Los geht’s – nicht weiter so
5 Machi 2018
Haikuwa rahisi, lakini mwishoni kila kitu kimekwenda sawa. Wanachama wa SPD wamepiga kura ya ndio kukiruhusu chama chao kushiriki katika serikali nyingine ya muungano na Bi Angela Merkel, kwa wingi wa kuridhisha. Serikali mpya inatarajiwa kuwa imeundwa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, kabla ya Pasaka.
Umekuwa mchakato mgumu, ulioshuhudia kushindwa kwa juhudi za awali za kuunda serikali ya muungano na vyama vidogo na kuanguka kisiasa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa SPD Martin Schulz. Kansela Merkel alikuwa chini ya shinikizo kubwa, kwa kushindwa kupata wingi unaohitajika kuunda serikali, katika enzi hizi za vyama vingi vidogo.
Mazingira mapya ya kisiasa kwa Ujerumani
Ilikuwa hali mpya kabisa kisiasa nchini Ujerumani, kwa sababu tangu kuundwa kwa Jamhuri ya Shirikisho mwaka 1949, mojawapo ya vyama viwili vikuu kilikuwa kikihitaji tu kupata mshirika, na wakati mwingine kiliweza kuunda serikali peke yake. Miaka 12 iliyopita, hali ilikuwa ya kueleweka hata zaidi, Angela Merkel alikuwa ndiye Kansela, na kwa ulimwengu wa nje, mengine yote hayakuwa na umuhimu mkubwa.
Lakini, kuingia kwa chama cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD katika Bunge la Shirikisho, kumefikisha ukingoni siasa za mteremko. Vyama vilivyokuwa vikubwa vinaendelea kuwa vidogo, na vilivyokuwa vidogo vinabadilika kuwa vikubwa. Hali hii inalifanya zoezi la kuunda serikali ya mseto wa vyama kuwa gumu zaidi.
Hiyo ni hali hali ya matukio nchini Ujerumani. Vyama viwili vikuu vimewakatisha tamaa wanachama wao, kiasi kwamba wamegeukia vyama vya mirengo mikali, iwe upande wa kushoto, au kulia. Vyama hivyo havina jibu la kutuliza wasiwasi unaowakumba Wajerumani wengi, walio na hofu juu ya mustakabali wa familia zao, na kitisho wanachoamini kinaukabili mtindo wao wa maisha. Wanasiasa wa vyama hivyo wameshindwa kueleza uwiano uliopoa kati ya utandawazi, mwingiliano wa jamii na utambulisho binafsi wa kitaifa.
Ujerumani ina dira gani katika siasa za kimataifa?
Na kwenye uwanja wa kimataifa, haieleweki Ujerumani inataka kutoa mchango gani katika dunia ya akina Trump, Putin na Xi Jinping. Hali kadhalika, haijabainika wazi majukumu makubwa katika siasa za nje na za ulinzi za Umoja wa Ulaya, yatakuwa na maana gani kwa Ujerumani.
Mapambano ya kisiasa mnamo miezi michache iliyopita yanaweza kuwa kielelezo cha kile kinachohitajika kwa Ujerumani. Wanasiasa wanapaswa kuwahakikishia wapiga kura kwamba wameanza kuwasikiliza tena. Wanapaswa kuwahakikishia kwamba wanafahamu kwamba watu wa kawaida pia wanavyo vipaumbele vyao ambavyo inabidi vitiliwe maanani, bila kulazimika kurejea katika mitazamo hatari ya kizalendo.
Vile vile, serikali ya muungano wa vyama vikuu inapaswa kutafuta namna ya kuhakikisha kwamba kila chama mshirika kinabaki na sera zake, ambazo ni tofauti na kingine. Kuwa na misimamo inayoeleweka wazi wazi, ni kigezo pekee kitakachorudisha imani ya wapigakura.
Kuogelea pamoja, au kuzama pamoja
Ikiwa vyama vivyo vitashindwa kuonyesha mipaka katika sera zao, vyote vitaanguka pamoja katika uchaguzi ujao. Katika juhudi hizo, itakuwa muhimu kuepuka kutafuta sifa kutoka upande usio sahihi, na haitakuwa busara kutafuta uungwaji mkono katika ngome ya chama cha AfD.
Kansela Merkel anaweza kuunda serikali. Njia ndefu kuelekea katika mchakato huo ni ishara tosha kwamba mwelekeo wa kisiasa wa Ujerumani unapaswa kupatikana kwa njia ya majadiliano. Mwanasiasa wa chama cha Kijani cha Ujerumani Cem Özdemir ambaye wazazi wake ni wahamiaji kutoka Uturuki, alikuwa sahihi aliposema kwamba kujihusisha na misimamo mikali ya wanazi hakupashwi kuwa kigezo cha fahari na uzalendo kwa Wajerumani, bali kulinda mawazo tofauti, na kukubali nchi inayozingatia uhuru wa mtu. Risala kama hiyo zilikuwa hazijasikika kwa muda mrefu.
Mwandishi: Ines Phl
Tafsiri: Daniel Gakuba
Mhariri: Grace Patricia Kabogo