Maoni: Picha iliyotugusa sote
3 Septemba 2015Picha hii kwa vyovyote inaonesha taswira ya kuhuzunisha. Inatuonesha kitisho kinachowakabili watu wanaojaribu kuikimbia nchi iliyokwishasambaratishwa kwa vita, Syria. Picha hii ni kielelezo cha yale yanayotokea kila siku kwenye Bahari ya Mediterrenia.
Juu ya hayo, picha hii inaakisi pia ubaya wa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe. Ni taswira inayochafua nafsi. Ni picha inayomchoma mtu ndani kabisa ya hisia zake kwa mshindo. Inakusuta ikikwambia kuwa wewe huna maana. Inakufanya ufikirie mara mbili mbili, lakini bado ni picha inayotunyamazisha sote.
Hii ni picha ambayo sote tunaihisi - ni picha ya mwaka, na yumkini hata ya muongo mzima. Inasimamia kila kile ambacho kinatushitua, kinatugusa, kinatukasirisha na kutupandisha ghadhabu kwa miezi kadhaa sasa. Na ni picha ya kuhuzunisha.
Lakini swali kubwa kwenye tasnia yetu ya habari ni ikiwa kweli tunaweza au tunapaswa kuionesha? Kuna sababu zinazoshawishi kwamba tusifanye hivyo. Sababu za heshima kwa utu wa kitoto hiki na mahitaji yenye uhalali kutoka kwetu watu wa vyombo vya habari.
Tunaichapisha kwa uzito wake
Ila kwa makusudi kabisa, tumeamua kuionesha. Sio kwa kuzusha hamasa, sio kwa kusaka "clicks" nyingi zaidi kwenye kurasa zetu, sio kuwania dhamira yetu ya kuelekea kwenye matangazo ya televisheni. Hapana. Tunaionesha kwa kuwa inatugusa sote. Tunaionesha kwa kuwa ni alama ya balaa la mzozo wa sasa wa wakimbizi.
Masikini, wazazi wasio hatia wa kitoto walilazimika kukichukuwa kwenda nacho safari ya hatari kusaka mustakabali mwema, safari yao ikaishia kwenye mauti ya baharini, nacho kikasombwa ufukweni kuja kutusimulia sisi tulio hai hadithi yake.
Kwa hivyo, tunaionesha picha hii kwa sababu imetutikisha na kwa sababu kwenye mkutano wa jopo la wahariri tulijikuta tumesinzima na kuduwazwa. Tumeguswa na mateso na mauti. Tunaionesha kwa kuwa tumeumizwa sana na mateso haya, na kwamba licha ya pirika na harakati zote kwenye kazi zetu kama waandishi wa habari, tumejikuta tumepoozeshwa na picha hii.
Mwandishi: Alexander Kudascheff
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba