1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Maoni: Mwaka 2022 ulikuwa wa wanawake

27 Desemba 2022

Ingawa Putin anaendeleza vita vyake nchini Ukraine na Ayatollah wa huko Iran anatumia kifo kuwaadhibu wakosoaji wa serikali yake, mimi binafsi ninauona mwaka 2022 kuwa ulikuwa ni mwaka wa wanawake, anasema Astrid Prange.

Bulgarien Protest gegen den Ukraine-Krieg in Sofia
Picha: Georgi Paleykov/NurPhoto/IMAGO

Wanawake wenyewe walianzisha mapambano dhidi ya wababe wa vita, kwa namna waliyoiona wao inawafaa katika kipindi chote cha mwaka 2022.

Nchini Iran baada ya kifo cha Mahsa Amini Septemba 16, wanawake walianzisha vuguvugu dhidi ya utawala wa kidini. Picha za wanake wa Iran wakikata nywele zao na kuvua hijab ziliwavutia wengi ulimwenguni. Harakati zake juu ya haki za wanawake ziliongezeka na kuwa vuguvugu la kuupinga utawala wa Tehran. Mamilioni ya watu wakashinikiza uhuru na kuhitimishwa kwa utawala huo wa kidini.

Soma Zaidi:Raia wa Iran waendelea kuandamana licha ya onyo la Mahakama

"Si yeye!"

Na huko Brazil ni nguvu ya wapiga kura wanawake ndio hasa ilimuondoa madarakani rais aliyetambulika kwa ubaguzi na chuki dhidi ya wanawake. Jair Bolsonaro, aliyeyafananisha maradhi ya UVIKO-19 kama mafua tu na hata kudiriki kutamka wazi kwamba anajuta kwa nini wakosoaji waliteswa tu badala ya kuuawa wakati wa utawala wa kidikteta alilazimika kuondoka kwenye makazi ya rais. Kampeni kama za ElNao ikimaanisha "hafai" iliwasaidia wanawake wa Brazil kumrejesha rais Inacio Lula da Silva aliyewahi kuitawala Brazil kati ya mwaka 2003 hadi 2011, baada ya kupata ushindi mwembamba.

Nikiangalia huko kwenye maeneo ya Palestina wanawake wameonekana kuchukua jukumu kubwa kupambana dhidi ya manyanyaso ya wanajeshi. Kufuatia kifo cha mwandishi wa habari mwenye asili ya Marekani na Palestina Shireen Abu Akleh Mei 11, ndugu yake Lina sasa anaongoza kampeni ya kuwajibishwa wahusika wa kifo hicho. Kutokana na mafanikio ya kampeni yake, jarida la Marekani la Time limemtaja kwenye orodha ya viongozi vijana wenye ushawishi mkubwa zaidi kwa mwaka 2022.

Shireen Abu Akleh kabla ya kufikwa na mauti baada ya kupigwa na risasi akiwa kazini.Picha: Al Jazeera Media Network/AP/picture alliance

Ikumbukwe kwamba Shireen Abu Akleh alifariki akiwa anaripoti uvamizi wa vikosi vya Israel, IDF katika eneo wanalolikalia kimabavu la Ukingo wa Magharibi. Taarifa ya mwisho ya maafisa juu ya uchunguzi wa kifo hicho kutoka upande wa jeshi la Israel ilisema kile ilichotaja kama uwezekano mkubwa kwamba mwandidhi huyo wa habari wa Al-Jazeera aliuawa kwa bahati mbaya wakati wa makabiliano kati ya vikosi vya Israel na waPalestina waliojihami kwa silaha.

Rekodi ya uhalifu wa kivita.

Nchini Ukraine, wanawake wenye ujasiri mkubwa wanapambana dhidi ya uvamizi wa Urusi na uhalifu wa kivita chini ya kivuli cha rais Volodymyr Zelensky. Mshindi wa tuzo ya kimataifa ya amani ya Nobeli Oleksandra Matviichuk, ambaye ni mwanzilishi wa shirika la haki za binaadamu la Center for Civil Liberty, anataka kufungua mashitaka ya uhalifu wa kivita uliofanyika huko Ukraine, Syria, Mali na Georgia, mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC. Shirika hilo lililoanzishwa na mwanasheria mwaka 2007, lilikuwa la kwanza kurekodi visa vya uhalifu vilivyofanywa na jeshi la Urusi katika Rasi ya Crimea, Luhask na Donesk. Alitunukiwa tuzo ya Nobeli mwaka 2022 kutokana na kazi yake hiyo.

Na hata kazi kubwa ya daktari wa watoto Irina Kondratova aliyejulikana baada ya mwanasoka wa Uingereza David Beckham kumpa akaunti yake ya Instagram, anatambuliwa na mamilioni ya watu kwa juhudi yake ya kuwasaidia wanawake wajawazito na watoto wachanga wakiwa mafichoni kwenye vyumba vya chini ya ardhi huko nchini Ukraine na kusahau kwa muda hatari iliyopo mbele yao.

Rais wa Halmashauri ya Ulaya Ursula von der Leyen naye amekuwa na mchango muhimu katika kuongeza mbinyo dhidi ya Urusi.Picha: Olivier Matthys/AP/picture alliance

Na kwenye ngazi za juu kabisa za Umoja wa Ulaya, rais mwanamama Ursula Vod der Leyen naye ameendelea kuratibu msururu wa vikwazo vya umoja huo dhidi ya wanasiasa wa Urusi, jeshi na hata benki. Von der Leyen amefanikiwa kuushawishi Umoja wa Ulaya kuiunga mkono Ukraine, licha ya tofauti miongoni mwa wanachama.

Picha za matumaini.

Si rahisi kuwataja wanawake wote. Lakini hawa wote wamefanikiwa kuhakikisha kwamba sio tu kumekuwepo na taswira za machafuko kwa mwaka huu, bali pia za matumaini, kama ilivyo kwa mamilioni ya vidio zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha wanawake wakikata nywele zao kote ulimwenguni wakiwaunga mkono wanawake wa Iran. Na hata picha za watoto wachanga waliozaliwa katikati ya marindimo ya mabomu nchini Ukraine pia huwapa matumaini wazazi wao kwenye mazingira hayohayo ya vita.

Na bila ya mshikamano huu madhubuti wa mapambano, nia ya kuishi na kuwa huru, mwaka 2022 ungekuwa wa masikitio makubwa kwao. Wanawake wamepambana kuwapinga wavamizi, watesaji, madikteta na wanajeshi. Kwa mtizamo wangu, wamehakikisha kwamba kuna umuhimu wa kuwa na matumaini ya maisha ya mazuri badala ya kukatishwa tamaa na vita, machafuko na vifo.