Maoni: Lazima tuchukue hatua sasa kuhusu tabia nchi
10 Agosti 2021Baada ya kushuhudiwa mwezi wa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha mafuriko na matukio ya moto wa msituni barani Ulaya, haishangazi kufahamu -- kwa mara nyingine tena – kuwa ongezeko la joto duniani linalosababishwa na binadamu, ndio la kulaumiwa. Ripoti ya karibuni ya watalaamu wa mabadiliko ya tabia nchi – IPCC imethibitisha kuwa joto linaweza kuongezeka duniani kwa nyuzi 1.5 za Celcius ikilinganishwa na 1900 ndani ya miaka 15 – hali ambayo ingeepukika hadi mwisho wa karne hii kama tungepunguza utoaji wa gesi chafu kama ilivyofikiwa Paris mwaka wa 2015.
Lakini tumeambiwa kuwa hatujachelewa sana. Kama dunia inaweza kufikia sifuri viwango vya utoaji gesi chafu ifikapo mwaka wa 2050, viwango vya joto vitaongezeka kidogo tu zaidi ya nyuzi 1.5 za Celcius kabla ya kutulia. Kwa hali hiyo, vinaweza hata kupungua ifikapo 2100.
Kuna dhamira ya kisiasa ya kufanikisha hilo? Hakuna kwa ushahidi wa sasa. Ahadi tupu za muafaka wa tabia nchi wa Paris zimetuweka kwenye mkondo wa kufikia karibu nyuzi 3 ifikapo mwisho wa karne hii.
Kwa sasa, joto ni nyuzi 1.1 za celcius, na tayari tunashuhudia matukio ya moto wa msituni, mafuriko na kuongezeka kwa kina cha bahari. Kama tutafika nyuzi 3 za celcius, tutakuwa katika matatizo makubwa sana.
Soma pia: IPCC: Gharika zinatokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi
Mwaka jana, Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa – UNEP lilipendekeza kuwa kwa kuwekeza katika ajira Rafiki kwa mazingira na miundombinu na kuchagua sera Rafiki kwa mazingira, viongozi huenda wakapunguza utoaji gesi chafu kwa robo ya kile wangepaswa kuwa ifikapo 2030. Badala yake, nchi tajiri zinaendelea kuunga mkono hali ilivyo ya kiwango kikubwa cha gesi ya kaboni.
Ahadi ya China kupunguza gesi ya kaboni ifikapo 2060 huenda isitimie. Australia ambayo ilikumbwa na matukio mabaya ya moto wa msituni kwa miezi kadhaa katika mwaka wa 2019 na 2020, imekataa kusaini lengo la kufikia sifuri gesi ya kaboni ifikapo 2050.
Wakati wa kuwawajibisha wachafuzi wa mazingira
Bahati nzuri ni kuwa kuna mbinu mpya katika mapambano ya kupunguza kwa kasi gesi ya kaboni inajitokeza haraka. Wanaharakati na vijana wanakwenda mahakamani na kuzishitaki serikali na makampuni yanayotengeneza fueli asilia. Wanafanikiwa katika kuhoji kuwa wachafuzi wanatishia mustakabali wao na hivyo haki zao za binaadamu.
Serikali ya Ujerumani imelazimika kuja na malengo kabambe ya tabia nchi; Kampuni kubwa za Mafuta kama vile Shell zimeamrishwa kupunguza pakubwa uzalishaji wa gesi chafu kwa asilimia 45 katika miaka 10 na kulipa faini za mabilioni ya euro. Wawekezaji wao pia wanadai kuchukuliwa hatua.
Soma pia: Ripoti ya IPCC: Dunia yashindwa kudhibiti uzalishaji gesi chafu
Bi Kaisa Kosonen, anayesimamia sera ya tabia nchi katika shirika la Greenpeace, amesema ataipeleka ripoti ya IPCC mahakamani. Ameongeza kuwa ushindi wa kihistoria mahakamani dhidi ya Shell nchini Uholanzi ulitokana na kuiunga mkono sayansi ya IPCC.
Soma pia: IPCC - Matumizi ya ardhi na mabadiliko ya Tabia Nchi yanahusiana
Licha ya nia njema iliyojitokeza kupitia maandamano ya wanafunzi kuhusu tabia nchi ya Fridays for Future, shinikizo la umma pekee halitoshi kuyalazimu mabunge kuchukua hatua. Ni kupitia wimbi la kesi za kisheria za tabia nchi ambalo litapiga mahakamani kote ulimwenguni ambapo raia wenyewe wanaweza kuchochea hatua ya kupunguzwa kwa kasi gesi ya kaboni – na kuepusha janga baya kabisa la ongezeko la joto duniani.
LINK: https://www.dw.com/a-58809149