1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Miaka 100 baada ya Vita Vikuu II yaliyopita ni ndwele

Daniel Gakuba
12 Novemba 2018

Ulaya ya miaka 100 baada ya Vita Vikuu vya II bado imejaa hofu na tahadhari ya kutokea tena kwa uhasama, na walioamini kwamba umwagaji damu wa Ypres na Verdun ni kumbukumbu tu ya kihistoria, wanapaswa kufikiria upya.

Frankreich Nationalfriedhof Douaumont Gedenken Schlacht von Verdun
Picha: Reuters/P. Wojazer

Maadhimisho ya miaka 100 tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili, yalipaswa kuwa wakati ambapo historia ya Ulaya ingebaki kuwa kumbukumbu katika majumba ya makumbusho. Siku ambapo viongozi wangeshikana mikono, wakiwa na uhakika kwamba baada ya miaka 100, machungu ya Vita Vikuu vya Kwanza yangekuwa tu mada kwa wanahistoria. Lakini ghafla hali ya kutisha na yenye kutoa tahadhari imejidhihirisha mahali kama Ypres au Verdun, ambapo vijana wengi wa Ulaya walimwaga damu yao. 

Alipozungumza mbele ya hadhara iliyowajumuisha viongozi wa mataifa 60 mjini Paris, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema kwamba historia wakati mwingine hufuata nyayo za njia yake ya zamani ya hatari, na kuharibu amani ambayo tunaamini ilitiwa muhuri kwa damu ya mababu zetu.

Katika hotuba yake, Macron alitahadharisha dhidi ya mapepo wabaya na itikadi mpya ambavyo kwa mara nyingine tena vinatishia amani. Kwa hali ya kupoteza mwelekeo, nchi za kidemokrasia za Ulaya zimeanza kufuata mkondo usioeleweka vyema.

Siasa za uchochezi na uhamasishaji

Katika nchi kama Poland, Italia na Hungary, viongozi wenye sera kali za mrengo wa kulia wanajinufaisha na hali ya wasiwasi miongoni mwa watu wao, na kutumia historia kama silaha kuhujumu mustakhabali wa pamoja wa Ulaya. Ishara hizi kutoka karne ya 20 zimerudi.

Makundi ya walio wachache yanageuzwa kisingizio cha yote mabaya katika jamii.Ukitazama kwa makini unamuona Salvini nchini Italia, ambaye anawaumbua watu wa jamii ya Gypsies na wahamiaji, kwa kuhubiri chuki katika mitandao ya kijamii. Nchini Poland, Jaroslaw Kaczynski anatia sumu katika mahusiano kati ya nchi yake na majirani zake, akiimarisha utawala wa kiimla. Viktor Orban wa Hungary natumia kila mbinu ya kifashisti, kama chuki ya wayahudi na chuki dhidi ya wageni, ili serikali yake ya kifisadi iendelee madarakani.

Nchini Ufaransa yupo Marine Le Pen anayehubiri sera ya kujifungia ndani ya mipaka ya kitaifa, na nchini Uingereza, Boris Johnson anaazimia kuitumia Brexit kama chombo cha kurejesha himaya ya Uingereza.

Kinachotenganisha maisha ya amani kila siku yanayoendela barani Ulaya, na janga linaloweza kufuatia vuguvugu hili la kisiasa, ni mikataba ya Umoja wa Ulaya, na wanasiasa wachache wenye kuwajibika.

Wasiwasi utokanao na mabadiliko unajenga pengo katika jamii

Raia wengi wa Ulaya wanahadaika na simulizi za nema za siku zilizopita. Hawaelewi changamoto zitokanazo na maendeleo ya teknolojia, na wanajihisi kukabiliwa na kitisho, na wanahani wametelekezwa.

Katika ombwe hilo wanajitokeza wanasiasa wanaowakumbusha kengele ya kanisa kongwe wanakotoka, ambalo wanasiasa hao wanasema linatishiwa na Uislamu, hata kama hawajakanyaga kanisani kwa miaka mingi.

Wakati mwingine wanasiasa hao huchechea chuki dhidi ya majirani, wakiwaita maadui wa taifa, kama inavyofanyika nchini Italia dhidi ya Wajerumani, au nchini Uingereza, dhidi ya raia wa nchi nyingine za Ulaya.

Wanasiasa hao wanavyo viungo vyote wanavyoweza kuvichanganya na kutengeneza sumu ya utaifa, ya kuwatenga wengine, kuwachukia wakosoaji na kurudisha ghasia zilizosababisha majanga ya miaka 100 iliyopita.

Katika mkutano wa wanasiasa wa vyama vya demokrasia ya kikristo, Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk ambaye anatoka nchini Poland, aliwaonya kwa lugha ya wazi kabisa wanasiasa hao, kwamba wanakaribia kusukumwa pembezoni mwa mchakato wa kidemokrasia. Kwa bahati mbaya, kwa kuzingatia hali halisi katika nchi kama Austria, tayari hilo ni dhahiri.

Miaka 100 tangu kumalizika kwa vita vikuu vya kwanza, ukiangalia kwa makini unaona ukweli wa kutisha, kwamba yaliyopita sio historia, kwamba yanaendelea.

Mwandishi:  Barbara Wesel

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri: Grace Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW