1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Manifesto ya CDU/CSU haina majibu yanayotosheleza

22 Juni 2021

Matarajio juu ya manifesto ya pamoja ya vyama vya CDU na CSU kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba ni makubwa, lakini kwenye maoni yake mwandishi wetu, Kay-Alexander Scholz, angelipenda lau ingelikuwa vyengine.

CDU / CSU Wahlprogramm 2021 Armin Laschet Markus Söder Angela Merkel
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kwa mtazamo wa wanachama wao wenyewe, kuna mengi mazuri na yaliyo sawa kwenye manifesto ya CDU/CSU.

Lakini kusema kwamba ni ya kutikisa kama alivyodai mkuu wa CSU, Markus Soeder, kwenye uzinduzi wa ilani hiyo hapo jana, ni utiaji chumvi mkubwa.

Badala yake, ukiacha machache ya kushangaza, mengine mengi muhimu yanakosekana.

Muna mengi ya muendelezo, maombi ya kuwataka watu wajifanyie mambo wenyewe na mambo ambayo yanasikika vyema masikioni, ila sio kwa mtikisiko wa gitaa la umeme, bali doro kama piano ya Mozart. 

Maoni yameandikwa na Kay-Alexander Scholz.

Yamo baadhi ya mambo kwenye manifesto hii ambayo yanatangaza mabadiliko. Mathalan, kwenye maeneo ya ulimwengu wa dijitali na upunguzaji wa urasimu serikalini.

Lakini inapozingatiwa kwamba ni muungano wa vyama hivyo viwili ambao umekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 16 sasa, mtu huweza kujiuliza kwa nini haukufanikiwa kwenye mengi ya hayo.

Hayo hayajibiwi kwa ufasaha ndani ya kurasa 138 za manifesto hii. 

Walinzi wa Mazingira na AfD

Kwa wengi, tayari muziki umekuwa ukipigwa kwengine – yaani na chama cha Kijani cha walinzi wa mazingira.

Hatimaye imeonekana kwa mara ya kwanza kwamba inawezekana kwa muungano wa CDU-CSU kutokuweza kuamuwa nani awe kansela, na kwamba Kijani wangelichukuwa nafasi hiyo. Lakini katika siku za hivi karibuni, mgombea wao wa nafasi hiyo, Annalena Baerbock, amesababisha mtafaruku miongoni mwa wapiga kura.

Ila pamoja na hayo, baada ya miaka 16 madarakani, majibu yaliyomo kwenye manifesto ya CDU/CSU iko kimya sana kwa mtazamo wa kitisho cha wazi cha kupoteza madaraka.

Bila kusahau kundi la muziki wa matangi matupu, AfD, ambao zogo lao kwenye chumba cha mazoezi linamkera kila mtu.

Na mwenyekiti wa CDU na mgombea wa muungano huo, Armin Laschet, akiwa kinara mpya bado hajichanganyi sana na watu akilinganishwa na mwenzake wa CSU, Markus Soeder.

Japokuwa wote wawili walitangaza vita vya kuwania kiti cha ukansela vimekwisha, lakini Soeder alithibitisha kuifahamu na kuwasilisha na kuifurahia vyema zaidi manifesto kuliko Laschet.

Manifesto si ushindi

Manifesto ya uchaguzi bado si ushindi wa uchaguzi. Ni maandishi tu yaliyoandikwa kwa ajili ya mazungumzo ya uundaji serikali ya mseto.

Linapokuja suala la kuongoza serikali, kawaida watu huyapitia upya maandishi kama hayo. Lakini mara hii si jambo la kawaida kwa kuwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1949, kiongozi wa kikosi hawanii tena uchaguzi.

Ndio maana ile nyimbo kongwe ya Kansela Angela Merkel iitwayo “Munanijuwa” haivumi tena sasa.

Kwa hivyo, mwishoni mwa kipindi cha miaka 16, mtu angelipenda kusikia kutoka kwa mwanamke huyu aliyeongoza mtawaliwa mihula minne, akisema kwa nini kikundi chake kiendelee kuruhusiwa kutumbuiza.

Hadhira ukumbini wangelifurahi sana kama wangepata maneno machache ambayo yangepenya masikioni mwao.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW