1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Tanzania wadai bunge jipya halina uhalali

Deo Kaji Makomba
27 Januari 2026

Kuanza kwa vikao vya Bunge la 13 la Tanzania kumeibua mjadala mpana, huku vyama vya upinzani, wachambuzi na wananchi wakitoa maoni yanayokinzana kuhusu uhalali, nguvu na mustakabali wa bunge hilo.

Tanzania, Dodoma 2025 | Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wabunge bungeni
Bunge la sasa la Tanzania linaenelezwa kuwa na uwakilishi mdogo zaidi wa wapinzani tangu 1992, kufuati hatua ya chama cha CADEMA kususia uchaguzi mkuu uliyopita.Picha: Stringer/REUTERS

Wakati vikao vya Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vikianza Jumanne hii jijini Dodoma, kumeshuhudiwa maoni mseto kutoka kwa viongozi wa vyama vya siasa, wachambuzi wa masuala ya siasa na wananchi. Baadhi ya wadau hao wamelitaja bunge hilo kuwa la upande mmoja na kukosa uhalali wa kisiasa.

Makamu Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amesema chama chake hakilitambui Bunge la 13, akidai kuwa limeundwa bila ridhaa ya wananchi.

Akizungumza na DW, Heche alisema kuwa hakuna hata mbunge mmoja aliyepata uhalali wa kuchaguliwa na wananchi kwa kura huru.

"Sasa wewe unaendaje kutunga sheria za watu ambao hawajakuchagua? Hakuna ridhaa. Hakuna mtu hata mmoja kwenye hilo linaloitwa Bunge ambaye anaweza kusimama akasema amechaguliwa na wananchi. Kwa maoni yangu na chama chetu, hilo Bunge hatulitambui,” alisema Heche.

"Ni watu wamejiweka madarakani kwa nguvu. Ni kama waliofanya mapinduzi ya kijeshi halafu wanajidanganya kuwa wanajadili mambo ya kidemokrasia.”

Kauli hiyo imeongeza mjadala kuhusu uhalali wa bunge hilo, hasa ikizingatiwa kuwa CHADEMA haikushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi uliounda Bunge la 13.

Bunge la 13 linaongoza na Spika Mussa Azan Zungu, mbuge wa jimbo la Ilala kupitia chama tawala cha CCM.Picha: Parliament of the United Republic of Tanzania

Wachambuzi watoa mtazamo wa kati

Kwa upande wa wachambuzi wa siasa, kuna mtazamo unaotaka mjadala huo uangaliwe kwa mapana zaidi. Hamduni Malceli, mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania, anakiri kuwa hoja ya "bunge lisilo na meno” inaweza kujadiliwa, lakini suala la uhalali si rahisi kulikubaliana nalo.

"Inawezekana kabisa watu wakahisi bunge halina meno, hilo ni jambo la kujadili. Lakini kusema halitambuliwi ni suala gumu kidogo,” alisema Malceli.

"Vyama 19 vilishiriki uchaguzi, 18 kati yao vimetambua serikali. Kimoja pekee ndicho hakitambui.”

Kauli hiyo inaakisi mgawanyiko wa mitazamo juu ya nafasi ya upinzani na uzito wa hoja zake katika mazingira ya sasa ya kisiasa.

Upinzani bungeni: ‘Tutapaza sauti'

Hata hivyo, wabunge wachache wa upinzani waliopo bungeni wamesisitiza kuwa hawatakaa kimya. Mbunge wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, amesema kuwa licha ya idadi ndogo ya wabunge wa upinzani, bado watasimamia masilahi ya wananchi.

"Licha ya uchache wetu, tutajitahidi kadri ya uwezo kupaza sauti na kusimama imara kwenye masuala yanayogusa masilahi ya wananchi,” alisema Shaibu.

"Itakuwa jukumu la serikali na kiti cha Spika kuhakikisha hoja hazipimwi kwa chama, bali kwa uzito wa hoja yenyewe.”

Kauli hiyo inalenga kuwahakikishia wananchi kuwa bado kuna sauti mbadala ndani ya Bunge, licha ya uwiano mdogo wa nguvu.

Waziri Mkuu Mwigulu Lameck Nchemba ataongoza shughuli za serikali katika bunge la 13.Picha: Parliament of the United Republic of Tanzania

Kwa macho ya baadhi ya wananchi, Bunge la 13 linaonekana kukosa ushindani wa hoja. Baraka William, mkazi wa mkoa wa Mwanza, amesema bunge la sasa halifanani na mabunge ya awali.

"Kwa upande wangu mimi naona kama Bunge la sasa halijakaa vizuri kama mabunge mengine. Zamani tulikuwa tunasikiliza hoja za huku na huku,” alisema Baraka.

Maoni hayo yanaakisi hisia za sehemu ya wananchi wanaoamini kuwa demokrasia ya bunge inahitaji upinzani wenye nguvu zaidi.

Kwa mujibu wa takwimu, wabunge wa upinzani katika Bunge la 13 ni 11 pekee — tisa waliochaguliwa majimboni na wawili wa viti maalumu. Hii ni idadi ndogo zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mwaka 1992.

Je, Bunge la 13 litakuwa na uwakilishi sawia wa Watanzania?

17:44

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW