Burundi:sasa ni wakati wa kuchukua hatua!
9 Julai 2015Matokeo ya uchaguzi wa Bunge nchini Burundi hayakumshangaza yeyote. Uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki. Kwani, ulifanyika bila ya usimamizi wa tume huru ya uchaguzi na bila ya waangalizi huru.
Wanasiasa wasiokubaliana na hali ya mambo nchini Burundi wameondoka nchini mnamo wiki zilizopita,miongoni mwao wajumbe wa tume ya uchaguzi,wanasheria na waandishi wa habari.
Vyama vya upinzani vilitoa mwito wa kuususia uchaguzi. Vyombo vyote huru vya habari vilizibwa midomo kabla ya uchaguzi, ofisi na vitendea kazi vyao viliharibiwa kabisa. Wananchi wa Burundi hawakuwa na fursa, kabla ya uchaguzi ya kupewa habari za kutosha na vyombo huru vya habari. Sababu ni kwamba vyombo vya habari vilivyopo ni vya serikali tu.
Uamuzi wa Nkurunziza
Tangu kujulikana, mmnmo mwezi wa Aprili kwamba Rais Pierre Nkurunziza atagombea muhula wa tatu wa urais,umwagijaki damu, na hofu imetanda nchini Burundi. Uchaguzi wa Bunge umempa Nkurunziza kile alichokitaka.Sasa njia ya kuleta mabadiliko ya katiba iko wazi kwake.
Mkutano wa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mjini Dar - Es -Salaam hapo juzi, haukuleta suluhisho na chembelecho Rais Nkurunziza mwenyewe hakuhudhuria mkutano huo. Taarifa rasmi iliyotolewa ni kwamba Rais huyo yumo katika kampeni za uchaguzi.
Alieumwa na nyoka hushtushwa na ukoka! Yumkini aliogopa kuondoka nchini , kutokana na kuhofia kile kilichotokea ,alipohudhuria mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mnamo mwezi wa Mei.Baadhi ya wanajeshi walijaribu kumwangusha.Lakini askari wake watiifu walilizima jaribio hilo.
Kenyatta na Kagame pia wajiweka kando
Lakini marais wa Kenya na Rwanda pia hawakuhudhuria kikao cha mjini Dar-Es -Salaam. Hayo yanaonyesha utepetevu wa viongozi hao juu ya mgogoro wa nchini Burundi. Lakini kwa hakika, sasa ndio ni wakati kwa viongoizi hao kuonyesha dhamira ya kuitetea demokrasia katika eneo lao la Afrika Mashariki.
Lakini badala yake Rais Yoweri Museveni wa Uganda amevishwa taji la kuwa mpatanishi wa mgogoro wa Burundi. Yeye mwenyewe ameibadilisha katiba ya nchi yake ili kukiondoa kipengere kinachoweka mipaka ya mihula. Uamuzi huo maana yake ni sawa na kumweka mbuzi kuwa mlinzi wa bustani!
Nkurunziza hasikii la mtu. Anachotaka ni mamlaka ,na mbingu zipasuke! Katika vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka 13 iliyopita watu zaidi ya 300,000 waliuliwa.Watu zaidi ya 150,000 wameshakimbilia katika nchi jirani. Watu zaidi ya 1000 washametiwa ndani na wengine wapatao 500 wamejeruhiwa. Watu zaidi ya 70 wameshauawa tangu mgogoro wa kisiasa uanze nchini Burundi.
Wanajeshi waliotaka kumwangusha Nkurunziza mnamo mwezi wa Mei mwaka huu wametishia kumwondoa Rais huyo kwa nguvu.Lakini yeye anadai kwamba wanajeshi hao wamekimbilia Rwanda ili kuandaa mapambano ya mtutu wa bunduki dhidi yake.
Miito ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika mpaka sasa haijasaidia kitu nchini Burundi. Lakini pia azimio la viongozi wa Afrika Mashariki ,baada ya mkutano wao wa Jumatatu mjini Dar -Es -Salaam, kutaka uchaguzi wa rais uahirishwe kwa wiki kadhaa.-mwito huo pia haukuleta tija.Lakini hata hivyo hatua hiyo ingelileta nini?
Uamuzi wa Rais Nkurunziza wa kuwania muhula wa tatu wa urais unaenda kinyume na katiba na pia unakiuka maadili. Kutokana na hali ya wasi wasi nchini Burundi jumuiya ya kimataifa haipaswi kunyamaa kimya na kushika tama.
Jumuiya ya kimataifa inao wajibu nchini Burundi
Baada ya kutukia mauaji ya halaiki nchini Rwanda,mnamo mwaka wa 2005, Umoja wa Mataifa, ulianzisha utaratibu wa kuchukua wajibu wa ulinzi,Huo ni mfumo mpya unaoziwajibisha nchi kuwalinda wananchi endapo haki zao za binadamu zinakiukwa kwa kiwango kikubwa na kuwalinda dhidi ya mauaji ya kimbari. Ikiwa nchi husika haiutekelezi wajibu huo basi jumuiya ya kimataifa italazimika kuuchukua wajibu huo na kuingilia kati kijeshi.
Hayo lazima yafanyike sasa nchini Burundi kabla ya mgororo wa kisiasa nchini humo haujasababisha maafa ya vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwandishi: Schmidt Andrea.
Mfasiri:Mtullya Abdu.
Mhariri:Iddi Ssessanga