Maoni: Obama na Merkel - Ukumbatiaji wa kimkakati
26 Aprili 2016Ingawa Obama amejitolea kumfunza Merkel kucheza mchezo wa gofu, rais huyo wa Marekani anayejiandaa kuondoka madarakani anategemea kwamba kansela Merkel hatalikubali pendekezo hilo wakati wowote hivi karibuni.
Sababu iko wazi: miezi michache kabla kuondoka madarakani, Obama anaona mambo aliyoyafanikisha kisiasa na urithi wake kisiasa viko hatarini. Mwenendo wa dunia, ulioundwa na muungano kati ya Marekani na Ulaya baada ya kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia, unaonekana kuyumba zaidi kuliko ilivyoshuhudiwa awali baada ya mihula yake miwili ya urais.
Vita vipya baridi vinaibua wasiwasi kuhusu amani ya Ulaya na imeifanya Ukraine kuwa eneo ambalo Urusi inamenyana na mataifa ya magharibi kung'ang'ania madaraka. Wanamgambo wa kigaidi wa Mashariki ya Kati wanaonekana kulisukuma eneo hilo katika ukingo wa kujiangamiza lenyewe. Na katika kipindi ha miezi kadhaa, mzozo wa wakimbizi ulitoa changamoto kubwa kwa historia ya miongo kadhaa ya mfungamano wa Ulaya.
Obama anaandaa mazingira ya kukabidhi madaraka
Bila shaka Obama kumkaribia Merkel ni mkakati: Rais huyo wa Marekani atakapokabidhi madaraka kwa mrithi wake Januari mwakani, atamhitaji mtu atakayeyaendeleza maono namisimamo yake ya siasa za ulimwengu. Nchini Marekani watu wengi wana wasiwasi kama mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump anaweza kutegemea iwapo atashinda katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Mtizamo kwamba mvutano kati ya mataifa ya Ulaya kuhusu mzozo wa wakimbizi unaweza kumfagia na kumyumbisha kisiasa kansela Merkel anayeonekana kuwa nembo ya uthabiti, kunaweza kuwa jinamizi la siasa za dunia kwa Obama. Hii ndio sababu kwa nini Obama anatumia nguvu zake zote zilizobakia za kisiasa katika kuimarisha mahusiano yanayoendelea katika ngazi zote zinazostahiki kwa kutumia nyenzo zifaazo. Na kwa sababu hiyo, anakubali kwa makusudi makabiliano na wapinzani kadhaa wa sera za uhamiaji za kansela Merkel.
Uumoja wa Ulaya ukivurugika, hakutakuwa na ulimwengu huru
Miradi ya pamoja inatakiwa isaidie kuandaa mazingira ya mambo mapya, kama mijadala kuhusu mzozo wa wakimbizi ambao unalileta pamja bara la Ulaya. Kwa Obama mkataba wa kibiashara kati ya Marekani na Ulaya ni kitu kiachounganisha ambao anataka kuutumia kuleta msukumo mpya kwa mjadala kuhusu uhusiano kati ya Marekani na mataifa ya Ulaya - na yeye anataka kumuweka kansela Merkel awe mratibu wa mkataba huo mpya wa kibiashara kati ya pande hizo mbili. Merkel kama mdhamini wa umoja katika bara la Ulaya ana jukumu la ziada katika suala hilo. Obama anachukulia kwamba Merkel atahakikisha umoja barani Ulaya.
Rais Obama anahisi kumetokea ombwe la kisiasa barani Ulaya. Imani ya mradi wa pamoja wa kuwa na Ulaya yenye umoja imemomonyoka. Umoja huu ni wa umuhimu, sio tu kwa Ulaya, bali pia kwa maeneo mengine ya ulimwengu ulio huru, anaamini Obama.
Wasiwasi wake kuhusu taasisi kama bvile Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, ni wa msingi. Bila kuwa na muungano imara kati ya Ulaya na Marekani taasisi hizi zilizoundwa baada ya kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia, hazitaendelea kuwepo kwa muda mrefu katika siasa za dunia karne ya 21.
Kwa sababu kwa kansela Merkel ulimwengu ulio huru ni muhimu sana, binafsi amekuwa mtu ambaye rais Obama analazimika kushirikiana naye kwa karibu na hawezi kumuacha. Pia ni sehemu ya mkakati wake rais Obama kumkumbatia kansela huyo wa Ujerumani. Kwa hivyo msaada kwa Merkel utakuwa sehemu muhimu ya urithi wa kisiasa wa Obama.
Mwandishi:Fuchs, Richard
Tafsiri:Josephat Charo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman