1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Vurugu Afrika Kusini zaharibu ndoto ya Afrika

5 Septemba 2019

Afrika Kusini imekumbwa na wimbi jengine la vurugu za chuki dhidi ya wageni. Makali ya vurugu hizo yameelekezwa kwa wadhaifu zaidi miongoni mwa wadhaifu. Ni mapambano mabaya ya ugawaji wa raslimali, Claus Staecker.

Südafrika Xenophobie Rassismus Unruhen
Picha: Getty Images/G.Guercia

Tena na tena mashambulizi hayo yanawalenga wageni nchini Afrika Kusini: Dhidi ya Makwerekwere milioni nne kama walivyozowea kuwaita. Milioni nne wanaotafuta maisha kusini mwa Afrika. Kama ilivyo kwa bara la Ulaya, uhamiaji limekuwa suala tete.

Inachopitia Afrika Kusini mara kwa mara - kuanzia 2008 na 2015 ni mapambano ya ugawanyaji wa raslimali katika ngazi ya chini kabisaa ya kiuchumi. Kwa kulinganisha na Ulaya hata hivyo, wengi wanaokwenda Afrika Kusini ni watafutaji wenye elimu  wanaokwenda huko kujaribu habati yao. 

Mara nyingi wanakuwa na mafanikio makubwa kuliko Waafrika Kusini wenyewe, ni wepesi, wajanja, wanao uzoefu mkubwa na zaidi ya yote, wako tayari kuteseka. Mtu yeyote anaelaazimika kuhudumia familia yake katika taifa jirani lililofeli la Zimbabwe, hawezi kupinga mazingira mabaya ya kazi na mishahara midogo.

Wazimbabwe ambao ndiyo kundi kubwa zaidi la wahamiaji, wanahitajika sana kwa sababu wanalalamika kidogo na wanazungumza Kiingereza kizuri cha biashara. Wanaweza kuhesabu, kusoma na kuandika. Wanapatiwa haraka majukumu ya unyampara na usimamizi, wakati wenzao wenyeji huzichukulia kazi mara nyingi kama sheria ya mirathi.

Mkuu wa Idhaa za Kiafrika wa DW Claus Staecker.

Hata katika sekta isiyo rasmi ambayo inawahudumia nusu ya raia wa Afrika Kusini, maduka ya Wasomali, Wapakistan au Wanigeria mara nyingi huwa na mafanikio zaidi kuliko maduka ya Spaza ya Waafrika Kusini wa kawaida. Na wakati huo huo Wanigeria hutengeneza pesa nyingi kutokana na biashara ya madawa na madanguro.

Na hili ndiyo hasa limeelezwa kuwa chanzo cha machafuko ya sasa katika mji mkuu Pretoria: Dereva Taxi wa Afrika Kusini aliuawa na wauza madawa wa Kinigeria. Uvumi unatosha tu kuwasukuma raia wenye hasira kwenye vitendo vya vurugu. Na kuna hasira zaidi kwa sababu raia zaidi ya milioni 8 wa Afrika Kusini hawajui namna ya kuzihudumia familia zao.

Mchanganyiko wa vurugu na husda ya kijamii

Hiki ni kisasi cha njia tatu: Kwanza kwamba chama tawala cha Africa National Congress ANC kimetoa ahadi za ukombozi zisizotimia; pili serikali ya Jacob Zuma iliudidimiza uchumi; na tatu mfumo wa elimu umepiga hatua kidogo katika kutoa vigezo vinavyohitajika vya soko la msingi la ajira.

Jambo jengine muhimu ni kwamba serikali inaonekana kana kwamba imesalimu amri kwa vurugu, ambazo zimegeuka jambo la kawaida sasa. Kwa mfano vifo vitano au saba katika vurugu ni jambo la kawaida nchini Afrika, ambako takwimu zinaonyesha kuwa watu 57 huuawa nchini humo kila siku. 

Katika mji wa Cape Town, ambako wasomi wa kiuchumi na kisiasa wa bara la Afrika wanakutana kwa ajili ya mkutano wa jukwaa la kiuchumi, maelfu waliandamana jana kupinga siyo chuki dhidi ya wageni, bali vurugu dhidi ya wanawake. Imetosha, walisema -kufuatia visa vya karibuni vya uhalifu wa kubaka, utendaji mbaya na mauaji.

Mjini Cape Town jeshi tayari limepelekwa kuzuwia vita vya umwagaji damu vya magenge, baada ya polisi kushindwa. Kwa miongo kadhaa matumizi ya vurugu yamekuwa sehemu ya utamaduni wa Afrika Kusini, na yanaelekeza kwenye kushindwa kwa serikali. Hata madai kwamba wageni ndiyo wanahusika na uhalifu wote hayajibiwi ipasavyo na serikali. Hisia za chuki dhidi ya wageni zinavumiliwa ama kimya kimya au hata kutetewa waziwazi.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alau amepata maneno sahihi. Tayari kuna mpango kazi wa kitaifa dhidi ya vurugu za chuki dhidi ya wageni. Lakini karatasi ina subira - na Waafrika hawana tena subira.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW