Maoni: Rais mpya - lakini hakuna mshindi
8 Novemba 2020Sehemu kubwa ya dunia ilikuwa pumzi juu. Na saa inaweza kushusha pumzi taratibu - na kupumua tena.
Imechukuwa muda mrefu, na ilikuwa mpambano mkali, lakini Joe Biden ameibuka mshindi mbele ya Donald Trump. Baada ya muhula mmoja tu madarakani na miaka minne iliyokuwa mirefu sana, rais huyo aliyekuwa akitetea nafasi yake anapaswa kuihama Ikulu ya Marekani tarehe 20 Januari.
Siku hiyo hiyo, Biden na Kamala Harris wataapishwa kuwa rais na makamu wa rais. Japokuwa Trump ameshatangaza kwamba atayapinga matokeo hayo mahakamani, lakini haonekani kuwa ana nafasi ya kushinda huko pia.
Habari njema kwa ushirikiano wa kimataifa
Kuchaguliwa kwa Biden ni habari njema kwa dunia inayoamini kwenye mipango ya pamoja na inayotamani sana Marekani inayoaminika.
Kwa watu wanaoamini kwenye maana nzuri ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kwenye Makubaliano ya Tabianchi ya Paris. Kwa wafanyabiashara wanaohitaji kanuni zinazoaminika kwa kampuni zao.
Na pia kwa wale wote ambao, kama ilivyokuwa zamani, wanaamini kwamba mahusiano yanayovuuka Bahari ya Atlantiki ni muhimu kwa mshikamano na umadhubuti wa demokrasia ya Magharibi.
Hata hivyo, zile nyakati ambazo Marekani ilikuwa ikijibebesha pekee mzigo wa kuwa polisi wa dunia sasa zimekwisha. Alikuwa ni rais wa zamani, Barack Obama, aliyeweka wazi kabisa kwenye tamko lake "Kuongoza kutokea nyuma", kwamba kujihusisha kwa upana na kifedha kwenye masuala ya kijeshi kulikuwa kukitazamiwa na ulimwengu. Trump alijenga juu ya mageuzi haya ya mkakati - na Biden ataendelea nayo, japokuwa kwa njia ya kidiplomasia zaidi.
Kurejea kwenye Mkataba wa Paris
Biden, kama Obama aliyemtumikia akiwa makamu wake, ni muungaji mkono mkubwa wa mahusiano yanayovuuka Bahari ya Atlantiki. Anazithamini Ujerumani na Ulaya kama washirika wa kutegemewa. Aliahidi kuirejesha Marekani kwenye Makubaliano ya Paris ya mwaka 2015 na kuendelea kutimiza majukumu yake kwenye miungano mingine ya kimataifa kama vile NATO.
Chini ya Rais Biden, Marekani itakuwa tena mshirika wa kutegemewa.
Ikiwa Ulaya itaichukulia miaka ya indhari ya Trump kwa umakini, yumkini inaweza hata kuwa mshirika mwenye nguvu sawa. Hili linaweza kutokea pale upande wa Ulaya kwenye mashirikiano haya utakapobeba kiwango cha uwajibikaji ambacho kinaitendea haki dhima ya Ulaya ulimwenguni.
Mwenendo wa maharibiko
Ukiungalia kutokea ndani, unaweza kuutathmini uchaguzi wa mwaka 2020 kwa kiwango cha chini kabisa. Trump ameacha mkururo wa maharibiko. Uongozi wake uliokuwa umejikita kwenye uongo umeharibu imani kwenye mchakato wa kidemokrasia na taasisi na wafuasi wake wengi wataendelea kushikilia kwamba matokeo ya uchaguzi 'yalichakachuliwa'.
Wafuasi wa Trump watambebesha Biden dhamana ya kuporomoka kwa uchumi ambako Marekani utakushuhudia ndani ya miezi ijayo, ikiwa si miaka - hata kama Trump ni sehemu ya kuporomoka huko kutokana na jinsi alivyolishughulikia janga la COVID-19.
Ndani ya miaka minne ya kuwapo kwake madarakani, Trump ameibadilisha nchi. Democrat walikuwa wametarajia ushindi wa kishindo ambao ungeliashiria kuwa kwa wingi wao Wamarekani wanataka muelekeo mpya kabisa, lakini namna mchuano ulivyokwenda imeonesha kwamba hivyo sivyo hali ilivyo.
Kaulimbiu ya "Marekani kwanza haikumpatia Trump ushindi alioutarajiwa, lakini bado haijafifia hata kidogo. Trump amewaruhusu Wamarekani wengi kuelezea waziwazi ubaguzi wao wa rangi, chuki zao kwa wageni na dharau kwa watu wasiokuwa kama wao hadharani. Na wataendelea kufanya hivyo.
Kwa hivyo, hata kama Joe Biden ameshinda uchaguzi, lakini bado hajaweza kuishinda chuki iliyopandikizwa na Trump, na ambayo imeigawa vibaya Marekani.