1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ujerumani yakabiliwa na nyakati ngumu

3 Juni 2019

Kujiuzulu kwa mwenyekiti wa SPD Andrea Nahles kunaongeza uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi wa mapema nchini Ujerumani. Lakini vyama vya CDU na SPD vinapaswa kuepusha maamuzi ya haraka, anasema mhariri mkuu Ines Pohl.

Wolken über dem Reichstag in Berlin
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Matokeo ya uchaguzi wa bunge la Ulaya wiki moja iliyopita yalisababisha zilzala ya kisiasa nchini Ujerumani, ambayo madhara yake yanasikika hivi sasa. Tangazo la Jumapili la mwenyekiti wa SPD Andrea Nahles kujiuzulu nafasi zake chamani na bungeni ni zaidi ya tatizo la ndani ya chama cha SPD. Ni ishara ya mgogoro uliokikumba chama cha SPD na kile cha CDU cha kansela Angela Merkel - vyama viwili vikuu ambavyo kati yake vimetoa kila kansela aliewahi kuchaguliwa tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya shirikisho.

Hakuna kati ya vyama hivyo chenye utulivu unaohitajika kwa sasa kuchukua jukumu halisi la uongozi. Hili ni sahihi hasa kwa kuzingatia sera na watendaji wa vyama hivyo

Mwenyekiti wa SPD Andrea Nahles na Kansela Angela Merkel.Picha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

CDU: Kimezeeka, na kuchoka

Kwanza, chama cha CDU: Tangu Merkel alipokaa pembeni kama kiongozi wa chama baada ya CDU kupata matokeo mabaya katika uchaguzi wa majimbo, malumbano ya ndani ya kisiasa yamefikia kiwango cha kutodhibitika. Annegret Kramp-Karrenbauer, mwenyekiti mpya wa chama na mwenye uwezekano wa kumrithi Merkel kama kansela, hana mvuto. Kujielekeza kwake kwa wanachama wenye msimamo mkali wa kulia chamani wakati wa kampeni za uchaguzi wa bunge la Ulaya hakukinufaisha chama - na badala yake ilikuwa kinyume kabisaa.

Na janga la uhusiano wa umma alilosababisha kwa kumshambulia mtumiaji wa Youtube aliekosoa chama chake kwenye vidio lilionekana zito. Hapa pia, jaribio lake la kuonyesha ukali kwa kutaka udhibiti mkali wa intaneti lilimgeukia kabisaa. Hakuharibu tu sifa yake lakini pia ya chama, na kukifanya kionekane cha zamani, kilichochoka kisichofaa kwa wakati ujao.

SPD: Yatafuta nafasi yake

Kwa wa Social Democrat, hali ni ngumu hata zaidi. Kwa muda wa miaka sita sasa, chama kimekuwa mshirika mdogo katika serikali ya muungano mkuu na kimeshindwa kukabiliana na mbinu za kansela Merkel kwa kutumia za kwake chenyewe. Iwe kuhusu kima cha chini cha mshahara au huduma za watoto: Merkel amefanikiwa mara zote kuchukua sifa kwa karibu kila mageuzi yalioanzishwa na SPD.

Mhariri Mkuu wa DW Ines Pohl.Picha: DW/P. Böll

Badala ya kuja na sera zake na kutatua tatizo muhimu la kujitafutia nafasi yake katika uwanja wa siasa za Ujerumani, SPD imejiingiza katika malumbano ya ndani na mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi. Na sasa kiongozi wa sasa wa SPD anajiuzulu kutoka nafasi zake zote. Hii inamaanisha jambo lolote linawezekana. SPD imefikia kiwango cha chini kabisaa kiasi kwamba hivi sasa wanatoa wito wa kukomeshwa kwa zimwi linalojulikana kama "muungano mkuu," kwa gharama yoyote.

Hakuna maamuzi ya haraka

Lakini hilo ni hatari. Vipi kama uchaguzi wa mapema wa bunge unafanyika mwaka huu? Siyo SPD wala Wahafidhina wanazo takwimu za kutosha kuwaweka juu. Hakuna chama chochote kilicho na utashi wa kushughulikia wasiwasi wa raia wa Ujerumani. Suala la ulinzi wa mazingira ni mojawapo tu ya wasiwasi huo, hata kama kwa sasa ndiyo lenye sauti kubwa zaidi.

Mwenyekiti wa CDU Annegret Kramp-Karrenbauer.Picha: Reuters/H. Hanschke

Kwa wakati huu, Ujerumani iko kwenye msingi imara wa demokrasia. Hata kama uchaguzi mpya utaitishwa, hakuna hatari ya wafuasi wa siasa kali za kizalendo kushinda wingi wa kutawala. Hiyo ndiyo habari nzuri katika nyakati hizi za machafuko.

Jukumu la Ujerumani ulimwenguni

Katika muktadha wa mchango inaopaswa kutoa Ujerumani ulimwenguni hata hivyo, malumbano ya ndani ya vyama hayapaswi kuruhusiwa kuamua nini kinatokea katika siku zijazo. SPD na CDU wangeshauriwa kuchukuwa muda, katathmini athari sahihi na kutafakari hatua wanazozichukuwa.

Kwa sasa, Ujerumani inaweza kuendelea kuwa tulivu kisiasa na kusalia mshirika anaetegemewa kwa washirika wa kimataifa iwapo tu wale waliopo madarakani watafikiria kuhusu athari za baadae za kisiasa - na siyo tu kubakiza mamlaka ya kisiasa katika wakati wa sasa.

Mwnadishi: Ines Pohl/Iddi Ssessanga/ https://p.dw.com/p/3Jd6v

Mhariri: Daniel Gakuba