Maoni: Jeshi la Ujerumani lilipoteza dhima yake Kunduz
7 Oktoba 2013Kwa kuangalia katika vyombo vya habari vya Ujerumani kutumia neno "Kunduz" kila mara utapata matokeo sawa: shambulizi dhidi ya malori mawili ya mafuta lililosababisha vifo vya watu 100, mapambano dhidi ya Taliban, wanajeshi 54 wa Ujerumani waliouwawa, ushirikiano mgumu, kama sio uliosambaratika, na vyombo vya usalama vya Afghanistan. "Hapa ndipo kazi ya jeshi la Ujerumani ilipobadilika kutoka kuchimba visima na kuwa ya mapigano," alisema waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziére. Kwa maneno makali zaidi mtu anaweza pia kusema: Kaskazini mwa Afghanistan jeshi la Ujerumani limepoteza hali yake ya kutokuwa na hatia kama jeshi lenye amani.
Kila kitu kilianza kwa matumaini makubwa wakati kikosi cha kwanza cha makomando wa Ujerumani kilipowasili Kunduz msimu wa mapukutiko mnamo mwaka 2003. Kwa haraka haraka vipande vya ardhi vikanunuliwa katikati ya mji, na kulindwa kwa kuzungushiwa ukuta na nyaya za sing'eng'e. Kazi ya ulinzi ikachukuliwa na vyombo vya usalama vya Afghanistan, kwa haraka kutafuta wafanyakazi katika jamii ya Waafghanistan. Zaidi hayakuhitajika na wala kutakikana. Wanajeshi wa Ujerumani waliwasili kama marafiki, wakombozi na wasaidizi wa mchakato wa kuijenga upya Afghanistan. Hivyo ndivyo walivyojiona wanajeshi wenyewe na hivyo ndivyo walivyoeleweka na umma wa Afghanistan. Hali ilikuwa tulivu mno, kiasi kwamba muda mrefu haukupita kukaanza kuzungumziwa kile kilichoitwa "Bad Kunduz" - eneo la mapumziko.
Wanajeshi wa kwanza wa Ujerumani kufa tangu vita vya pili vya dunia
Wakati shinikizo dhidi ya kundi la Taliban lilipozidi kuanzia mwaka 2006 kusini mwa Afghanistan, wapiganaji walitafuta na kupata maeneo ya kukimbilia kaskazini mwa nchi, ambako hadi kufikia wakati huo kulikuwa na utulivu. Wakati huo jeshi la Ujerumani, Bundewehr, lilikuwa limehamia kambi mpya, ngome iliyojengwa kwenye kilima maeneo ya juu ya mji wa Kunduz – na kwa sababu nzuri. "Bad Kunduz" ikawa hadithi: Mara kwa mara misafara ya magari ya jeshi la Ujerumani ilishambuliwa na kujikuta katika mapambano makali. Kwa mara ya kwanza tangu kumalizika vita vya pili vya dunia rasmi kukazungumziwa wanajeshi waliokufa vitani. Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1945 wanajeshi wa Ujerumani wakafanya mashambulizi kwa uamuzi wao wenyewe yaliyosababisha matokeo mabaya kabisa. Kwenye mashambulizi ya mabomu dhidi ya malori mawili ya mafuta mnamo mwaka 2009, raia wengi wa Afghanistan walipoteza maisha.
Hizi zilikuwa picha ambazo hazikupokelewa vizuri nyumbani Ujerumani. Tume ya jeshi la Ujerumani Kunduz ikaibua mjadala mkali wenye hisia nzito kuhusu maana na uhalali wa Ujerumani kushiriki operesheni za kujihami na silaha katika nchi za kigeni.
Miradi ya kijamii iko hatarini
Kitu kilichozikwa katika kaburi la sahau ni ufanisi uliopatikana katika kipindi cha miaka 10 ya jeshi la Ujerumani kuwepo Kunduz na maeneo jirani. Barabara na shule zilijengwa, vituo vya afya, vituo vya kutoa mafunzo kwa waalimu vyenye wanafunzi hadi 1,600 na kiwanda cha kuhifadhia nyanya kwenye mikebe. Polisi walipewa mafunzo na mafundi kusaidiwa - mamia ya miradi midogo na mikubwa iliendeshwa, baadhi na wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya maendeleo yasiyo na mafungamano na jeshi, lakini yote katika maeneo yanayoizunguka kambi ya jeshi. Kambi ya jeshi la Ujerumani ya Kunduz yenyewe ikawa kipengele muhimu cha uchumi katika mji huo.
Juhudi hizi za kuijenga upya Afghanistan sasa zimo hatarini. Ni kwa wale watu wenye matumaini imara tu watakaoamini kwamba vyombo vya usalama vya nchi hiyo vitaweza kuhakikisha kunakuwepo utulivu na utangamano bila matatizo. Shirika la misaada ya maendeleo la Ujerumani, GIZ, pia limeshasema litaendelea na shughuli zake hata baada ya wanajeshi kuondoka Afghanistan. Lakini litazimika kujipanga upya na utawala mpya utakaokuwepo bila kujali utakavyokuwa katika siku za usoni. Kwani wapiganaji wa Taliban sasa wanaendelea kuimarika na tayari wamefaulu kuzidhibiti wilaya kadhaa zinazouzunguka mji wa Kunduz. Kwa wapiganaji hao mji huo ni mahala penye ishara ya nguvu na mamlaka. Hadi uvamizi ulioongozwa na Marekani baada ya mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001, mji wa Kunduz ulikuwa ngome ya Taliban eneo la kaskazini la Afghanistan. Wakiudhibiti tena baada ya wanajeshi wa Ujerumani kuondoka, basi hiyo itakuwa ni ishara nzito itakayowatia moyo wanamgambo wenye itikadi kali kuongeza kasi yao nchini Afghanistan.
Mwandishi: Weigand, Florian
Tafsiri: Josephat Charo
Mhariri: Daniel Gakuba