1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano yavunjika Berlin

20 Novemba 2017

Wajerumani na wakaazi wa Ulaya waamka kwa mshangao baada ya kushindwa mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano wa vyama vinne unaojulikana kama "Muungano wa Jamaika" mjini Berlin.

Ines Pohl Kommentarbild App
Picha: DW/P. Böll

Baada ya Brexit na Trump, sasa kinachomoza kisa chengine: Safari hii kinamhusu Angela Merkel aliyeshindwa angalao kwa sasa kuunda serikali. Katika nchi hii tulivu inayonawiri kiuchumi na inayojikuta kati kati ya bara la Ulaya, injini ya Umoja wa ulaya, wiki nane baada ya uchaguzi mkuu, bado haijukiani mambo yataendelea vipi. Muda mfupi kabla ya saa sita za usiku, Christian Lindner, kiongozi wa chama cha kiliberali cha FDP ametangaza kuvunjika mazungumzo akihoji bora kutokuwa na muungano kuliko kuwa na muungano wa hadaa.

Kishindo cha vyama saba bungeni

Mmatamshi hayo yamefuatia majadiliano makali ya kutathmini uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano, mazungumzo ambayo tokea mwanzo yalibainika kuwa ya muungano wa masilahi na sio wa mapenzi. Kwa muda wote huo pande zilizohusika  na mazungumzo hayo hazikufanikiwa kuzigeuza tofauti zao kuwa faida..

 Kwa mara ya kwanza chama cha siasa kali za kihafidhina, AfD kimefanikiwa kuwakilishwa katika bunge al shirikisho Bundestag-na hali hiyo imevuruga uwezekano wa kuundwa serikali. Si rahisi kufikia ufumbuzi katika bunge ambalo vyama saba vya kisiasa vinawakilishwa. Baada ya SPD kutangaza tangu mwanzo wanakalia viti vya upinzani, na kwa namna hiyo kutoweka pia uwezekano wa kuundwa serikali nyengine ya muungano wa vyama vikuu, kansela Angela Merkel akajikuta akilazimika baada ya miaka 12 madarakani, kujiunga na mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano ingawa alitambua tangu mwanzo hana nguvu za kukiwakilishwa ipasavyo chama chake . Kutokana na kudhoofika chama chake baada ya uchagzi mkuu uliopita, kansela Merkel pia amedhoofika na ndio maana ameshindwa.

 Suala la wakimbizi ndio mzizi wa fitina

Yadhihirika kana kwamba FDP ndio waliomzuwia Angela Merkel kuunda serikali mpya ya muungano. Mzizi wa fitina ni suala la wakimbizi. Msimamo wa kiliberali wa Angela Merkel kuelekea wakimbizi ndio uliowapatia nguvu AfD. Na mwishoe yadhihirika kana kwamba suala hilo hilo ndio chanzo cha kushindwa mazungumzo ya kuunda serikali mpya. Huo lakini si ushahidi kwamba yalikuwa makosa kuwasaidia watu wanaohitaji kusaidiwa. Kushindwa kuundwa serikali mpya kunabainisha kwamba Ujerumani pia inajikuta njia panda. Na kwamba licha ya neema za kiuchumi, watu bado wanahofia  wimbi la wakimbizi lisije likavuruga mustakbali wao katika ulimwengu huu wa utandawazi.

 

Jumatatu ya leo sio wajerumani peke yao walioamka kwa mshituko, bali Ulaya nzima. Kwasababu wiki kadhaa kama si miezi inatusubiri na hakuna anaejua nini kitatokea.

Mwandishi: Pohl Ines/Hamidou Oummilkheir

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW