1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nafasi ya Martha Karua katika uchaguzi wa Kenya

5 Agosti 2022

Martha Karua, mgombea mwenza wa Raila Odinga kupitia tiketi ya muungano wa Azimio la Umoja anatajwa kuwa kiungo muhimu katika kuamua hatma ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 anasema Babu Abdalla katika uhariri wake.

Kenia | Raila Odinga und in Nairobi
Martha Karua aliyesimama kati kwenye picha, aliteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga mnamo Mei 16, 2022.Picha: Raila Odinga press Team

Martha Karua ana sifa tatu muhimu ambazo zinachukuliwa kama silaha katika uwanja wa mapambano kuelekea uchaguzi huo, nazo ni jamii anakotokea, jinsia yake, na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi. 

Wakati kampeni za siasa zikiingia kipindi cha lala salama, imetabiriwa kuwa kinyang'anyiro cha urais mwaka huu kitakuwa na ushindani kati ya farasi wawili- Raila Odinga na William Ruto. Ndio, nakubali kuwa uchaguzi huu utakuwa na ushindani kweli kweli.

Hata hivyo, uamuzi wa Raila kumteua Martha Karua kuwa makamu wake kunamuweka katika nafasi nzuri ya kuchaguliwa kuwa rais wa tano wa taifa hilo la Afrika Mashariki. 

Upigaji kura kwa misingi ya ukabila

Wafuasi wa muungano wa Azimio la Umoja mjini NakuruPicha: James Wakibia/Zuma/picture alliance

Inauma, japo ndio ukweli wa mambo kwamba Wakenya wengi hupiga kura kwa kuzingatia misingi ya kikabila. Sio sadfa kwamba Raila na Ruto waliteua wagombea wenza wao kutoka kabila la Wakikuyu, bali ni mbinu ya kisiasa. Kabila la Kikuyu ndilo kubwa zaidi nchini Kenya. Raila na Ruto hawangethubutu kuteua wagombea wenza kutoka kabila lengine, la sivyo uwezekano wa kuangukia pua ni mkubwa.   

Karata ya Raila kumchagua Martha, ambaye ni Mkikuyu, aliicheza katika wakati mwafaka anapohitaji uungwaji mkono wa kisiasa kutoka jamii ya Wakikuyu na kwa upana makabila kutoka eneo la Mlima Kenya. Eneo hilo lina utajiri mkubwa wa wapiga kura.

Eneo la Mlima Kenya linalojumuisha pia kaunti za Nakuru na Laikipia kutoka bonde la Ufa, anakotokea Naibu rais William Ruto, lina zaidi ya wapiga kura milioni tano waliosajiliwa. Kulingana na takwimu za tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC, watu wa kanda hiyo walimpigia kura kwa zaidi ya asilimia 80 Rais Uhuru Kenyatta wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Eneo la Mlima Kenya limechukuliwa kwa muda mrefu kuwa ngome ya Ruto, lakini tangu uteuzi wa Martha Karua ambaye pia anatokea eneo hilo, ghafla upepo umeanza kubadilika. Kuna upepo wa matumaini unaovuma kuelekea upande wa Raila Odinga na Martha Karua. 

Babu Abdalla ni mhariri na msomaji habari katika Idhaa ya DW Kiswahili.Picha: Babu Zingo/DW

Uungwaji mkono huu sio miujiza, bali ni athari ya moja kwa moja ya bi. Karua. Wakikuyu na jamii nyengine za Mlima Kenya zimemkumbatia Martha kama binti yao na wameonyesha utayari wa kumpeleka mwana wao pamoja na Raila ndani ya Ikulu. 

Niwe mkweli, Raila ambaye ngome yake kuu ya kisiasa ni eneo la Nyanza na sehemu kadhaa za Magharibi mwa Kenya, sio kipenzi cha wapiga kura wengi wa eneo la Mlima na hilo linathibitishwa kwa idadi ndogo ya kura alizokuwa akipata miaka ya nyuma. 

Lakini, Martha Karua anaonekana kuwa jibu la fumbo analohitaji kupata uungwaji mkono wa jamii ya Wakikuyu. Bi Martha, tangu uteuzi wake, amevuruga kwa kiasi kikubwa mafanikio yote aliyoyapata Ruto katika eneo la Mlima Kenya. 

Kimsingi, Ruto alianza kufanya kampeni katika eneo hilo takriban miaka minne, lakini ujio wa Martha chini ya miezi mitatu tu, kumebadilisha kabisa mitazamo ya kisiasa ya wengi kuhusu Raila Odinga. 

Wafuasi wa dhati wa Raila, wanakiri kuwa ilikuwa vigumu hata kwenye ndoto, kwa mwanasiasa huyo kuupanda mlima, ila sasa hali imebadilika. Raila anaukwea mlima tena kwa mwendo wa madaha kabisa, kwa sababu ameshikwa mkono na binti kutoka Mlima Kenya.

Hata baadhi ya Wakikuyu, hata kwenye mikutano ya hadhara, wanakiri waziwazi kuwa kwa mara ya kwanza katika maisha yao, wanaweza kumpigia kura Raila Odinga. 

Suala la jinsia kama silaha ya kisiasa

Makundi mbalimbali ya wanawake yapokea kwa matumaini uteuzi wa Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa Raila OdingaPicha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Ama kwa upande wa karata ya jinsia, hapa napo Raila amepatia. Suala la jinsia ni mojawapo ya silaha maalum za kisiasa. Kuteuliwa kwa Martha Karua kumewagusa nyoyo za akina mama, wanawake na mabinti wengi nchini Kenya. Wanahisi uhusiano wa moja kwa moja, sikwambii kuhusu umuhimu wa mama katika jamii, sote tunafahamu! 

Iwapo Raila Odinga atachaguliwa kuwa rais, Martha Karua atakuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa wa juu kabisa wa kisiasa nchini humo. Uteuzi wake pekee, unawakilisha matumaini ya Kenya iliyo bora, usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake. Wanawake, hasa wenye malengo ya kujitosa kwenye siasa, wana kila sababu ya kuwa na matumaini.

Naamini kwa dhati kabisa kwamba wanawake watachukua fursa hii kwa mikono miwili ya kumpigia kura mmoja wao. Kuna upepo unaovuma kwa kasi duniani wa wanawake kushikilia nyadhifa za uongozi: Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, rais wa Benki Kuu ya Ulaya Christine Lagarde na orodha ni ndefu. Upepo huu wa kisulisuli pia umewapiga Wakenya.

Martha Karua anawakilisha fursa adimu ya kuvunja dhana kuwa wanawake hawawezi, na kazi yao kubwa ni kukaa majumbani. Madamu mmoja wao anakaribia Ikulu, nahisi itawapa msukumo mamia kwa maelfu ya wanawake kustahamili foleni ndefu wakati wa kura na kumpigia kura mwenzao.

Tuitizame shilingi upande wa pili, William Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua nao sio kidogo pia. Wameendesha kampeni imara katika azma yao ya kuchukua usukani wa kuliongoza taifa.

Ajenda yao ya "hustler” yaani mpambanaji, imekuwa na mvuto mkubwa hasa miongoni mwa vijana ambao wanajumuisha idadi kubwa ya wapiga kura wapya katika uchaguzi wa mwaka huu. Ruto amejipambanua kama mwanasiasa anayetetea watu wa kipato cha chini.

Je, kipusa wa bahati atasimama na "wapambanaji” katika uchaguzi wa Agosti 9?  Letu ni jicho! 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW