1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kuhusu kumuhamisha kazi Hans-Georg Maassen

19 Septemba 2018

Uamuzi wa Kansela Angela Merkel wa kumhamishia mkuu wa idara ya upelelezi wa ndani Hans- Georg Maassen kwenye wadhifa wa naibu waziri umewakasirika wananchi wengi nchini Ujerumani.

Berlin Hans-Georg Maaßen nach dem Parlamentarischen Kontrollgremium
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemwondoa mkuu wa idara ya ujasusi wa ndani Hans-Georg Maassen kwenye wadhifa huo licha ya upinzani, na kwa kuchukua hatua hiyo Merkel amewaridhisha washirika wake wa serikali ya mseto.

Tunaweza kusema kwamba uamuzi huo unaonyesha hulka yake yaani wote wanaohusika wameambulia chochote, chama cha SPD kilichokuwa kimekaa chonjo kusubiri bwana Maassen ajiuzulu na pia waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer aliyekuwa anamtetea bwana Maassen kwa nguvu zote.

Waziri Seehofer hatimaye ameweza kumpandisha cheo mkuu huyo wa ujasusi wa zamani kwa kumteua kuwa naibu waziri kwenye wizara yake. Kansela Merkel amelifikia lengo lake muhimu kabisa. Serikali ya mseto itaendelea kuwepo na kufanya kazi.

Mzozo juu ya bwana Maassen uliotishia kusababisha mgogoro mkubwa serikalini umetatuliwa kwa umahiri mkubwa wa kisiasa licha ya ukweli kwamba suluhisho hilo limewakera wananchi wengi nchini Ujerumani. Hadi wiki za hivi karibuni, Hans-Georg Maaßen aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi wa ndani nchini Ujerumani aliitikisa imani ya kansela Merekel. Hilo si jambo la kawaida.

Maassen alidai kwamba wahamiaji hawakuwindwa na kushambuliwa kwenye mji wa Chemnitz tofauti na aliyosema Merkel hapo awali. Lakini baada ya bwana Maaßen kushidnwa kuyathibitisha aliyokuwa anadai, uaminifu wake uliingia mashakani na kuzua mjadala.

Kushoto: Hans-Georg Maassen. Kulia: waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst SeehoferPicha: Reuters/F.Bensch

Badala ya kuwatuliza wananchi kwa kuwapa uhakika wa usalama alipandikiza mbegu za hofu na mashaka. Pia katika mikasa ya hapo awali, ya kuchunguza ugaidi wa manazi mamboleo wa mtandao wa (National Sozialist Underground) NSU na kuuliwa kwa Anis Amri kwa kupigwa risasi na polisi mjini Milan bwana Maaßen hakuonyesha ustadi uliostahili. Na kwa hivyo ni jambo la mashaka makubwa kumpandisha cheo mtu kama huyo!

Kile ambacho kimetambuliwa kuwa kipaji cha kansela Merkel cha kuweza kutatua migogoro kinaweza sasa kugeuka na kuwa udhaifu wake. Swali ni kwa muda gani wananchi wake wataendelea kuutathimini mkakati huo? Haiwezekani kumpandisha  mtu cheo ambaye hapo awali hakuifanya kazi yake vizuri. Ni mtu aliyembeza kansela, ni mtu anayesemekana kuwa amesimama karibu na chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD vipi mtu kama huyo anaweza kuendelea katika wadhifa mwingine?

Jee hilo ndilo suluhisho la kisiasa ambalo wananchi watalikubali watakapokwenda kupiga kura katika uchaguzi wa jimbo la Bavaria la kusini mwa Ujerumani?  Wananchi milioni tisa wa jimbo hilo, hawataamua tu juu ya mustakabal wa mwenyekiti wa chama cha CSU Horst Seehofer, bali pia katika akili zao watakuwa wanauchekecha  mwafaka uliofikiwa  juu ya Maassen.

Mwandishi: Zainab Aziz/ Romaniec, Rosalia (PuG)/ LINK: http://www.dw.com/a-45548892

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman