1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mbali na dosari kadhaa, amani na umoja vitawale

30 Oktoba 2020

Wagombea wa upinzani Tanzania walibugudhiwa na kukamatwa. Kumekuwa na vurugu na vitisho, hata hivyo Watanzania wanapaswa kusimama imara kudumisha amani na umoja, anaandika Grace Kabogo katika maoni yake.

Tansania | Präsidentschaftswahlen
Picha: Ericky Boniphace/DW

Dosari kadhaa ikiwemo kusimamishwa kwa baadhi ya wagombea wa upinzani kufanya kampeni kwa siku kadhaa kwa madai ya kukiuka maadili ya uchaguzi, wengine kuondolewa kwenye kinyang'anyiro isivyo halali, ghasia zilizosababisha mauaji zilishuhudiwa, mawakala kuzuiwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura, mawasiliano kutatizwa na huduma za intaneti kupungua kasi zimesababisha hali ya sintofahamu miongoni mwa Watanzania.

Baadhi yao tayari wamesema wamepokonywa haki yao ya uchaguzi, huku baadhi ya viongozi wa upinzani wakiwataka wafuasi wao waingine mitaani kudai haki yao kwa njia ya amani. Je tunahitaji kweli kuingia mitaani, iwapo matokeo yatakuwa yamechakachuliwa? Hapana, sidhani hivyo ingawa kulingana na katiba ya Tanzania matokeo ya uchaguzi wa urais yanayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC, hayawezi kupingwa mahakamani.

Muda kwa wanaharakati wa demokrasia kujitokeza zaidi

Sheria ya sasa hairusu matokeo ya urais kupingwa katika mahakama kama ilivyo kwa matokeo ya ubunge na udiwani. Mtu anaweza kufikiria kwamba kihalali sasa ni muda muafaka kwa vyama vya siasa, mashirika ya kiraia na watetezi wa haki za binaadamu, kuendelea kushinikiza mabadiliko ya katiba ili kuiondoa sheria hii iliyopitwa na wakati.

Watanzania wanapaswa kukumbuka kwamba uchaguzi umemalizika na wana jukumu kubwa na safari ndefu sana kama taifa baada ya uchaguzi, kuilinda amani kwa gharama yoyote ile. Hivyo matokeo ya uchaguzi yasiwe sababu ya kuwepo uhasama. Uchaguzi unakuja na kuondoka, na mwisho wa siku anapatikana mshindi mmoja tu, awe kutoka chama tawala au upinzani. Matokeo hayapaswi kuwagawa Watanzania, bali yasaidie kuwaleta pamoja ili kulijenga taifa katika miaka mitano ijayo na wasahau tofauti zao za kisiasa.

Grace Kabogo, DW KiswahiliPicha: DW/L. Richardson

Serikali mpya kwa kushirikiana na vyama vyote vya kisiasa wanapaswa kujitathmini kuhusu dosari zilizojitokeza na kuzirekebisha, kwa lengo la kujipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao wa 2025. Serikali hiyo ihakikishe inaelekeza na kuitekeleza mipango na miradi ya maendeleo kwenye maeneo yote yenye mahitaji bila ubaguzi wowote ule, na bila kujali wananchi walichagua upande gani. Inapaswa pia kuweka mazingira mazuri ambayo kwa mara nyingine, vyama vyote vya kisiasa vitajisikia viko salama katika kutekeleza majukumu yao.

Taasisi za serikali zinapaswa pia kupinga mwelekeo wowote unaojihusisha na siasa na badala yake zitoe fursa sawa kwa vyama vyote vya siasa na kulinda uhuru wa kila mmoja ili kupata nafasi ya kushiriki katika shughuli za kisiasa, bila ya kuwa na hofu.

Tume mpya ya uchaguzi inahitajika 

Watu wa Tanzania wameonyesha hamu ya kidemokrasia na serikali ijayo haipaswi kulipuuza suala la Tume Huru ya Uchaguzi, kama msingi wa haki na amani, ambalo kwa miaka sasa limekuwa likidaiwa na wapinzani, ambayo itakuwa na uwezo wa kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Maendeleo ya Tanzania yanahitaji amani, utulivu na umoja; tunu zinazojengwa katika misingi ya maelewano, mshikamano na maridhiano. Kama ambavyo Baba wa taifa la Tanzania na rais wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema: ''Demokrasia sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuagiza. Demokrasia inapaswa kuendelezwa kulingana na nchi husika.''

Wananchi wote, kwa pamoja wanapaswa kutambua kwamba wana jukumu la kuilinda na kuidumisha amani, ambayo nchi yao imeifurahia tangu ilipopata uhuru 1961.

Uchaguzi sio kuhusu nani anayeshinda, lakini pia ni kuhusu nini kinafuata na maana yake kwa wananchi. Je serikali mpya ya Tanzania itakuwa na nia ya kuirekebisha taswira yake, itataka kuangalia mwelekeo wake wa kidiplomasia au kuhakikisha demokrasia haikandamizwi? Haya yote yatategemeana na utashi wa serikali mpya, ambayo itatoa mwangaza wa wapi Tanzania inaelekea katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW