1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mshikano una kasoro unapowaacha nje Waafrika Ukraine

Josephat Charo
3 Machi 2022

Ulimwengu umeungana kwa kauli moja kuonesha mshikamano na watu wanaokimbia vita nchini Ukraine - Mshikamano lazima ujumuishe kila mtu. Ndivyo anavyosema mwandishi wa DW Wafaa Albadry katika uhariri wake.

Ukraine-Krieg | Flüchtlinge aus Afrika und Asien
Picha: ROBERT GHEMENT/EPA-EFE

Uvamizi wa kushtusha wa Ukraineunatishia mamilioni ya maisha ya watu. Nusu milioni wamekimbilia nchi jirani kutafuta hifadhi katika kipindi cha wiki moja, na mamia kwa maelfu wamelazimika kuyakimbia makazi yao. Wanaume wa Ukraine wametenganishwa na wapendwa wao na wamebaki ili kupigana nchini huku familia zao zikikimbia mguu niponye kutafuta usalama na hifadhi, wakiwa na kiwewe na kukosa uhakika wasijue kitakachotokea katika maisha yao.

Watu wanasema vita hudhihirisha mazuri na mabaya ndani ya binadamu. Katika mizozo hii watu katika nchi jirani na karibu nchi zote wanaifungua mipaka, makazi yao, na hata mikono yao kuwasaidia wanaokimbia machafuko. Mashirika ya misaada, watu wa kawaida na wanasiasa kote ulimwenguni wanaonesha mshikamano. Kwa hiyo watu wengi wanajaribu kusaidia kwa njia moja au nyingine - na hii inatia moyo.

Lakini pia kuna upande wa pili wa shilingi, upande ambao ni jinamizi kwa watu weusi na wengine wenye asili mataifa mengine wanaonyimwa ruhusa ya kuvuka mipaka na kuingia maeneo yenye usalama. Watu wengi wanaotokea Afrika, Mashariki ya Kati na maeneo mengine wanaoishi nchini Ukraine hawakukaribishwa kama walivyokaribishwa wengine.

Wengi walinyimwa fursa ya kupanda treni au mabasi yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya kuwasafarisha wakimbizi kutoka Ukraine kuwapeleka maeneo salama, wakaambiwa raia wa Ukraine pekee waliruhusiwa. Na walipowasili mpakani kwa miguu, walizuiwa na wakasukumwa nyuma katika baadhi ya mipaka ya Poland.

Wanakabiliwa na kitisho, wana hofu, na wamevunjika moyo kama walivyo watu nchini Ukraine. Hii ni aina gani ya mshikamano unaowabagua na kuwaacha nje wasipate msaada?

Wafaa Albadry wa DWPicha: S. Overdhal

Wanafunzi wa kigeni waliokesha mara kadhaa karibu na mipaka ya Poland walisema pia walinyimwa fursa ya kupata chakula na maji, mahitaji muhimu yaliyogawanyiwa wale waliokuwa wakisubiri kuvuka mpaka. Walilazimishwa kurudi nyuma katika maeneo ambayo yanashambuliwa kwa mabomu na kutafuta njia mbadala ya kujiokoa.

Zaidi ya wanafunzi 76,000 wa kimataifa wanasoma nchini Ukraine, na zaidi ya asilimia 25 wanatokea India na nchi za Kiafrika, zikiwamo Nigeria, Morocco na Misri. Kuna wafanyakazi na wahamiaji ambao pia walihitaji kupata eneo salama.

Familia zao nyingi upande wa pili wa ulimwengu wana wasiwasi. Hata wakifanikiwa kukimbia kutoka maeneo yanayoshambuliwa kwa mabomu, wataishi vipi kwa kusukumwa na kukataliwa kwa siku kadhaa bila msaada? Hali hiyo imeibua taswira ya kutisha zaidi ya kile kinachoendelea huko: Kwa wale ambao si wazungu, ni vita na ubaguzi.

Ubinadamu wa kuchagua?

Katika mitandao ya kijamii, video zinasambaa za waafrika wanaoomba msaada na zinazoonesha ubaguzi uliowakabili. Kutoka maafisa wa usalama waliowanyoshea mitutu ya bunduki wanafunzi waliopiga kelele kusema hawajajihami na silaha, hadi video inayoonesha mtoto kuwa miongoni mwa wale walioachwa wapigwe na baridi.

Kauli za chuki mtandaoni muda mfupi baadaye zilianza kuwaandama

Watu walituma upuuzi, wakiwatuhumu watu weusi kwa kutokuwa wastaarabu vya kutosha kiasi cha kuokolewa. Wanadai kipaumbele kinatakiwa kupewa wazungu. Wanasema watu weusi na wengine wenye asili ya mataifa mengine wanatakiwa wabaki na wapigane nchini Ukraine, kana kwamba walikuwa na haki ya kuchagua ni nani anastahili kupata ulinzi na nani lazima avikabili vita. Inatamausha - na ni ubaguzi wa wazi kabisa. Haukubaliki, hili ni wazo la kijinga kwamba huruma inategemea rangi ya ngozi ya mtu. Na ni aibu kubwa kweli kweli kwamba hali hii inatokea wakati wa vita.