1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Putin hana budi kuchochea vita ili anusurike

21 Septemba 2022

Uhamasishaji wa kijeshi Urusi na kura za haraka za maoni katika maeneo yanayokaliwa mashariki mwa Ukraine ni ishara za udhaifu. Putin amekosea; gharama wanalipa maelfu ya Warusi kwa maisha yao, anasema Miodrag Soric.

Russland Teilmobilmachung Symbolbild
Picha: Mikhail Metzel/Kremlin Pool/Planet Pix/ ZUMAPRESS.com/picture alliance

Rais Putin hawezi kurudi tena nyuma: Na ikiwa atashindwa katika vita vyake vya uvamizi dhidi ya Ukraine, itamgharimu madaraka yake, na yumkini zaidi ya hayo. Hali iatkuwa hivyo kwa wawakilishi wa bunge la Duma, ambao hatma yao hivi imeunganishwa na ile ya mkuu huyo wa Kremlin.

Wote wako katika hali ya taharuki kufuatia mafanikio ya karibuni ya vikosi vya jeshi la Ukraine katika kurejsha maeneo ya nchi yao yaliokaliwa. Hali inaitishia Moscow kushindwa kijeshi, jambo ambalo hakuna alielitarajia mjini Moscow. Kutokana na hofu hiyo, Putin ameamuru kuwekwa tayari wanajeshi laki tatu wa akiba kwa ajili ya kwenda uwanja wa vita. Jukumu la wanajeshi hao litakuwa kuzuwia kasi ya vikosi vya Ukraine kusonga mbele zaidi.

Dhaifu, ametengwa

Siku  chache zilizopita kando mwa mkutano wa shirika la ushirikiano la Shanghai  nchini Uzbekistan, Putin alieonekana akipambana kijiweka sawa alisema Urusi haikuwa na haraka nchini Ukraine. Katika hali halisi lakini dunia iliona Putin aliedhoofika na alietengwa.

Soma pia: Warusi wakimbia baada ya tangazo la uhamasishaji wa kijeshi

Kamera za televisheni zilionesha mwanaume anaezeeka, ambaye wakuu wengine wa mataifa na serikali walikaa wakimsubiri. Putin alikaa kistadi kwenye kochi na kuwasikiliza. Uturuki, India na hata China ziliweka wazi kwamba zinapinga vita vya Putin, zinaunga mkono uhuru wa mipaka ya Ukraine. Na zilikuwa sababu za msingi: Vita hivyo ni mzigo kwa uchumi wa dunia na vivyo hivyo kwa mamlaka ya wanasiasa hao, ambao Putin alitumai kupata uungwaji wao mkono kwa ajili ya vita vyake.

Mabadiliko ya mwelekeo katika Kremlin

Kwa mtazamo wa Kremlin, mambo hayangeweza kuendela hivi. Hivyo mjini Moscow, Putin anaharakisha kubadili mwelekeo na hivyo ukusanyaji huo wa wanajeshi kwa sehemu ni kukiri juu ya udhaifu wa kijeshi mashariki mwa Ukraine.

Soma pia: Rais Putin atangaza uhamasishaji wa sehemu wa kijeshi Urusi

Kwa matangazo ya kuitisha kura ndani ya siku chache katika maeneo yaliotekwa kuhusu kujiunga na shirikisho la Urusi, ni wazi kwamba wa Ukraine hawataki kujiunga na Urusi. Kwa sababu kura inayofanyika mbele ya mtutu wa bunduki, kura ya maoni katika magofu, hakuna yeyote duniani anaweza kuichukulia kwa uzito.

Mwandishi wa SW Miodrag Soric.Picha: DW

Putin anataka kupata mali zilizoporwa. Maeneo yaliotekwa yatakuwa sehemu ya shirikisho la Urusi. Kisha Putin anaweza kutoa wito wa kutetea taifa kwa kutumia nguvu za kijeshi. Kile kinachoitwa operesheni maalumu ya kijeshi, ambayo ina mipaka ya muda na nafasi na ambayo haikuhusika kwa vyovyote na maisha ya kila siku ya Warusi walio wengi, inageuka kihistoria utetezi wa ardhi ya Urusi kwa njia zote, ikiwemo silaha za nyuklia.

Mwisho wa 'peresheni maalumu'

Mtu haitaji kuwa nabii mkuu kutabiri mwisho unaokaribia wa neno operesheni maalumu. Propaganda ya Kremlin italizika neno hilo. Badala yake, kutakuwa uongo zaidi na zaidi wa kipumbavu na kuchanganya, uzushi, vitisho ambavyo vituo vya televisheni vinavyodhibitiwa na serikali vitatumia kuwarubuni Warusi. Hata sasa inadaiwa kuwa Urusi haifanyi vita dhidi ya Ukraine, lakini inanjitetea nchini Ukraine dhidi ya Marekani na Uingereza. Hilo wanaliamini wanaotaka kuamini.

Soma pia:Scholz autaja uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuwa ubeberu

Uchochezi mpya wa Putin utachuliwa kwa uzito na viongozi wa dunia wanaokutana hivi sasa katika hadhira kuu ya Umoja wa Mataifa mjini new York. Lakini sera yao kuelekea Moscow haitabadilika pakubwa. Kiev itaendelea kupokea silaha, jeshi lake litadelea kupambana. Na wanajeshi 300,000 wa akiba wa Urusi? Hawajawahi kuwa vitani, hawana zana za kutosha. Ni watu wenye familia, wanaume wanaotenganishwa na maisha ya kila siku dhidi ya matakwa yao.

Nchini Ukraine, wanapaswa kuilinda Urusi - wakiwa sambamba na wahalifu na mamluki wa Chechnia. Hii haiwezi kuwenda vyema. Wataona kwa macho yao kwamba wa Ukraine hawataki kuwa sehemu ya Urusi. Makumi kwa maelfu ya watu watakufa ili Putin na watu wake waweze kusalia madarakani, ili wasiweze kuhalilisha uhalifu waoe dhidi ya watu wao. Hilo ndiyo janga halisi la uamuzi wa karibuni na usio sahahi wa kiongozi wa Kremlin.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW