1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Olaf Scholz mjini Kyiv — Kurejesha imani kiasi

17 Juni 2022

Ziara ya kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz mjini Kyiv ilikusudia kuipa Ukraine matumaini na iwasilishe kile kinatajwa kuwa‘'masuala thabiti''.

Ukraine | Olaf Scholz besucht Irpin
Picha: Ludovic Marin/AP/picture alliance

Japo wengi waliliona lengo hilo kushindikana, amesema Rosalie Romaniec, mwandishi wa DW akiongeza kuwa kila kitu kilifaulu kupita matarajio. 

Scholz mwenyewe ndiye alifanya ziara yake kuwa ya hadhi ya juu hivyo matarajio yakawa makubwa hivi kwamba baadhi walihofia huenda angefeli. Mwezi uliopita alisema "siendi Ukraine kama wengine wanaokwenda kwa muda mfupi kupiga picha na kurudi. Nikienda, ziara yangu itahusu masuala muhimu”.

Hakuelekea Kyiv peke nyake, bali aliandamana na viongozi wengine wa nchi za Magharibi akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Italia, Mario Draghi.

Japo ziara hiyo ilikuwa fupi na picha nyingi zilipigwa, kulikuwa na mengi zaidi ya hayo.Picha: Ludovic Marin/Pool/AP/picture alliance

Viongozi hao watatu huongoza mataifa matatu yenye nguvu zaidi kiuchumi na kisiasa barani Ulaya. Walipofika Kyiv, mji mkuu wa Ukraine, Rais wa Romania Klaus Lohannes aliungana nao, akiwakilisha mashariki mwa Ulaya.

Scholz alifahamu kitu cha kufanya

Kimsingi, ziara ya viongozi hao watatu wa magharibi mwa Ulaya, ilikusudia kutoa ishara ya mshikamano wa Ulaya na Ukraine. Ilikuwa muhimu kwamba walifaulu kutimiza hilo, huku macho yote hususan ya Waukraine yakimlenga Olaf Scholz.

Baada ya zaidi ya siku 100 za vita, kansela huyo wa Ujerumani alipanda treni ya usiku na kuwasili Kyiv.

Matarajio makubwa kutoka Ukraine ni silaha nzito nzito za kivita kutoka mataifa ya Magharibi na jibu la ‘ndiyo' kwa ombi lake la kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Rosalia Romaniec, DW BerlinPicha: Ronka Oberhammer/DW

Kuhusu ombi la silaha, jibu lilikuwa la kuridhisha kwa kiwango fulani. Kwani Scholz aliahidi kuwapa silaha zaidi, ila alisema itachukua muda kidogo ili ziwafikie. Aliongeza kuwa tayari, wapo wanajeshi wa Ukraine wanaopewa mafunzo Ujerumani.

Vile vile kansela Scholz hakuwakatisha tamaa Waukraine kuhusu ombi lao la pili. Bali aliiwahi nafasi hiyo kama kiongozi wa taifa lenye nguvu zaidi katika Umoja wa Ulaya na moja lenye jukumu la historia ya kipekee kuhusu Ukraine na kuweka mambo bayana: "Ukraine ni sehemu ya familia ya Ulaya.” Kwa sentensi hiyo Scholz alionekana kuchukua taji la uongozi ambalo kansela wa Ujerumani anapaswa kuchukua katika hali ya sasa. Asingeweza kuwa na msimamo tofauti.

Ipo siku watakuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya

Kwamba Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky aliuita uamuzi huo wa ‘kihistoria' ilikuwa njia ya busara kuonyesha mshikamano wa Ulaya, licha ya tofauti zote zinazoweza kutarajiwa kutokea katika mchakato wa kutaka kuwa mwanachama hadi kuwa mwanachama rasmi.

Kwa wiki kadhaa, imani ya Ukraine na mashariki mwa Ulaya katika kutegemewa kwa Ujerumani ilipata pigo kufuatia ukosefu wa msimamo thabiti wa Berlin. Lakini kufuatia ziara hiyo, Scholz alifaulu kuondoa dhana ya kuwa kiongozi anayesitasita na mwenye woga.

Ziara ya viongozi hao watatu wa magharibi mwa Ulaya, ilikusudia kutoa ishara ya mshikamano wa Ulaya na Ukraine.Picha: Natacha Pisarenko/AP/picture alliance

Kwa Zelensky, kulikuwa na mengi zaidi njiani kuelekea mwanachama wa Umoja wa Ulaya zaidi ya matamshi rasmi. Nchi yake iko vitani. Wenzake wanaonesha ujasiri na nia ya kupigana vita ambavyo Ulaya haijashuhudia tangu Vita Vikuu vya Pili Ulimwenguni. Na kila siku wanalazimika kuvumilia. Matarajio ya kuwa siku moja watakuwa sehemu ya Ulaya huwasaidia katika vita hivyo.

Kitu kingine ambacho kilikuwa muhimu kwa Ukraine ni kauli ya rais wa Ufaransa kwamba "ni sharti Ukraine ivishinde vita hivyo”. Huo haukuwa ujumbe wa wazi tu mwa Waukraine bali pia kwa Urusi. Maneno hayo yalitoa matumaini na ahueni kwa wengine pia walioko mashariki mwa Ulaya.

Kwa Olaf Scholz, ziara hiyo ilitoa nafasi pia ya kutuliza ukosoaji wa awali dhidi yake. Lakini ili kuhakikisha ukosoaji huo unadumu kwa zaidi ya wakati huu, itabidi sasa abaki kwenye mkondo huo.

Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Italia wawasili Kyiv

01:52

This browser does not support the video element.

Mwandishi: Rosalie Romaniec

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW