1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIndonesia

Mkutano wa G20 waonyesha umuhimu wa mataifa yanayoinukia

Daniel Gakuba
17 Novemba 2022

Indonesia imeunusuru mkutano wa kilele wa G20, ambao ulielekea kushindwa kutokana na tofauti juu ya vita vya Ukraine. Kwa hilo, imehalalisha raia ya nchi zinazoinukia kuwa na sauti, anasema Alexandra von Nahmen wa DW.

Tangu mwanzoni kabisa mwa mkutano huo wa kilele wa G20, rais wa Indonesia Joko Widodo alitoa wito wa kukomeshwa kwa vita, na aliuzungumzia uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, na huo ulikuwa mwelekeo wa mkutano huo kwenye kisiwa cha Bali.

Soma zaidi: Urusi kuridhia taarifa ya pamoja mkutano wa G20 ukimalizika

'Kama vita hivi havitamalizika, itakuwa vigumu kwetu kutimiza wajibu wetu kwa vizazi vya baadaye,'' alisema rais huyo. Kauli yake hiyo ingesikika kama ya kutia huruma, lakini ilitanguliwa na miezi kadhaa ya diplomasia iliyofanyika nyuma ya pazia.

Alexandra von Nahmen-DWPicha: DW

Widodo alizizuru Moscow na Kiev, na alikataa shinikizo la kuitenga Urusi katoka kundi la G20, lililotoka hasa katika nchi za magharibi. Indonesia ambayo ilikuwa mwenyekiti wa kundi hilo hadi jana Jumatano, iliazimia kuufanya mkutano wa Bali kuwa wenye mafanikio.

Indonesia, mwenyeji aliyeandaa mkutano kwa weledi

Ukweli kwamba, kinyume na ilivyotarajiwa, mkutano huo wa kilele uliweza kutoa tangazo la pamoja, lisemalo wazi kuwa sehemu kubwa ya nchi wanachama inalaani uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, ni sifa kwa Indonesia. Wanadiplomasia wanasema nchi hiyo mwenyeji iliuandaa mkutano vizuri na kuuendesha kwa werevu, ingawa ulianza vibaya.

Soma zaidi: Biden na Xi wakutana mjini Bali nchini Indonesia

Kulikuwapo hofu kuwa Urusi na China zingezuia kila azimio, na kwamba mataifa yanayoinukia yangechelea kuikosoa Urusi, na kwamba mkutano huo ungeambulia patupu.

Ulaya pia ilifanikiwa katika mkutano wa G20

Mafanikio hayo ya Indonesia yanaweza kuchukuliwa pia kama ufanisi kwa Umoja wa Ulaya, ambao tangu kuanza kwa vita vya Ukraine ulifanya juhudi kuzishawishi nchi zinazoinukia kuwa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine haukuwa na sababu yoyote ya kuuhalalisha. Pia umoja huo ulifafanua bila kuchoka, kuwa vita hivyo ndivyo sababu ya upungufu wa chakula na mfumko wa bei.

Lakini Ulaya pekee isingeweza kuushawishi mkutano wa Bali, kwa sababu uongo wa Urusi kuwa vikwazo vya nchi za magharibi ndivyo mzizi wa matatizo bado unakubalika katika baadhi ya sehemu duniani.

Soma zaidi: Zelensky awaambia viongozi wa G20 kuna taifa la kigaidi kati yao

Urusi kwa hali ya kipekee inatumia udhaifu wa nchi za magharibi, na hisia za kuichukia Marekani, kupigia debe ushawishi wake, na bado katika sehemu hizo Putin anaonekana kama mtu mwenye nguvu.

Bali kama jukwaa la mkutano baina ya Marekani na China

Vile vile mkutano wa kilele kisiwani Bali ulikuwa jukwaa la mazungumzo baina ya Rais Joe Biden wa Marekani na mwenzake wa China Xi Jinping, ambao umelegeza mivutano na pengine kupunguza uungaji mkono wa China kwa Urusi, angalau kwa muda.

Bila shaka, mwisho wa yote maazimio ya mkutano ni karatasi tu, na Indonesia yumkini inachokifuata ni maslahi yake. Miaka mitatu inayofuata, uenyekiti wa G20 utayaendea mataifa yanayoinukia, India mwaka 2023, Brazil mwaka 2024 na Afrika Kusini mwaka 2025. Nchi hizo zitataka umuhimu wa kundi hili kuimarika, sio kudhoofika. Lakini pia zitapigania mazungumzo yenye usawa baina ya mataifa wanachama.