Maoni: Ujerumani itakuwa na kipupwe cha kutisha mwaka huu?
1 Agosti 2022Je, ni kweli kuna kitisho cha kuwa na kipupwe cha kuangamiza nchini Ujerumani kama moja ya magazeti makubwa ya UjerumanI linavyoandika? Kwamba watu watalazimika kuganda kwa barafu kwa kuwa hawataweza tena kulipia ankara zao za gesi? Je, kutakuwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi kutokana na ongezeko la kutisha la bei za bidhaa muhimu?
Kwa ufupi, unaposoma, kusikiliza ama kuangalia taarifa za habari, kuna hali fulani ya mgogoro. Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine unaibuwa, kwa uwazi kabisa, kile ambacho kimekuwa kikifanywa sivyo ama kupuuzwa hapo awali. Kama vile mwanzo wa janga la korona ulivyoonesha kufeli kwa mifumo ya afya na elimu, ndivyo hali ilivyo sasa.
Hata hivyo, itakuwa makosa kukata tamaa ama kuangukia kwenye nadharia kwamba "kila kitu ni upuuzi tu". Lau alama za nyakati zinatambuliwa mapema na hatua kuchukuliwa, mzozo huu nao unaweza ukawa fursa. Kwa kuwa, sasa ni wazi kwetu sote: gesi asili ni bidhaa ya thamani na inayomalizika ambayo lazima itumiwe kwa tahadhari.
Hili linahusu pia mafuta yote ya kisukuku. Na tayari umeshashuhudia nakisi hii kwenye mfuko wako mwenyewe na utaendelea kuishuhudia - angalia bei ya petoli, mathalan.
Tuliacha lengo la nishati jadidifu
Na kwa hakika, tunajuwa pia kwamba tulishajitenga mbali na lengo la kuelekea kwenye nishati jadidifu - hatua ambayo ni muhimu kwa mabadiliko ya tabianchi. Serikali iliyopita chini ya Kansela Angela Merkel ilikuwa ikirejelea mara kwa mara propaganda ya kipindi hiki cha mpito kutoka nishati za visukuku kuelekea jadidifu.
Lakini, ni machache sana yaliyojiri - machache sana kabisa.
Baada ya yote, unahitajia nini kuwa na kinu cha umeme wa upepo mbele ya dirisha lako ikiwa gesi kutoka Urusi inatiririka kwa uhakika? Na hivyo, kidogo kidogo Ujerumani imekuwa ikizidisha utegemezi wake kwa gesi ya Urusi ndani ya miongo michache iliyopita.
Inafahamika zamani kwamba Urusi imekuwa ikitumia gesi kama silaha wakati wa mizozo na majirani zake na kufunga mifereji wakati wa kipupwe.
Hakuna wa kuachiwa kufa kwa baridi
Fursa inayozuka kwenye mzozo huu wa sasa ni kutanuwa nishati jadidifu haraka iwezekanavyo na hata kabla ya mwaka 2045, muda ambao serikali ilikuwa imetangaza kuwa taifa linalotumia nishati rafiki pekee kwa mazingira.
Hii ni kwa kuwa, hata madikteta wanapokwenda vitani, jua na upepo na maji huwa pia yapo.
Mradi huu unahitaji juhudi za kijamii, lakini kuiokowa sayari ya dunia kamwe halijawahi kuwa jambo jepesi. Na ndio kwanza tumejifunza jinsi hili lilivyo la lazima: Kipupwe kijacho hapana shaka kitakuwa kigumu zaidi kuliko kilichopita, lakini kuchanganyikiwa si jambo sahihi. Lililo sahihi ni kukabiliana na jukumu hili kwa pamoja.
Kauli ya Kansela Olaf Scholz kwamba: "Hamutatembea peke yenu" lazima ifuatiliwe na vitendo, ikiwemo hatua ya kutoa ruzuku ya gesi ya kupashia joto majumba kwa watu wenye kipato cha chini na pia kanuni dhidi ya kutumia vibaya nishati.