1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kupambana na chuki

Mohammed Khelef27 Julai 2016

Katika maoni yake, Christoph Strack wa DW anasema mauaji dhidi ya padri mzee kaskazini mwa Ufaransa yanatoa picha halisi ya magaidi kuwa hawawakilishi imani yoyote ya kidini na haja ya kupambana na kuzishinda chuki.

Rais Francoise Hollande wa Ufaransa akizungumza na Meya Hubert Wulfranc wa Saint-Etienne-du-Rouvray kufuatia mkasa wa mauaji kanisani.
Rais Francoise Hollande wa Ufaransa akizungumza na Meya Hubert Wulfranc wa Saint-Etienne-du-Rouvray kufuatia mkasa wa mauaji kanisani.Picha: Reuters/B. Maslard/Pool

Padri mzee, Jacques Hamel, alikatwa koo akiwa kanisani kaskazini mwa Ufaransa hapo jana (Jumanne, 26 Julai) baada ya watu wawili kulivamia kanisa hilo na kuwateka nyara waliokuwemo.

Mashambulizi hayo kwenye kijiji cha Saint-Etienne-du-Rouvray kando kidogo na mji mkongwe na mashuhuri wa Normandy yalifanyika wakati bado Ufaransa ikiwa hata haijapona vizuri kutokana na mauaji ya Siku ya Taifa mjini Nice ambayo yaliangamiza maisha ya watu 84, na ambayo yote yanadaiwa kufanywa na kundi la kigaidi lijitalo Dola la Kiislamu.

Ulikuwa unyama uliowashitusha watu duniani kote. Mauaji ya kikatili dhidi ya mchungaji huyu mzee akiwa kwenye misa kanisani mwake, moja ya makanisa makongwe kabisa, kwa hakika, hayawezi kutajwa kwa lugha nyepesi.

Ni tukio la kinyama ambalo linakusudia hasa kuongeza machungu kwenye roho ya Ufaransa ambayo tayari imeshajeruhiwa. Machungu kwenye dola linalojitambulisha kama lisilochanganya dini na siasa na pia taifa kubwa la kiviwanda. Hakika, Ufaransa ni binti mkongwe wa Dola ya Kirumi.

Christoph StrackPicha: DW

Kutaka kujuwa hayo, viangalie hivi vijiji vya Normandy, Burgundy, Vendee, mbali huko kando na miji mikubwa na ya kisasa. Maeneo haya ndiyo yenye makanisa makongwe kabisa, ambako mfumo wa maisha huko ni ukristo safi.

Ndiko ambako mara kwa mara watu hukusanyika kwa matamasha na sherehe za kidini, kama alivyokutwa padri huyu na mauti akiwa kwenye moja ya mikusanyiko hiyo. Yalikuwa ndiyo maisha yake.

Kifo cha 'shahidi'

Padri Hamel alikuwa na miaka 85 tayari, akiwa amelihudumia kanisa kwa miaka 58 ya uhai wake, jamii yake ikimuelezea kama mtu rafiki, mwepesi wa kufanya urafiki naye, masikini na mwenye heshima – kama walivyo mapadri wa vijijini nchini Ufaransa.

Miaka 10 baada ya kustaafu rasmi, jana alikuwa amesimama kando ya madhabahu wakati magaidi wawili walipoingia kanisani humo na kumtaka apinde magoti. Alipotaka kujitetea, wakamkata koo yake, mule mule kanisani, pale pale madhabahuni.

Ikiwa dhana waliyonayo wauaji hawa ni kufa mashahidi, basi Padri Hamel ndiye aliyekufa shahidi. Si wao ambao ni wahalifu wasiokuwa na ubinaadamu na waliojawa na unyama, wanaomwaga damu ya yeyote, mahala popote.

Naam, Padri Hamel ndiye hasa shahidi wa kweli. Hakuwa na kosa lolote, alikuwa kanisani kwenye ibada, akauawa. Ufaransa inaweza ikawa bado inatikiswa na mifano ya mauaji kama haya. Hivi karibuni, taifa hilo liliyakumbuka mauaji kama hayo mwaka 1996, ambapo wachungaji saba walichinjwa kwenye milima ya Atlas nchini Algeria.

Askofu Mku wa Rouen Dominique Lebron aliyataja mauaji ya padri wake kwenye Siku ya Vijana Duniani, na huku akiwa ameshitushwa na kuumizwa, alisema: “Kanisa Katoliki halina silaha nyengine yoyote zaidi ya sala na udugu baina ya watu.“ Sasa Kanisa la Ufaransa linataka liwe na siku moja ya kufunga na kusali.

Mwandishi: Chrisptoh Strack
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf