1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Uamuzi wa Kabila ni matumaini Congo

Andrea Schmidt
8 Agosti 2018

Kukubali kung'atuka madarakani kwa rais Joseph Kabila ni ishara nzuri, anasema mkuu wa idhaa ya Kiswahili ya DW Andrea Schmidt katika maoni yake, lakini bado ni mapema kufurahia uchaguzi huru na wa haki nchini DRC.

DR Kongo Kampagne für Präsident Joseph Kabila
Picha: DW/K. Tiassou

Hatimaye taharuki imefikia tamati. Mpaka saa za mwisho, wasiwasi ulikuwa umetanda juu ya iwapo rais Joseph Kabila angewania tena au la. Kulingana katiba ya Congo Kabila hakupaswa kuwania muhula mwingine, lakini hilo halingemzuia kuahirisha uchaguzi huo ambao umekuwa ukibadilishwa kalenda tangu mwaka 2016.

Shinikizo kubwa kutoka jamuiya ya kimataifa na hata mashirika ya kiraia nchini mwake kama vile Lucha na makundi ya kanisa yaliopinga muhula wa tatu kwa Kabila lilikuwa kubwa na hivi sasa athari za shinikizo hilo zimeweza kuonekana. Hiyo ni ishara chanya hata kwa mataifa jirani. Ishara ya matumaini, kwamba inawezekana kuzuwia utawala wa maisha wa madikteta kwa njia za amani.

Muungano wa Kabila wa vyama tawala wa Common Front for Congo (CFC), utawakilishwa na waziri wa zamani wa mambo ya ndani na mshirika wa karibu wa Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary. Bado ni mapema kujua iwapo mgombea huyo anayo ajenda yake mwenyewe ya mageuzi kwa ajili ya taifa hilo zima pamoja na mikoa yake 26 ambalo ukubwa wake unazidi kanda nzima ya Ulaya ya Kati.

Mkuu wa idhaa ya Kiswahili ya DW Andrea Schmidt.Picha: DW/L. Richardson

Kikaragosi cha Kabila

Tayari fununu zimeanza kuzagaa kwamba Shadary ni kikaragosi wa Kabila atakaendeleza tu sera zake. Taasisi zote za kiserikali zipo kwa ajili yake na huenda hilo likawa jambo litakalomsaidia kutumia rasilimali za serikali wakati wa kampeni za uchaguzi kwa manufaa yake.

Ikiwa uchaguzi utafanyika Desemba 23, 2018 kama ilivyopangwa, kinyang'anyiro kinatarajiwa kuwa cha kukata na shoka kati ya Shadary na mbabe wa zamani wa kivita, anaetarajiwa kupeperusha bendera ya chama cha upinzani cha MLC Jean-Pierre Bemba. Yeyote atakaeshinda kati yao, atakabiliwa na changamoto kubwa.

Karibu miaka 60 tangu ilipojipatia uhuru wake Juni 30, 1960 Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imekuwa ikijikokota, huku ikikabiliwa na hali tete ya kiusalama, wakimbizi zaidi ya milioni 4.5, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, rushwa iliokithiri, upendeleo, viwango vya juu vya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na umaskini uliopindukia miongoni mwa jamii kubwa ya raia wa nchi hiyo. Karibu taasisi zote za serikali hazifanyi kazi huku makundi kadhaa ya waasi waliojihami kwa silaha nzito yakiendelea kutikisa taifa hilo.

Ukosefu wa imani katika siasa miongoni mwa jamii kubwa ya vijana nchini humo ni mkubwa mno. Hawajui kinachoitwa uchaguzi huru na wa haki mpaka sasa. Lingekuwa jambo jema kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo pamoja na watu wake kuona mabadiliko chanya na kwa rais ajaye kufanya kazi kwa manufaa ya raia na mustakabali bora wa taifa la Congo.

Mwandishi: Andrea Schmidt

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW