Maoni: Matokeo ya Uchaguzi Afrika Kusini
10 Mei 2019Miaka 25 baada ya kumalizika mfumo wa ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid nchini Afrika Kusini, kila kitu kiko kama kilivyokuwa. Upande wa upinzani unalalama na chama cha African National Congress kinatawala. Licha ya kampeni za kusisimua za uchaguzi, waliberali wa Democratic Alliance na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kushoto "Wapigania uhuru wa kiuchumi-EFF" hawakufaulu kuibadilisha hali ya mambo. Matokeo ya uchaguzi yanalingana na makadirio
ANC wamepoteza kura lakini si sana hivyo kama ilivyokuwa ikitarajiwa. Sambamba na hayo hakuna, si chama cha Democratic Alliance na wala si kile cha Wapigania uhuru wa kiuchumi, EFF kilichoweza kufaidika pakubwa na mkwamo mkubwa wa chama tawala-kinyume na jinsi watu walivyokuwa wakifikiria. EEF hakikufanikiwa kama chama cha malalamiko na Democratic Alliance kimepoteza kura. Mageuzi hayakutokea.
Bungeni hali ya mambo inabakia kama ilivyokuwa:
Wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kushoto EFF wataendelea na shinikizo lao na kufika hadi ya kutoa matamshi ya kibaguzi dhidi ya wazungu walio wachache."Uhuru wa kiuchumi ni jina tu wanalojiita, lakini wanaishia kuuwekea vizuwizi uhuru wa kiuchumi.
Na wafuasi wa siasa za kiliberali za kiuchumi kutoka chama cha Democratic Alliance wataendelea kujitambulisha kama wao peke yao ndio wenye uwelewa wa kiuchumi. Watajiepusha na mitindo ya kutaka kuwabughudhi wajasiriamali na wapigakura asilia wa kizungu na kwa namna hiyo kufifiisha matatizo makubwa ya kijamii yaliyosababishwa na karne nne za utawala wa kiburi wa wazungu. Lakini mada hizo hasa ndizo zenye umuhimu mkubwa kwa wakaazi walio wengi wa nchi hiyo. Na Afrika Kusini haijapata njia ya kuzipatia ufumbuzi mada hizo baada ya enzi za Nelson Mandela. Kati kati kinaranda chama kilichopoteza hadhi yake cha ANC kinachokabwa na rushwa na ambacho kinataka kujitambulisha kwa wakati mmoja kama chama cha ujamaa wa kizalendo na pia cha kiliberali.
Vijana wanataka njia mbadala
Chama cha ANC ambacho wapigania uhuru wa zamani bado mpaka leo wanajinata kuwa na haki ya kudhibiti hatamu ya uongozi. Chama cha ANC kinachotumia urithi wa Mandela na kudai kipatiwe muda kila uchaguzi unapoitishwa na baadae kuutumia vibaya hakiwezi kudumu milele. Ushahidi umeonekana kutokana na idadi ya walioteremka kupiga kura. Imepindukia kidogo asili mia 60-hiyo ikiwa idadi ndogo kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1994. Vijana wamekata tamaa, hata kupiga kura hawendi. Na waliokwenda kupiga kura idadi yao haijafikia hata asili mia 20. Hali hiyo inaonyesha jinsi vijana walivyochoshwa. Hakuna chama chochote kinachowavutia vijana. Bado kuna upungufu wa nguzo ya kimambo leo ya upinzani inayoweza kuwavutia raia vijana wa Afrika Kusini. Upande wa upinzani una muda ziada wa miaka mitano kujiandaa vyema.
Mwandishi: Claus Stäcker/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Khelef