1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni juu ya makubaliano ya Hamas na Fatah

Abdu Said Mtullya24 Aprili 2014

Vyama vya Wapalestina Hamas na Fatah vimefikia makubaliano ya kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa. Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu anayapinga makubaliano hayo .Loay Mudhoon wa DW anatoa maoni yake

Wanasiasa wa nchi za magharibi wamekuwa wanaitumia kila fursa ,mithili ya ibada ,kutoa miito kwa Wapalestina ya kuchukua hatua thabiti ili kuumaliza mgawanyiko baina yao. Sababu ni kwamba bila ya maridhiano ya ndani baina yao itakuwa vigumu kuleta amani katika Mashariki ya Kati.

Mwandishi wa DW Loay MudhoonPicha: DW

Baada ya miaka zaidi ya minane, ya kukabiliana kiadui na kugawanyika kisiasa, sasa Wapalestina wanataka kulifikia lengo hilo Hapo jana wawakilishi wa ngazi za juu wa vyama vya Hamas na Fatah waliyafikia makubaliano juu ya kuvikomesha mara moja vita vya ndugu kwa ndugu na kuunda serikali ya wataalamu ya umoja wa kitaifa.

Kwa mujibu wa matapano yaliyofikiwa, pande mbili hizo zitaandaa uchaguzi wa rais na wa Bunge katika maeneo ya Wapalestina, mnamo kipindi cha nusu mwaka. Huo utakuwa uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia tokea mwaka wa 2006.

Umoja baina ya Wapalestina ni jambo muhimu.

Hata hivyo ni vigumu kwa sasa kusema iwapo mapatano yaliyofikiwa yatatekelezwa, kwani makubaliano kama hayo yameshawahi kufikiwa baina ya pande mbili hizo hasimu za Wapalestina mnamo miaka ya 2011 na 2012 lakini utekelezaji ulishindikana.Lakini hatua hizo zinapaswa kutiliwa maanani.Makubaliano hayo siyo jambo la kushangaza kwa sababu awali ya yote yanatokana na busara ya kuutambua udhaifu wa pande zote mbili za Hamas na Fatah.

Kwanza,kwa upande wa Hamas ,udhaifu huo unatokana na athari za kuondolewa madarakani kwa Rais Mohamed Morsi nchini Misri alietokea katika chama cha Udugu wa Kiislamu. Kutokana na kuondoka kwa Morsi chama cha Hamas kilianza kututusa katika njia kombo.Matumaini yote ya Hamas, yalijongomea iliyoyaweka juu ya Mohammed Mursi na chama chake cha Udugu wa Kiislamu.

Pigo kwa Hamas

Na sasa chama cha Udugu wa kiislamu kimepigwa marufuku baada ya kutangazwa na serikali kuwa ni cha kigaidi nchini Misri. Na kwa upande wake chama cha Fatah kimo katika hali ngumu kwani mkataba wa Oslo unakaribia kusambaratika.Chama hicho cha Rais Mahmoud Abbas kinachozingtiwa kuwa na siasa za wastani kinakabiliwa na changamoto ya kuutetea uhalali wake.

Fatah iliamua kuifuata njia ya mazungumzo katika msingi wa mkataba wa Oslo.Lakini baada ya kufanya mazungumzo kwa muda wa miaka 20 iliyopita chama cha Fatah hakijavuna mazao yoyote. Ndoto ya kuunda nchi ya kipalestina na mji mkuu wake Jerusalem Mashariki, imezidi kusogea mbali, kutokana na mpango wa Israel wa kuendelea kujenga makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina. Njia ya kuelekea kwenye suluhisho la nchi mbili imekuwa inawekewa vigingi mtindo mmoja.

Marekani yavunjika moyo

Badala ya kuyaunga mkono makubaliano yaliyofikiwa baina ya Wapalestina yanayoashiria kuibuka mfumo wa kidemokrasia na kuunga mkono mpango wa kuitishwa uchaguzi, Marekani inaonyesha "imevunjika moyo"huku serikali ya Israel ikionya juu ya kuhatarishwa mchakato wa amani. Lakini mtu akiangalia kwa undani atatumbua kwamba lengo la makubiliano ni kinyume na mitazamo ya Marekani na Israel.

Rais Abbas mpenda amani anaetambuliwa kimataifa,anahitaji ridhaa ya Wapalestina wote.Na lengo hilo haliwezi kufikiwa bila ya kushirikishwa kwa Hamas .

Lakini jambo la kushangaza ni kusikia kauli ya si mwengine bali Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu kwamba Abbas hawezi kuleta amani ati kwa sababu hawezi kuzungumza kwa niaba ya Wapalestina wote.

Madhali makubaliano yaliyofikiwa na Wapalstina yamo katika msingi wa suluhisho la nchi mbili na mkataba wa Oslo, yanaweza kuifungulia njia Hamas ya kuitambua haki ya nchi ya Israel ya kuendelea kuwepo Ndiyo sababu kwamba makubaliano ya Hamas na Fatah ni habari njema kwa Israel vile vile.

Mwandishi:Mudhoon,Loay

Tafsiri:Mtullya Abdu

Mhariri. Josephat Charo