Maoni: Jamii ya kimataifa iisaidie Nigeria
19 Mei 2014Ishara iliyotolewa na mkutano huo wa Paris ni njema. Hatimaye, Nigeria na majirani zake wako tayari kushirikiana dhidi ya Boko Haram. Imebainika wazi katika wiki za hivi karibuni kwamba Nigeria pekee haiwezi kulikabili tatizo hili.
Lakini lazima isemwe kwamba uamuzi huu wa Paris umechelewa mno na una mapunfugu yake. Boko Haram imekuwa ikiendesha harakati zake ndani ya Nigeria na kwenye mataifa jirani ya Niger, Cameroon na, yumkini, hata Chad, kwa muda mrefu sasa. Bado kuna mashaka ikiwa kweli serikali zote zilizoshiriki kwenye mkutano huo wa Paris zitachukuwa hatua za dhati dhidi ya kundi hilo.
Shinikizo dhidi ya Niger
Hali ya usalama nchini Niger ni mbaya sana, na serikali mjini Niamey inamuangalia jirani yake wa kusini kwa wasiwasi mkubwa. Niger na Nigeria zimeungana kwa mengi: zina mpaka wa pamoja wenye urefu wa kilomita 1,500, na raia wao wanazungumza lugha moja huku wakiwa na mafungamano makubwa ya kibiashara.
Maelfu ya Wanigeria wanaohofia mashambulizi ya Boko Haram wamekimbia kwenye jimbo la Diffa nchini Niger, lililo umbali wa kilomita 1,400 kutoka mji mkuu Niamey, lakini ulio kando tu ya mji wa Borno nchini Niger.
Ni kwenye mji huo ndiko Boko Haram wanakopata vijana wapya wa kuwaingiza kwenye mapambano yao - hawa ni vijana wadogo wa kimasikini, ambao wako tayari kuyaingiza maisha yao hatarini kwa fedha kidogo tu.
Mara kadhaa, vyombo vya usalama vya Niger vimeripoti kuwakamata viongozi wa Boko Haram na kuzuia mashambulizi yao.
Ufaransa haitaki kujiingiza tena
Mapambano dhidi ya Boko Haram ni mabaya pia kwa Ufaransa. Baada ya kufanikiwa kudhibiti ugaidi nchini Mali, ambako kulikuwa na faida pia ya kumlinda jirani Niger, serikali mjini Paris haitaki kufungua uwanja mpya wa vita.
Mshirika wa Ufaransa nchini Mali, dikteta wa Chad Idriss Deby, anaweza pia kuwa na msaada mkubwa katika kupambana na Boko Haram. Hakuna kitu ambacho Deby anakiogopa kama kuwa na kundi la waasi asiloweza kulidhibiti kwenye eneo lake.
Mji mkuu wa Chad, N'Djamena, umetenganishwa na upande wa kaskazini wa Nigeria kwa sehemu ndogo tu ya Cameroon. Mashambulizi na utekaji nyara wa mara kwa mara kwenye eneo hilo la Cameroon, tukio la karibuni zaidi likiwa ni lile lililotokea siku moja kabla ya mkutano wa Paris, yanaonesha wazi kwamba serikali mjini Yaounde haina tena uhakika wa usalama kwenye ardhi yake yenyewe.
Hii maana yake ni kwamba serikali hiyo pia ina maslahi yake makubwa katika kushirikiana na Nigeria.
Tatizo ni kuwa utayarifu huo umekuwa shida sana kuushuhudia. Rais Paul Biya wa Cameroon amekuwa akisisitiza kuwa ni jukumu la Nigeria pekee kuwakabili wanamgambo wa Boko Haram, kwani kundi hilo linafanyia shughuli zake kutokea kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Mwandishi: Thomas Mösch/DW Kihausa
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman