1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mtazamo nchini Mali unahitaji kuwa watu, siyo jeshi

18 Februari 2022

Hakuna alieshangazwa Mali na kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa na Umoja wa Ulaya. Sasa ni wakati wa kupitia mikakati ya zamani na kuacha kushirikiana na mafisadi, anasema mkuu wa idhaa ya Kifaransa ya DW Dirke Köpp.

Mali I Unruhen I Konflikt
Picha: Michele Cattani/AFP/Getty Images

Baada ya vitisho vingi na uahirishaji mwingi, hatimaye Ufaransa na washirika wake wa Umoja wa Ulaya walitangaza siku ya Alhamisi kwamba wataondoa wanajeshi wao kutoka Mali. Walisema kwamba mpango wao ulikuwa kuendelea kupambana dhidi ya ugaidi katika kanda ya Sahel kutokea taifa tofauti.

Nchini Ujerumani, tangazo hilo limesababisha mshtuko kwa sababu ya ushiriki wa jeshi la nchini hiyo Bundeswehr. Hata hivyo, nchini Mali kwenyewe, wengi wanaonekana kutojali, na kwa hakika wengi wamefurahia kuondoka kwa Ufaransa.

Kuna sababu nyingi za hali hii. Mojawapo ni mfumo wa "Francafrique", ambao ni utaratibu ambao kupitia kwake, taifa la Ufaransa limetumia kwa miongo kadhaa, na kwa kushirikiana na watawala mafisadi katika mataifa mmoja mmoja, kunyonya rasilimali za Afrika. Watu wengi katika mataifa ya Afrika yanayozungumza Kifaransa wamechoka kabisaa na mfumo huu - na wako sahihi.

Wanaonufaika na wimbi la chuki dhidi ya Ufaransa

Wakati huo huo, Urusi imetumia fursa hii ya chuki dhidi ya Ufaransa kwa malengo yake yenyewe -- ambayo bila shaka siyo mazuri sana kuliko ya wengine wengi. Zaidi ya kuzinyemelea rasilimali kama vile dhahabu, urani au vito, Moscow inalenga hasa ushawishi wa kimkakati katika eneo hilo. Na vivyo hivyo watumiaji wa mitandao wa Urusi  wameijaza mitandao ya kijamii na propaganda dhidi ya Ufaransa, habari za uongo na madai ya simulizi za ufanisi wa operesheni za kijeshi za Urusi.

Rais wa mpito wa Mali Assimi Goita (kulia) na waziri mkuu wa nchi hiyo Choguel Kokalla Maiga (kushoto) wakiwa katika sherehe ya siku ya jeshi mjini Kati, Januari 20, 2022.Picha: FLORENT VERGNES/AFP

Utawala wa kijeshi wa Mali, ambao ulipatiwa mafunzo barani Ulaya, lakini pia nchini Urusi, pia unatumia wimbi za chuki dhidi ya Ufaransa kujiimarisha madarakani. Kwa miezi kadhaa umekuwa katika mapambano ya kidiplomasia na Ufaransa, na wakati huo huo ukiimarisha ushirikiano wa kijeshi na Urusi, ushirikiano ambao umekataa kuuweka wazi kwa washirika wake. (Ushirikiano huo ni kati yake na mamluki kutoka kundi la Wagner au na jeshi la kawaida la Urusi)

Soma pia: Je hatua mpya za kupambana na ugaidi Sahel zinajitosheleza?

Kilicho bayana ni kwamba Ufaransa na Umoja wa Ulaya wana undumila kuwili. Na hiki ndiyo hasa kimewachukiza Wamali wengi. Wakati viongozi wa mapinduzi Mali wamewekewa vikwazo, rais wa mpito wa Chad anaendelea kukaribishwa, licha ya ukweli kwamba hata yeye alinyakua madaraka kwa njia isiyo ya kidemokrasia kabisaa, baada ya kifo cha kisichoelezwa cha baba yake wa kuasili.

Linahitajika suluhisho lisilo la kijeshi

Mkuu wa idhaa ya Kifaransaya DW, Dirke Köpp.Picha: DW

Mtu hahitaji kufikiria kwa zaidi ya sekunde kuelewa kwamba suluhisho la Sahel haliwezi kuwa la kijeshi. Wanachotaka watu kwenye kanda hiyo ni maendeleo, mifumo ya kitaifa ya kuaminika na matarajio ya mustakabali salama. Na hii haimaanishi tu kuwalinda dhidi ya magaidi. Ni suala la kuendelea kuishi.

Ingekuwa bora zaidi kwa watu wa kanda ya Sahel endapo mabilioni ya euro yangewekezwa katika kuziendeleza jamii zao, kama yanavyowekezwa kwenye jumbe za kijeshi.

Ingekuwa hata bora zaidi iwapo kila kitu kilifanywa kuhakikisha fedha zinazowekezwa haziishii katika mifuko ya watawala mafisadi. Hali ni ya janga. Mavuno ama yanakauka au yanafurika kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Kuna idadi inayoongezeka ya watu wanaohitaji kulishwa kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya watu. Serikali haiko katika maeneo mengi, na majambazi wameachwa kusababisha vurugu.

Soma pia: Mali yashindwa kulipa madeni yake

Katika baadhi ya maeneo, wapiganaji wa itikadi kali wameunda mifumo mbadala ya kodi. Kuna kazi kidogo sana. Kuna hospitali chache. Na barabara nyingi ziko katika hali mbaya.

Zaidi na zaidi, wanachama wa makundi tofauti ya kikabila wanazoza kwa sababu ya rasilimali, ambazo zinazidi kuwa haba. Mamilioni ya watu wako hatarinini kukumbwa na njaa na kukosa chakula. Mamilioni wametoroka. Mamilioni ya watoto hawawezi kwenda shule kwa sababu ya kitisho cha ugaidi. Kizazi kilichoptea kinakua.

Mwanajeshi wa Ufaransa kutoka kikosi cha Barkhane mbele ya gari la wanajeshi wa Mali.Picha: Frederic Petry/Hans Lucas/picture alliance

Hatua za kukata tamaa

Mapambano ya kila siku na ukosefu wa matarajio vinawasababishia wengi kukata tamaa. Hivyo inaweza kuwa rahisi wa wapiganaji wa itikadi kali kuwavutia watu kwa ahadi ya maisha bora na pesa. Hizi siyo shutuma na siyo kila moja anavutiwa na mapendekezo ya magaidi. Lakini ni watu wangapi wako salaama barani Ulaya wanaweza kusema kwa uhakika kwamba wanaweza kukataa vishawishi kama hivyo iwapo familia zao zitakuwa hatarini?

Kwa muda mrefu sana, jumuiya ya kimataifa imeweka karata yake kwenye suluhisho la kijeshi tu. Sasa, inapaswa kutafuta njia nyingine za kuwasaidia watu waliotelekezwa wa kanda ya Sahel.

Soma pia:Mali yampa balozi wa Ufaransa saa 72 kuondoka nchini humo

Hii inamaanisha kuwachukulia wao na mahitaji yao kwa uzito. Inamaanisha kushirikiana nao kutafutua suluhisho la ndani. Inamaanisha kuhakikisha kuwa watoto wanaweza kwenda shule na wazazi wanaweza kurejea mashambani bila kuwa na hofu.

Ikiwa hii inamaanisha kuzungumza na makundi yenye silaha kwanza, basi hii ndiyo njia ambayo inapaswa alau kukubaliwa. Katika baadhi ya maeneo, mikakati kama hii imepelekea watu kuishi katika usalama zaidi.