Maoni: Trump ni njia ya Putin kuelekea White House?
13 Desemba 2016Siku hizi wakaazi wa mji mkuu wa Marekani, Washington, wana utani. Huwa wanaulizana: “Hivi ni nani hasa aliyeshinda uchaguzi? Trump au Clinton?” Na jibu lake huwa: “Hapana, ni Putin!”
Ni aina ya utani ambayo kicheko chake huwa kinakusakama kooni, kwa sababu tangu ripoti za kwanza kujitokeza kwenye jarida la Washington Post mwishoni mwa wiki, maafisa zaidi wa serikali wanasema sio tu kwamba Urusi ilidukua mfumo wa kompyuta wa chama cha Democratic – jambo ambalo lilikuwa limeshukiwa kwa miezi kadhaa – bali pia mfumo wa mawasiliano wa Republican nao uliingiliwa pia.
Matokeo yake, watu wa intelijensia nchini Marekani sasa wanadai kuwa sio tu kwamba Urusi ilitaka kumchafua Clinton na demokrasia ya Marekani, bali kwamba mashambulizi yake yalifanyika ili weze kuingilia moja kwa moja kumsaidia Trump ashinde.
Kwa miaka mingi sasa, wataalamu wamekuwa wakionya kwamba vita vya siku zijazo vitashindwa sio ardhini, baharini au angani, bali mtandaoni. Hadi sasa, filamu za kutisha zimekuwa zikijikita zaidi na matukio ambapo wadukuzi wanaweza kuvizima vinu vya nyuklia.
Lakini wiki hii imekuja kuonekana kuwa ni wazi kuwa mapambano haya ni zaidi ya kuathiri mfumo wa kusambaza nishati au kubuni miongozo ya ulinzi wa data.
Mashambulizi dhidi ya demokrasia
Ikiwa tunataka kuthibitisha ukweli wa shutuma hizi, mashambulizi haya yanaelekezwa kwenye ule msingi hasa wa demokrasia: yaani uchaguzi huru kwa kura ya siri. Hasira nchini Marekani ni kubwa, lakini jibu la raia ajaye, Donald Trump inakasirisha.
Badala ya kuitisha haraka tume huru ya uchunguzi, amekuwa akijaribu kuzipuuzia shutuma hizi kwa ujumbe wa Twitter wa kuudhi. Hoja yake: “Kwa nini niyaamini mashirika ya usalama leo wakati hayakuwa sahihi pale yalipodai kuwa Saddam Hussein alikuwa na silaha za kemikali?”
Mashambulizi haya ya hadharani dhidi ya vyombo vya kiintelijensia ni makubwa sana kwani rais huyu mteule anarejelea kukataa kuhudhuria kwenye vikao vya kila siku vya taarifa za kiusalama. Sababu yake: Anajua sana kinachoendelea na hana haja ya kupewa taarifa hizo hizo kila siku.
Hii ni tabia ya ama mtu asiyeelewa mambo au ishara ya akili ya mfanyabiashara, lakini vyovyote iwavyo, ni hatari. Inawezekana ikawa ni kweli kuwa Trump mfanyabiashara amekuwa akifanya kazi na Urusi kwa miaka mingi sana na ndio sababu hataki mtu yeyote aviangalie vitabu vyake.
Ndiyo inayoweza kuwa tafsiri ya yeye kumteua mwenyekiti wa ExxonMobil, Rex Tillerson, kuwa waziri wake wa mambo ya nje, kwa kuwa ana mafungamano makubwa na Rais Vladimir Putin wa Urusi kutokana na mikataba ya biashara ya gesi.
Lakini yote hayo hayana thamani mbele ya ofisi kubwa kabisa ya kisiasa duniani, na kwa hakika ni hatari sana.
Mwandishi: Ines Pohl
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Grace Patricia Kabogo