Maoni: Mwanzo mpya kwa Cuba?
19 Aprili 2018Mama yangu alizaliwa chini ya utawala wa Castro, mimi nilizaliwa chini ya utawala wa Castro na mtoto wangu wa kiume alizaliwa chini ya utawala wa Castro. Kwa uchache, vizazi vitatu vya Wacuba wameishi chini ya utawala watu wawili wenye jina hilo.
Ukiritimba huu umemalizika leo (Aprili 19), ambapo Diaz-Canel Bermudez ametangazwa kuwa rais mpya.
Ama hatua hii iwe inapendelea muendelezo wa yale yale, au inaanzisha mageuzi, kuwa na mtu mpya kwenye uongozi wa juu wa taifa kunaashiria ukweli mmoja wa kihistoria: mwisho wa zama za Castro nchini Cuba.
Lakini pamoja na kuja kwa siku hii inayojitokeza kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka miaka 50 ya historia ya Cuba, matumaini kwenye mitaa ya Havana si makubwa, hata kama taifa linakabaliana na mabadiliko makubwa huko juu.
Sababu za kukosekana hamasa
Na kuna angalau sababu tatu za kukosekana kwa hamasa ya mabadiliko haya miongoni mwa wananchi wa kawaida. Kwanza ni hali mbaya ya kiuchumi, ambayo inawalazimisha watu wengi kupapia maisha ya siku hadi siku.
Kuna masihara kuhusu Cuba mpya, lakini yanakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile uwezo wa mtu kupata chakula chake cha mchana au kuhangaika kwenda kazini.
Sababu ya pili inayohusishwa na ukosefu huu wa hamasa, ni wananchi kutoshawishika kuwa mabadiliko ya kiongozi mmoja wa juu yanaweza kubadilisha chochote kwenye uhalisia, hasa kwa kuwa anayeingia hana tafauti yoyote na anayeondoka panapohusika mfumo wa utawala wa kikomunisti.
Na sababu ya tatu inayofahamika na watu wote ni ukweli kwamba hakuna anayeyajuwa mazingira ya kisiasa yasiyokuwa ya mfumo wa kikomunisti na hivyo hakuna cha kuulinganisha nao na hivyo pia, hakuna cha kurejelea kama ni mfumo mbadala kwa kizazi hiki cha kihistoria.
Hisia kwamba kila jambo litaendelea kama lilivyokuwa kabla ni matokeo ya miongo sita ya utawala wa akina Castro kwenye taifa hilo la kisiwa.
Kwa kuukandamiza kila upinzani na kumfyeka kila aliyeonesha dalili za kuwa mshindani wao, ndugu hawa wawili wamegeuka kuwa viumbe wasioweza kutenganishwa na historia ya miongo sita ya Cuba.
Baada ya yote, akina Castro wamekwisha
Lakini ukweli mmoja uko wazi pia. Zaidi ya asilimia 70 ya Wacuba walizaliwa baada ya Januari 1959, pale kundi la vijana wenye ndevu lilipowasili mjini Havana wakiwa na silaha mikononi na tabasamu usoni.
Muda mchache baadaye, vitabu vyote vya kiada, vyombo vyote vya habari, na propaganda za serikali zikawa zimewaremba wanamapinduzi hao kama waokovu walioiokoa nchi.
Kwa miongo kadhaa, walisambaza ushawishi kwamba Cuba ilikuwa na itikadi moja tu rasmi, chama kimoja cha kisiasa cha kikomunsti na kiongozi mmoja tu, Castro.
Sasa, baiolojia inahitimisha ukurasa huu wa historia ya Cuba. Unaweza mwaka sifuri kwenye historia ya Cuba, mwaka mpya kwa mwanzo mpya.
Lakini badala ya watu kushangiria mitaani wakipeperusha bendera, kilicho wazi mjini Havan ni mateso ya kimaisha tu.
Hii ndiyo hali ya watu ambao imani na hamasa yao imepondwapondwa kabisa kutokana na kusubiri kwa muda mrefu sana.
Mwandishi: Yoani Sanchez
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo