoyote na Iran yanayoweza kuwa hatari kwa usalama wa Israel. Hata Netanyahu mwenyewe anayajua hayo vizuri sana.

Siku zote Maseneta wamekuwa macho

Kwa mfano kwa muda wa miaka mingi Seneta wa chama cha Republican, John McCain, amekuwa anaukosoa utawala wa Obama juu ya suala la Iran. Na jana tu Seneta wa chama cha Obama, Demokratik, Chuck Schumer alisema haiamini Iran.

Obama anaweza kukosolewa kwa haki kabisa,lakini yeye ni mwanasiasa anayetambua hali halisi. Ndiyo kusema anajua fika kwamba mapatano yoyote na Iran yanayoweza kuyahatarisha maslahi ya Israel, hayatakubalika.

Mwandishi wa maoni kutoka DW Michael KniggePicha: DW/P. Henriksen

Jee ni sawa kuuuliza iwapo Baba Mtakatifu ni mkatoliki?

Ndiyo sababu alichokuwa anajaribu kukifanya Netanyahu hapo jana kilikuwa sawa na kuuliza iwapo Baba Mtakatifu ni Mkatoliki!

Lakini zaidi ya hayo Netanyahu jana hakuonyesha heshima inayostahili kwa Rais Obama na kwa wabunge wa Marekani. Hotuba ya Netanyahu pia imeonyesha ishara kwamba Waziri Mkuu huyo wa Israel hawaamini wabunge wa Marekani.

Ni utovu mkubwa wa heshima kwa Netanyahu kusimama mbele ya wabunge wa Marekani na kuanza kuzibeza juhudi anazozifanya Rais Obama. Kwa ufupi, hotuba ya Netanyahu haikuleta tija hata chembe. Vipi mtu kama Netanyahu anathubutu kuonyesha ujeuri kwa nchi iliyokwishaipa Israel zaidi ya dola zaidi ya Bilioni 120 tokea nchi hiyo iuundwe mnamo mwaka wa 1949.

Mwandishi: Knigge Michael

Tafsiri: Mtullya abdu.

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW