Maoni: Mashambulizi ya Berlin yataibadilisha Ujerumani
21 Desemba 2016Shambulio hilo la kikatili limelengwa dhidi yetu sote, sisi tunaopendelea kuishi maisha huru na ya amani. Ni kitendo cha kishenzi dhidi ya kiu chetu cha kupendelea uhuru. Na ndio maana shamabulio la kigaidi la Berlin limeibadilisha Ujerumani. Hatuko tena kama ilivyokuwa kwa muda mrefu ikitajwa-kandoni mwa ugaidi wa kimataifa - tumegeuka kuwa wahanga sawa na Waingereza, Wafaransa, Wahispania, Waisraeli, Wamarekani na wengineo.
Na hapo ni mamoja tu, kama shambulio hilo limefanywa na mtu aliyepungukiwa na akili, mbwamwitu anaependelea upweke na mwenye kiu cha kuuwa au kundi la wafuasi wa itikadi kali. Limeiathiri jamii huru.
Kwa kupiga katika soko la Krismasi, limeiathiri alama ya Ukristo - kitambulisho cha desturi na mila za Wajerumani na Wazungu kwa jumla.
Shambulio la aina pekee
Kansela hajakosea: Hii ni siku ya huzuni kwa wajerumani. Na unahisi pia (mashambulio kadhaa yametokea miaka ya nyuma na mengine kwa bahati nzuri yaligunduliwa mapema.
Shambulio hili ni la aina pekee. Tabia ya wajerumani itabadilika. Hali ya kuishi bila ya shida wala manung'uniko,bila ya hofu wala mashaka itabadilika. Ujerumani itajisikia haiko salama. Na hali haitakuwa salama.
Zaidi ya hayo kuna kitisho cha zilzala ya kisiasa inayoweza kusababishwa na shambulio hilo, hasa kama aliekuwa nyuma ya shambulio hilo ni mkimbizi. Mtu alioyeomba hifadhi humu nchini. Mtu aliyetaka akubaliwe kinga ya ukimbizi.
Mtu ambae hakutimuliwa na viongozi wa nchi hii. Ikiwa kweli mkimbizi aliyefunguliwa mlango wa Ujerumani kwa dhati ndie aliyefanya shambulio hilo, basi hali hiyo itaitumbukiza katika janga la matatizo siasa ya kansela kuelekea wakimbizi. Hapo imani ya jamii kuelekea watu wenye dhiki itachafuliwa.
Na wakati huo Ujerumani pia itajikuta ikielemea zaidi mrengo wa kulia na kuwapatia ushindi wafuasi wa nadharia kali za kizalendo. Hapo jamii iliyo wazi itajifungia.
Na uhuru utakabiliwa na mashaka. Bila ya shaka katika siku kama hii watu wanabidi wawe na subira na kuonyesha busara. Lakini haitakuwa rahisi. Usiku wa decemba 19 ni usiku ulioibadilisha Ujerumani-kwa kiwango gani? Hilo tutalijua baadae.
Mwandishi: Alexander Kudascheff/Hamidou Oumilkheir
Mhariri: Iddi Ssessanga