Mkutano wa kirafiki
12 Juni 2018Nani angeweza kuamini kuwa hilo lingewezekana? Kwa uhakikisho juu ya usalama wake, Korea Kaskazini itaachana na mpango wake wa silaha za nyuklia, inahitaji kutazama mbele na kufanikisha mabadiliko ya kweli katika mahusiano. Ni jambo la kutia matumaini na hisia kubwa za ahueni zinasambaa.
Miezi michache iliopita ilionekana kana kwamba mgogoro huu usiokoma ulikuwa unazidi makali, wakati ambapo wawili hao walipotoleana maneno makali, na Trump kutishia mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa, kuisambaratisha Korea Kaskazini. Na sasa wawili hao wameshikana mikono na wanatafuta makubaliano ya amani.
Ushindi kwa Trump na Kim
Trump ameweza kujidhirisha - hasa mbele ya raia wa nchi yake, kama mwanadiplomasia mkubwa aliefanikisha amani katika mgogoro ambao ulikuwa hautatuliki. Kwa namna fulani, ni jambo la kustajaabisha kwamba Trump aliekosolewa sana ameweza kupiga hatua katika mgogoro huu wa muda mrefu, na yumkini akawa rais wa Marekani anaeweza kusaini makubaliano ya amani na Korea Kaskazini siku za usoni.
Si marais wademokratic Bill Clinton na Barack Obama, wala Warepublican George Bush mkubwa na mdogo waliweza kufikia mafaniko kama hayo, na hivyo mtu anapaswa kutoa shukuran kwa rais huyu asietabirika.
Lakini Kim pia anaweza kujihisi kama mshindi: Kwa kizazi hiki cha tatu cha familia ya Kim, hatua hii iliofikiwa ni mafanikio makubwa. Kwanza alitumia ubabe kulaazimisha mazungumzo na kisha akaweza kukutana ana kwa ana na rais wa Marekani.
Utawala wake haupaswi kuishia kama wa Saddamu Hussein au Muammar Ghadafi na hivyo amejiweka katika hatari ya kudhibitiwa. Na wakati huo huo, Kim kwa ueledi mkubwa amepata uungaji mkono wa China na Urusi. Hivyo madola hayo mawili yalikuwepo kwenye mkutano wa Singapore bila kuonekana, kama ilivyokuwa kwa Japan, ambayo haitaki kupoteza ushawishi wake kwa Marekani katika kanda hiyo.
Kujengan imani kunachukuwa muda
Hatua ya kwanza muhimu imepigwa, lakini kujenga uaminifu kunahitaji muda, na kama wanavyosema, vipengele vidogo vya makubaliano kama hayo ndiyo vinaweza kusababisha matatizo makubwa baadae, kama ilivyotokea kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran, ambao Trump aliutupilia mbali.
Lakini pia ikiwa rasi ya Korea itapata amani swali litakuwa ni namna gani Marekani itajipanga katika kanda ya Asia, kwa kuzingtia nguvu na ushawishi wa China vinavyozidi kuimarika.
Katika Mkutano huo wa Singapore, Trump ameweza kudhihirisha jukumu kuu la Marekani kama taifa kubwa kwenye jukwaa pana. Wakati meli za kivita za Marekani zinapofanya doria kwenye njia za bahari zilizowazi barani Asia au kutia nanga katika bandari rafiki, ujumbe unasalia ule ule - kwamba tunapinga mahasimu kama China, na tuko pamoja na washirika wetu.
Mwisho wa ushawishi wa Marekani
Lakini mashaka yanazidi iwapo Marekani itaweza tena, kama ilivyofanya miaka 65 iliopita katika vita vya Korea, kutuma wanajeshi vijana, kupigania demokrasia na uhuru katika upande huo wa dunia, na inapowezekana kufia dhamira hiyo.
Kwa sera yake ya "Marekani kwanza", viwango vya ushuru wa forodha vinavyonuwia kuwaadhibu washirika wake na ukiukaji kadhaa wa makubaliano, Trump pia hajajenga uaminifu na kanda ya Asia.
Na hivyo, mbali na siasa za kiishara, mkutano huu wa kihitoria wa Singapore unaashiria mwanzo wa mwisho wa Marekani kama polisi wa dunia na msimamizi wa kuaminika wa amani.
Mwandishi: Alexander Freund
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman