1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Joe Biden ndiye Rais sahihi wa Marekani wakati huu

Daniel Gakuba
21 Januari 2021

Rais mpya wa Marekani Joe Biden ndiye mtu anayefaa kuzishughulikia changamoto zinazoikabili nchi hiyo kwa sasa. Hata hivyo kama anavyoandika katika maoni yake, Ines Pohl wa DW, anasema haitakuwa kazi rahisi.

USA Washington | Amtseinführung: Joe Biden
Joe Biden, Rais mpya wa Marekani akilihutubia taifaPicha: Patrick Semansky/REUTERS

Picha za Januari 6, 2021, ni ushuhuda wa kutisha wa hali ambamo Marekani inajikuta baada ya miaka minne ya utawala wa rais Donald Trump. Ni kumbukumbu ambayo haitasaulika, na sio kwa Wamarekani tu, bali kwa ulimwengu mzima, jinsi wafuasi wa Trump waliochochewa kwa nadharia za chuki na uzushi, walivyolishambulia jengo la bunge mjini Washington, ambalo ni moyo wa demokrasia ya Marekani.

Soma zaidi: Biden aapishwa kuwa rais: 'Demokrasia imeshinda'

Wiki mbili baadaye, rais mpya ameapishwa. Licha ya majaribio yote ya uongo, Trump hakuweza kuzuia hili. Hiyo ndio habari njema. Sote tunapaswa kupumua pumzi ya ahueni.

Ines Pohl, mwandishi wa DW mjini WashingtonPicha: DW/P. Böll

Ingawa Trump sio rais tena, mawazo anayoyawakilisha bado yapo. Marekani haijawahi kujikuta katika mgawanyiko kama uliopo sasa tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe zaidi ya miaka 150 iliyopita. Kambi kuu mbili za kisiasa nchini humo zinaonekana kutoweza kutangamana, iwe bungeni au hata ndani ya nyumba za watu. Makumi ya mamilioni ya wafuasi wa Trump wanaendelea kunaswa katika mtandao wa uongo alioujenga.

Urithi mbaya wa Trump, kikwazo kwa Biden

Trump pia anaacha urithi mbaya wa sera ya kigeni baada ya miaka minne ya maamuzi ya upande mmoja. Washirika wa muda mrefu wa Marekani waliotengwa na Trump  wamefadhaika, wakati viongozi wa kiimla huko Urusi na China, kwa mfano, walijawa na tabasamu walipoona matukio ya Januari 6.

Soma zaidi: Trump aondoka rasmi ikulu kwa mara ya mwisho kama rais

Biden amerithi machafuko na mfumo mbaya wa uchumi. Anahamia Ikulu ya White House ambapo hakuna chochote kinachofaa. Kwa wiki kadhaa, hakuna mtu aliyekuwa akifanya chochote katika taifa hilo lenye nguvu kubwa kiuchumi na kijeshi. Hii ilikuwa hatari, na sio tu kwa Marekani bali pia kwa jamii ya kimataifa.

Kwa bahati nzuri, hakuna rais yeyote mpya ambaye angekuwa na tajriba kama ya Joe Biden. Amekuwa katika siasa kwa zaidi ya miaka 50, akipata sifa ya maelewano na upatanisho na mahasimu wa kisiasa. Baada ya utumishi wa muda mrefu katika baraza la Seneti, alikuwa makamu wa rais Barack Obama kwa miaka minane. Anajua fika changamoto anazokabiliana nazo. Lakini anajiamini.

Mpatanishi mwenye tajriba

Katika hotuba yake baada ya kula kiapo, Biden alijionyesha kama mpatanishi, akisisitiza mada za umoja na maridhiano. Aliyatamka maneno hayo nyuma ya vizuizi vizito vya usalama ambavyo viliweka mbali umati wa watu ambao kwa kawaida wangekuwepo kusherehekea mabadiliko ya kidemokrasia.

Soma zaidi: Sera ya Marekani kuhusu Mashariki ya Kati itabadilishwa?

Washirika wa kimataifa wa Marekani wanaweza kuhakikishiwa kuwa wanaye tena mshirika katika Ikulu ya White House. Kiongozi anayeelewa kuwa Marekani haiwezi kusimama peke yake katika ulimwengu wa utandawazi, na anayeamini katika ushirikiano wa kimataifa kama vile umoja wa kujihami wa NATO.

Hakuna shaka kwamba Biden ndiye mtu sahihi kwa wakati huu. Amechagua timu ya wataalam wenye uzoefu. Biden atatafuta maelewano na Warepublican kufanikisha mpango wake wa uokozi kuhusu janga la COVID-19, na kuanza kushughulikia madhara yaliyosababishwa na janga hilo. Kwa hilo, anaweza kuepusha shari kamili kwa nchi yake.

 

Chanzo: https://p.dw.com/p/3oBwi