1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ujerumani sio timu ya juu tena

DW Kiswahili | Iddi Ssessanga
Iddi Ssessanga
2 Desemba 2022

Ujerumani imetoka kwenye Kombe la Dunia la 2022 katika hatua sawa na Urusi miaka minne iliyopita. Uchunguzi kuhusu soka la Ujerumani utafuata, lakini ukweli ni kwamba Ujerumani siyo nzuri tena, anasema Jonathan Harding.

Licha ya kuifunga Costa Rica mabao 4-2 Alhamisi usiku, hasara ilikuwa tayari imetokea. Safari hii kuondoka kwao kulikuwa kwa uchungu hata zaidi kwa sababu waliacha hatma yao mikononi mwa wengine na wamelipa gharama baada ya  Uhispania kushindwa na Japan.

Baada ya kutolewa katika hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Dunia iliyofuatana na kutoka katika hatua ya 16 bora kwenye michuano ya kombe la mataifa ya Ulaya majira ya joto yaliyopita, Ujerumani imethibitisha jambo moja: hii si timu ya mashindano tena.

Soma pia: Ujerumani yabanduliwa katika hatua ya makundi

Licha ya juhudi bora za Niclas Füllkrug, Ujerumani haina nambari tisa. Kwa ulinzi, ni Antonio Rüdiger pekee ambaye ameonekana mrithi mzuri wa kutosha katika kizazi kinachofuatia Mats Hummels na wenzake. Vurugu zilizoshuhudiwa katika eneo la beki wa kulia tangu Joshua Kimmich ahamie kwenye safu ya kiungo zimekuwa janga na ukosefu wa ubora wa kweli katika nafasi ya beki wa pembeni hatimaye umeigharimu Ujerumani.

Mwandishi wa michezo wa DW Jonathan HardingPicha: DW/P.Henriksen

Masuala ya kimuundo

Haya yote ni masuala, kwa sehemu, yanayohusiana na soka la vijana nchini Ujerumani. Ukiwa umefanyiwa mageuzi kwa kuanzishwa vyuo vya soka mwanzoni mwa miaka ya 2000, mfumo wa Ujerumani ulizalisha kizazi cha wachezaji wenye vipaji vya kiufundi na werevu.

Soma pia: Ujerumani haitasusia Kombe la Dunia la 2022 huko Qatar

Hilo lilipelekea, kwa kiasi fulani, ushindi wa 2014 lakini tangu wakati huo Ujerumani imekuwa ikijikokota kwenda na wakati huku ulimwengu mzima ukishika kasi. Mageuzi sasa yamefanyika, lakini yatachukua sehemu kubwa zaidi ya muongo mmoja kabla ya kuzaa matunda.

Ukufunzi pia limekuwa suala. Ujerumani ilikuwa timu ya kuburudisha chini ya Joachim Löw, ambaye polepole akawa kocha ambaye mara chache sana alipata uwiano sawa na mwishowe alikaa kwa muda mrefu sana, akiivusha Ujerumani katika michuano miwili iliyopita lakini siyo kuipeleka katika enzi mpya.

Ujio wa Hansi Flick, kocha ambaye aliigeuza Bayern Munich kuwa mashine ya hatari na ya ushindi katika muda mfupi aliokaa klabuni hapo, ulileta matumaini makubwa. Badala yake, kandanda ya Flick iliyumba-yumba nchini Qatar kwa Ujerumani kushindwa kuonesha makali yanayohitajika. Matatizo yamebaki na ufumbuzi wa kweli umekosekana. Flick lazima abebe lawama hapa kwa baadhi ya chaguzi zenye shaka na amekumbushwa kwamba Ujerumani si Bayern Munich.

Picha: Federico Gambarini/dpa/picture alliance

Ubora unakosekana

Haya yote yanapelekea kwenye hitimisho la wazi lakini la kushangaza kwamba katika muktadha wa mchezo wa sasa wa kimataifa, Ujerumani sio sehemu ya timu za juu. Wao ni timu nyingine tu. Takwimu zinathibitisha hilo: Ujerumani ina ushindi mara tatu pekee katika mechi 10 za mwisho za mashindano.

Timu inalijua hilo pia, kama ilivyodhihirishwa na maoni ya Ilkay Gündogan na Manuel Neuer baada ya kushindwa na Japan. Mchezo dhidi ya Uhispania pia ulionekana kuwa mkali kwa timu na kocha wao mkuu. Ni wazi kwamba Ujerumani siyo timu bora tena.

Yumkini Flick atasalia, huku michuano ya nyumbani ya kombe la Ulaya katika miaka miwili ikiwa nafasi ya mwisho na pengine pekee ya ukombozi. Meneja wa timu Oliver Bierhoff, kwa upande mwingine, anaweza pia kujikuta matatani.

Uti unaozeeka wa mgongo wa timu yake umefikia kikomo chake. Thomas Müller alitangaza kustafu mara tu baada ya mchezo wa Costa Rica. Haitashangaza kuona Ilkay Gündogan, Mario Götze na pengine hata Manuel Neuer wakifanya vivyo hivyo, bila kujali mashindano ya nyumbani yanayokuja katika miaka miwili. Magurudumu ya mapinduzi ya haraka na makubwa yanasonga.

Vyovyote iwavyo, ukweli ambao umekuwa ukiendelea kuvuma kwa muda mrefu sasa umedhihirika wazi na hauwezi kukanushwa: Ujerumani si timu ya juu tena.

Mwandishi: Jonathan Harding

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW