1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Matarajio ya Afrika kwa Marekani

Josephat Charo
10 Novemba 2020

Joe Biden anabaki kuwa rais mteule wa Marekani. Lakini matarajio mengi yameanza kumiminika kutoka kila kona ya dunia huku kiongozi huyo akiwekewa matumaini makubwa, anasema Mkuu wa Idhaa za Kiafrika wa DW, Claus Stäcker.

USA Wilmington | Rede Joe Biden und Kamala Harris
Picha: Carolyn Kaster/AP Photo/picture alliance

Tayari alipojitokeza kwa mara ya kwanza kabisa kama mshindi wa uchaguzi wa Marekani, hali ya wasiwasi ilianza kuibuka: Joe Biden alipanda jukwaani kama mwanaspoti, lakini mbio za rais huyo mteule mwenye umri wa miaka 77 zilionekana kuwa dhaifu kuliko washauri wake wa vyombo vya habari walivyokuwa pengine wamenuia. Je, Joe huyu wa kukimbiakimbia anaweza kutimiza matarajio makubwa anayowekewa kote ulimwenguni?

Barani Afrika, rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aliongoza katika kutoa wito: "Namtolea wito bwana Biden atumie uzoefu wake mpana asaidie kupunguza athari hasi za siasa za kizalendo katika masuala ya kimataifa.

Kukubalika haraka

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kwa haraka alimtaja Biden kama rafiki wa Kenya, anayetoa jukwaa kubwa na zuri zaidi kwa ushirikiano wa karibu. Na rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliwaongoza Waafrika na waumini wenzake wakristo kuitangaza Marekani kama mshirika asili.

Biden ni rais wa saba wa Marekani anayeshuhudiwa na Museveni mwenye umri wa miaka 76. Kwa busara rais Museveni hakuzungumzia maadili ya demokrasia ambayo yangeiuanganisha Uganda na Marekani. Jeshi lake la polisi lilikuwa limemtia mbaroni mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, ambaye umri wake ni mdogo kuliko wa Museveni kwa karibu miaka 40. Kiongozi huyo wa upinzani alithubutu kuwasilisha fomu zake kama mgombea urais katika uchaguzi ujao wa Uganda huku akiinua ngumi na akiwa amezingirwa na wafuasi wake wakimshangilia. Bobi Wine anadai aliteswa tena akiwa kizuizini.

Ni wasaa wa viongozi wa kiimla

Madai ya mateso pia yanasambaa nchini Ivory Coast, ambako kiongozi wa upinzani na waziri mkuu wa zamani Pascal Affi N'Guessan alikamatwa wakati wa wingu la hekaheka za uchaguzi wa Marekani. Inaonekana kama kampeni ya kulipiza kisasi ya rais Allasane Drahman Ouattara, mwenye umri wa miaka 78, ambaye kinyume na katiba ameshinda awamu ya tatu madarakani. Upinzani uliususia uchaguzi uliofanyika nchini humo na sasa wameunda aina fulani ya serikali kivuli, na hii ndiyo sababu unalaumiwa kwa kuigawa nchi na kuwachochea wananchi.

Claus Stäcker, Mkuu wa Idara za Kiafrika, DW

Huko Afrika Mashariki nchini Tanzania rais John Pombe Magufuli, mwenye umri wa miaka 61, kwa sasa hivi naye ana hekaheka, ingawa alishinda kwa kishindo kikubwa uchaguzi wa Oktoba 28 kwa asilimia 84. Mtu angedhani sasa angekuwa na ukaribu mkubwa katika kuwakabili wapinzani wake ambao wamedhoofika kabisa. Mbunge wa zamani wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema ametimkia Kenya. Mgombea urais wa chama cha upinzani Chadema, Tundu Lissu hata alilazimika kuomba hifadhi katika ubalozi wa Ujerumani kutokana na vitisho vya kuuliwa. Mwanasiasa huyo alipitia mtihani mkubwa aliposhambuliwa kwa risasi katika jaribio la kumuua mnamo mwaka 2007 na kimiujiza akaponea chupuchupu baada ya kufanyiwa upasuaji mara 19.

Ethiopia na mizozo isiyokuwa na vichwa vya habari

Na pia kuna mwanamageuzi aliyemwagiwa sifa kedekede, Abiy Ahmed, waziri mkuu wa Ethiopia mwenye umri wa miaka 44. Alimtimua mnadhimu mkuu wa jeshi, mkuu wa idara ya ujasusi na waziri wa mambo ya nchi za nje na sasa anataka kusuluhisha mzozo wa ndani na jimbo la Tigray kutumia harakati ya kijeshi. Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kama mbabe wa vita: baada ya kupewa heshima kubwa kiasi hicho mtu angemtarajia awe na uwezo mkubwa kuulinda umoja wa Jamhuri ya Ethiopia.

Licha ya matukio haya yanayozusha hamasa kubwa, matukio ya umwagaji damu nchini Cameroon, Guinea, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo au mizozo ya kudumu kama ya nchini Zimbabwe au Mali, yote imetupwa katika kaburi la sahau. Sio suala la mjadala tena, ni wazi kwamba tawala za kiimla barani Afrika zinakabiliwa na wimbi la pili la uasi wa msimu wa machipuko. Sio tu viongozi wenye umri wa zaidi ya miaka 75 wa Uganda, Cameroon au Guinea wanaotumia ombwe lililosababishwa na kukosekana dola kubwa yenye ushawishi duniani. Hata viongozi wenye umri mdogo kama Abiy Ahmed wa Ethiopia mwenye miaka 44, pia wanajitia hamnazo kwa sababu hakuna mkosoaji makini mwenye mbavu za kuwakaripia na kuwarekebisha.

Madai ya mfumo wa demokrasia wenye maadili

Nadharia ya Trump haikutoa nafasi kwa maadili na mikakati ya kimataifa. Sera ya Trump kuelekea bara la Afrika sio tu kwamba haukuwa wazi kwa miaka minne, bali pia haikuwepo kabisa! Kitu kilichobaki kukwama ni jinsi ilivyozichanganya nchi na kuzibandika nchi ambazo hazikuwa na makosa kama mataifa yasiyo maana. Kufuatia ushindi wa Joe Biden, matumaini yanaongezeka tena, kwamba Marekani haitajikita tu kwenye mikataba ya biashara, lakini pia itazingatia haki za binadamu na viwango vingine vya demokrasia. Jukumu hili la Marekani barani Afrika limevurugika kwa kiwango kikubwa cha kutisha katika miaka ya hivi karibuni na huku muundo wa maadili ya mataifa ya magharibi ukiwashawishi vijana wa Afrika.

Joe Biden pekee hataweza kuyatatua haya yote. Macho mengi kwa hivyo yanamkodolea makamu wake, Kamala Harris, ambaye anaamiwa kuwa na ushawishi kwa kiasi fulani kwa bara la Afrika katika ikulu ya Marekani. Hii haihitaji mbio zilizoandaliwa na washauri kwa ajili ya vyombo vya habari, bali nguvu za kukimbia mbio za ndefu za marathon.

Mwandishi: Stäcker, Claus

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW