1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kubalini, Ujerumani inataka mabadiliko

27 Septemba 2021

Wapiga kura wameutikisa uwanja wa kisiasa nchini Ujerumani. Wameonyesha kwamba utawala wa vyama vya Kihafidhina vya CDU na chama chake ndugu CSU pamoja na chama cha kisoshalisti SPD umepitwa na wakati kwa sasa.

Deutschland Wahlen I SPD I Reaktionen Prognose
Picha: Maja Hitij/Getty Images

Ni mabadiliko yanayohitajika kama anavyosema mhariri mkuu wa DW Manuela Kasper-Claridge katika maoni yake.

Mabadiliko yamekuja, uamuzi wa wapiga kura Ujerumani uwazi. Ni mwisho wa serikali ya muungano iliyopita na sasa ni wakati wa changamoto kubwa kukabiliwa kama mabadiliko ya tabia nchi, utandawazi na maendeleo ya kisasa yanayohitajika kwa Ujerumani.

Changamoto hizi kubwa sasa zinaweza kukabiliwa kwa ushirikiano na vyama vidogo. Kwa serikali yoyote ya muungano itakayobuniwa, chama cha Kijani na Free Democrats FDP, vitakuwa na usemi mkubwa. Hakuna kitakachoweza kufanyika bila wao na hilo ni jambo zuri.

Kansela Angela MerkelPicha: Patrik Stollarz/AFP

Chama cha Kijani huenda kikasukuma ajenda zake katika majadiliano ya serikali

Idadi kubwa ya kura zilizokiendea chama cha Kijani ni jambo linaloonyesha wazi kwamba Wajerumani wana wasiwasi mkubwa kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kutokana na matokeo haya, chama cha Kijani kitaingia kwenye mazungumzo ya kuundwa kwa serikali ijayo wakiwa na imani kubwa. Watakuwa nyota katika mazungumzo hayo kwa hiyo wanaweza kusukuma mbele ajenda zao.

Ingawa labda Ujerumani haiko tayari kwa mabadiliko kama kilivyo chama cha Kijani pamoja na alivyotaraji mgombea wake wa Ukansela Annalena Baerbock, kama yanavyoonyesha matokeo hasa mabadiliko hayo yanapogharimu fedha.

FDP nacho kina usemi pia

Kuunda serikali bila waliberali FDP ni jambo ambalo halitowezekana pia. Wafree Democrat wanajiona kama wanaoweza kuleta mabadiliko makubwa na wanaweza kuzima baadhi ya matakwa au ndoto za wanamazingira. Waliweka imani yao kwenye soko, udijitali na kupunguza urasimu.

Mhariri Mkuu wa DW Manuela Kasper-ClaridgePicha: DW

Wanataka kulindwa kwa mazingira ila bila kuongezwa kwa kodi ila jinsi hilo litakavyotekelezwa, ni jambo ambalo wanastahili kulieleza katika mazungumzo ya awali ya kuunda serikali ya muungano.

CDU/CSU wako tayari kuwa wapinzani sasa

Kilicho wazi ni jinsi Wahafidhina walivyoshindwa pakubwa katika uchaguzi huu. Ingawa chama cha Christian Democratic Union CDU na chama chake ndugu cha Christian Social Union CSU vimepoteza viti vichache kuliko ilivyotabiriwa katika kura za maoni, matokeo yao huezi kuyalinganisha hata kidogo na matokeo ya uchaguzi uliopita wa shirikisho. Mgombea wao wa CDU Armin Laschet hakuweza kuwaridhisha wapiga kura licha ya kupata ufanisi kama waziri mkuu wa jimbo lenye idadi kubwa kabisa ya watu Ujerumani, North Rhine-Westphalia.

Kansela Angela Merkel alihutubia bunge kuhusu janga la Covid-19

01:20

This browser does not support the video element.

Uungwaji mkono wa chama cha CSU umeporomoka na haya yanaonekana kama matokeo mabaya zaidi ya chama hicho katika uchaguzi tangu mwaka 1949. Baada ya miaka 16 katika serikali, CDU na CSU wako tayari kuwa wapinzani.

Bila shaka vyama vya CDU/CSU vitajaribu kivyovyote vile viweze kuunda serikali mpya, Jamaica kama inavyofahamika kutokana na rangi za vyama itakavyoshirikiana navyo rangi nyeusi ya CDU/CSU, kijani ya chama cha wanamazingria na njano ya chama cha FDP.

Inawezekana licha ya kuwa wahafidhina wana chama cha pili kwa ukubwa. Mara tatu katika miongo kadhaa iliyopita, Kansela amekuwa si mwanachama wa chama chenye wingi zaidi bungeni na la muhimu hapa ni nani atakayeweza kushirikiana na wenzake na kuunda serikali ya muungano akiwa na wingi bungeni?

Olaf Scholz anastahili kuonyesha anachoweza sasa

Hiyo ndiyo changamoto ya Olaf Scholz ambaye amekiongoza chama cha SPD kuwa chama chenye nguvu zaidi katika uchaguzi huu. Ushindani ulikuwa mkali lakini amerudi katika uongozi ukizingatia kwamba katika kura za maoni, chama chake wakati mmoja kilikuwa kinasemekana kwamba kina uungwaji mkono wa hadi asilimia 12 na wakati huo, kilionekana hakitoleta ushindani wowote.

Ila Scholz alifanikiwa kubadilisha mambo lakini msimamo wake binafsi na kile anachokichukulia kuwa muhimu bado hakiko wazi. Anaonekana kama Merkel wa pili, anaweza kutabirika, anapenda hoja na ni mtu wa hisia mambo ambayo wapiga kura walionekana kuyapenda.

Mgombea wa Ukansela wa chama cha SPD Olaf ScholzPicha: Wolfgang Kumm/dpa/picture alliance

Sasa Scholz anastahili kuonyesha kile anachoweza. Iwapo anataka kuwa Kansela anayefuata wa Ujerumani, anastahili kuingia katika mazungumzo ya haraka na chama cha Kijani na FDP. Lengo lake kuu ni muungano wa nyekundu, njano na kijani ila haitokuwa rahisi. Atalazimika kukubali matakwa ya vyama hivyo vidogo, iwe ni katika sera za kimazingira au kodi. Chama cha CDU nacho, kitakuwa kwenye mchakato huo huo wa mazungumzo na vyama hivyo viwili na kitakuwa kinajadili mambo hayo hayo na kumuwekea shinikizo Scholz.

Matokeo ya kuundwa kwa serikali ya muungano hayatabiriki ila wapiga kura wameshazungumza, hawataki mwendelezo wa siasa za Angela Merkel. Nguvu na ushawishi wa vyama vikubwa vya CDU/CSU umeshuka pakubwa ikilinganishwa na miongo iliyopita.

Siasa za Ujerumani zinaelekea kuwa na wachezaji wengi na hii ndiyo nafasi ya kukabiliana na masuala makuu ya miaka ijayo, siasa ziwe rafiki kwa mazingira na za kisasa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW