1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Putin ametangaza vita

23 Februari 2022

Mtawala wa Kremlim ameukana uhuru wa Ukraine na kutuma wanajeshi Donetsk na Luhansk na ikiwa Ulaya itamuachia afanye atakavyo kwenye hili, basi vita vyengine vikuu haviepukiki, anasema Frank Hofmann.

Ukraine-Konflikt | Lage in Ostukraine |  Frontlinie in Novoluhanske
Picha: GLEB GARANICH/REUTERS

Sasa kila jambo linatokea kwa haraka sana: majeshi ya Urusi yanazikalia sehemu za nchi ya pili kwa ukubwa barani Ulaya. Sio chini kwa chini kama walivyokuwa wakifanya kwa miaka minane sasa, ama kama kundi la watu wasiojulikana waitwano “kijani” huko Crimea. Hapana. Vladimir Putin anatuma vikosi rasmi kulikalia dola moja la Ulaya ambalo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa – Ukraine.

Huu ni uvunjaji mwengine wa sheria za kimataifa. Kama mwengine mwingi huko nyuma. Huu ni uvunjaji wa mkataba wa CSCE wa Budapest wa mwaka 1994, ambao uliifanya Ukraine kusalimisha silaha zake ya nyuklia. Nayo ikapatiwa hakikisho la Urusi, Uingereza na Marekani kulindiwa mipaka yake kama ilivyokuwa wakati huo na ilivyo sasa.

Ukweli kwamba uvamizi wa karibuni wa Urusi kwa Ukraine unavunja makubaliano haya, unapaswa kuwa indhari kwa mtazamo ulioenea kote, hasa Ujerumani, kwamba yeye, Putin, hamaanishi hivyo baada ya yote. Ndiyo, anamaanisha hivyo hivyo. Ni sadfa kwamba wapiganiaji haki za kiraia kutoka Jamhuri ya zamani ya Ujerumani Mashariki wanafahamu kile hasa inachomaanisha: kwamba hili ni tangazo la wa wazi la vita.

Makucha ya Putin kwa Ukraine

Juzi Jumatatu (21 Februari), Vladimir Putin, akivalia suti na tai yake nadhifu na mikono yote miwili kaweka juu ya meza, aliwatangazia watu wake na wa Ulaya nzima akiwa anaamisha hasa kwamba: "Ukraine sio tu ni taifa jirani, bali ni sehemu muhimu ya historia yetu na mafungamano ya kiroho."

Ati mafungamano ya kiroho? Kwa wasiofahamu, nukta hapa ni kwamba wale waitwao "Warusi wa Kiev", jina wajiitalo leo wazalendo wa Kirusi, wana mashiko yao kwenye ngano asilia kuwa chimbuko lao ni Lavra, pango la watawa mjini Kiev.

Kwenye hotuba yake hii iliyorushwa moja kwa moja kwenye televisheni, mtawala huyu wa Kremlin aliwacha barakowa yake ivuke. Hakuna chochote kilichosalia ambacho Vladimir Putin anaweza kuwavutia wabunge wa Ujerumani kutaraji ati kuna jambo jema na jipya litatokea kwa Urusi mpya. Jioni ile ya juzi, Vladimir Putin yule yule ndiye aliyekuwa amekaa kwenye Ikulu ya Kremlin kama daima alivyo:  mwana wa shirika lake, KGB.

Jasusi huyu huyu wa zamani anayetimiza hivi karibuni umri wa miaka 70, kuna wakati alikuwa na makaazi yake mjini Dresden, Ujerumani, ndiye leo hii anayekaa nyuma ya meza ya kahawia akiinuwa mikono hewani kuashiria kauli yake: "Kizazi cha wasio shukrani wamelibwaga sanamu la Lenin nchini Ukraine kisha wanaita huko ni kuondosha ukomunisti."

Mwisho wa ukomunisti, mwanzo wa Ulaya mpya

Ikumbukwe kuwa baada ya mapinduzi ya Maidan yaliyoungwa mkono na Ulaya mwaka 2014, wazalendo wa Ukraine na wanaharakati wa haki za kiraia walikuwa wakitumia neno “kuondosha ukomunisti” kuelezea njia yao ya kuelekea Ulaya – kujiunga na jamii ya Ulaya. Katika mji mkuu Kiev na miji mingine mingi nchini Ukraine, kile kile kilichofanywa Ujerumani Mashariki baada ya kuanguka Ukuta wa Berlin, ndicho kilichofanywa: masanamu ya Lenin yalivunjwa kama ishara ya kuhama kutoka ukomunisti. 

Hilo halikumfurahisha kigogo huyu wa Kremlin, mtu ambaye aliibadilisha Urusi ya Borris Yeltsin kuwa muundombinu wa kiuchumi ya tabaka la KGB uliojikita kwenye mafuta na gesi. Hili linafahamika kutokana na mtazamo rahisi wa kidunia alionao Putin, ambaye hana habari yoyote na ufahamu wa Ulaya wa jinsi siasa, utamaduni na muakisiko wa kijamii unavyopaswa kushughulikiwa.

Mapinduzi ya raia wa Ukraine

Baada ya kile kilichoitwa Mapinduzi ya Chungwa ya mwaka 2004, Ukraine iliandama njia iliyojaa vikwazo. Mwaka 2013, maandamano yalianza kwenye uwanja wa Maidan mjini Kiev kupinga hatua ya serikali iliyoungwa mkono na Urusi kuukataa Mkataba wa Makubaliano na Umoja wa Ulaya. Rais wao akawa kiongozi wa pili baada ya kuporomoka kwa Muungano wa Kisovieti kufurushwa madarakani na raia.

Raia hawa wawanweza kufanya hivyo tena maana wanajuwa kinachoweza kufanyika. 

Ulaya sasa ina nafasi ya kuchaguwa: ama kuuzuwia uhalifu wa Putin au kuwa sehemu ya vita vikuu ambavyo bado vinaweza kuepukika. Lakini kila suluhisho ambalo linamruhusu sasa Putin kuchukuwa ardhi nyengine kwa kuyakalia maeneo ya waasi ya Donetsk na Luhansk tayari lina mbegu za vita halisi dhidi ya Ukraine. Na ndio maana sio suluhisho.

Kama sehemu ya Umoja wa Ulaya, Ujerumani ya kidemokrasia inabeba dhamana kubwa: kwa sababu walikuwa ni wanajeshi wa Kijerumani, kwa niaba ya Hitler, ndio waliokuwa wa kwanza kuivamia Poland, kisha Ukraine na Belarus.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW